Ahukumiwa jela kwa kuchota fedha akaunti ya mume wake

NA MWANDISHI WETU

AFISA Utamaduni Manispaa ya Lindi mkoani Lindi,Mwanamama Makalaghe Shekhalaghe amehukumiwa kutumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani au kulipa faini shilingi milioni saba baada ya kupatilana na hatia ya wizi wa shilingi 198,750,000 kutoka katika akaunti ya marehemu mume wake.

Pia Mahakama hiyo imeamuru kuchukuliwa kwa nyumba ya mshtakiwa Makalaghe iliyopo Msavu mkoani Morogoro na kuingizwa katika shauri la Mirathi namba 23 ya mwaka 2022.

Hukumu hiyo imesomwa Juni hadi 30, 2023 na Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate wa Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Kabate amesema, upande wa mashtaka kupitia mashahidi wake wamethibitsha pasipo kuacha shaka kuwa mshtakiwa ametenda kosa la wizi.

"Katika hukumu hii nimeangalia kifungu cha 258 na 265 vya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022 ambapo vifungu hivyo vinaeleza wazi wizi ni nini na mazingira gani ambayo yanatafsiriwa kama wizi."

Amesema, pia ushahidi uliotewa na wa mashahidi wanne wa upande wa mashitaka umeeleza jinsi ambavyo fedha ilikuwa ikitolewa benki na mshitakiwa baada ya kifo cha mume wake huku pia mshitakiwa mwenyewe akikiri kutoa na kutumia fedha kwa matumizi binafsi na kutoa sadaka katika Masjid Huddah mkoani Lindi.

Akiendelea kusoma hukumu hiyo Kabate amsema, kukiri kwa mshtakiwa na ushahidi wa taarifa za kibenki Mahakama imeona haina maswali ya ziada ya kujiuliza juu ya ukweli kuwa mtuhumiwa aliiba kiasi hicho cha fedha.

Aidha, ameongeza kuwa, kutokana na utetezi wa mshatakiwa alioutoa kabla ya hukumu kuwa sehemu ya fedha alizoiba alizitoa kama sadaka katika masjidi na shahidi wake alieleza jinsi ambavyo walinufaika na msaada huo mahakama imeona impunguzie adhabu.

Hata hivyo, kabla ya kusomwa kwa adhabu hiyo, mahakama iliwauliza upande wa mashtaka kama walikuwa na lolote la kusema ndipo wakili wa serikali, Agnes Mtunguja akasema, "Mheshimiwa hatuna kumbukumbu za makosa ya nyuma dhidi ya mshtakiwa ila tunaiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na kwa jamii inayomzunguka."

Katika utetezi wake, mshtakiwa ameiomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ana familia kubwa inamtegemea yeye, baba yake ni mzee anaumwa figo pia analea watoto yatima wanne na yeye pia ni mgonjwa anasumbuliwa na pumu.

"Nimesikiliza hoja za pande zote mbili ila hakuna ubishi kuwa kuna sehemu ya pesa shilingi milioni 198 ilitolewa msaada na sadaka msikitini Lindi ila mahakama inakuhumumu kutumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani au kulipa faini ya shilingi milioni saba,"amesema Hakimu Kabate.

"Pia katika harakati za kutafuta shilingi milioni 198 iweze kurudi, nyumba ya mshtakiwa iliyopo Msamvu mkoani Morogoro iwe sehemu ya mirathi na kama mshtakiwa anadanganya kuhusu uwepo wa nyumba hiyo basi akamatwe na kushtakiwa mahakamani,"alifafanua Hakimu huku Makalaghe akifanikiwa kulipa faini na kaachiwa huru.

Katika kesi hiyo inadaiwa kuwa kati ya Januari mwaka 2020 na Juni 2020 maeneo tofauti katika Mkoa wa Dar es Salaam mshitakiwa aliiba shilingi milioni 198,750,000 kutoka katika akaunti ya marehemu mume wake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news