Amezikwa yuko hai

NA LWAGA MWAMBANDE

JULAI 15,2023 mwanzilishi wa Kampuni ya Business Times Limited (BTL) yenye magazeti ya Business Times, Majira, Spoti Starehe, Sanifu, Dar Leo na Maisha, Rashidi Mbuguni alifariki.

Mzee Mbuguni alifariki akiwa ameacha historia kubwa ya kugusa maisha ya Watanzania wengi kupitia ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.

Ni kupitia, kampuni na miradi mbalimbali shirikishi na aliyoiendesha nchini kwa nyakati tofauti, hivyo kuwa faraja kwa wengi kuanzia mijini hadi vijijini.

Matokeo ya uwekezaji wake yaliwezesha kuwavusha wengi na hata sasa wapo katika ngazi mbalimbali za uongozi ndani ya Serikali, sekta binafsi na nje ya nchi.

Daima, tutakukumbuka na kuyaenzi yote mema uliyotuachia,kiongozi, baba, mlezi wa Watanzania wengi, Rashidi Mbuguni.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema kuwa, licha ya kuzikwa, bado Mzee Rashidi Mbuguni yupo hai. Endelea;


1.Kuna watu wanakufa, na kubaki wako hai,
Kwa sababu maarifa, yao yanabaki hai,
Wengine wakishakufa, kila kitu baibai,
Bwana Rashidi Mbuguni, amezikwa yuko hai.

2.Watu wamesema mengi, kuonesha yuko hai,
Tutazidi sema mengi, ya kwake hayachakai,
Hili jambo la msingi, tufe yetu yawe hai,
Bwana Rashidi Mbuguni, amezikwa yuko hai.

3.Naandika sijivungi, yake mengi yako hai,
Kwa uzito siyapangi, msije mkanidai,
Huyu Mbuguni na Mengi, hatuna cha kuwadai,
Bwana Rashidi Mbuguni, amezikwa yuko hai.

4.Liondoka Nyaulawa, akabakia Mbuguni,
Na kule Mengi katwaliwa, wanahabari nchini,
Ubunifu lojaliwa, wa manufaa nchini,
Bwana Rashidi Mbuguni, amezikwa yuko hai.

5.Sitaki zunguka sana, huyu baba kumweleza,
Eneo nimeliona, jinsi alitubariki,
Wengi unaowaona, toka huko tulitiki,
Bwana Rashidi Mbuguni, amezikwa yuko hai.

6.Miaka mwanzo tisini, hivi nani hakumbuki,
Vyombo habari nchini, serikali limiliki,
Ni vichache kama nini, wengine walimiliki,
Bwana Rashidi Mbuguni, amezikwa yuko hai.

7.Akatokeza Mbuguni, vyombo habari kushika,
Ni maarufu nchini, habari viliandika,
Waliokuwa nyumbani, ajira wakazidaka,
Bwana Rashidi Mbuguni, amezikwa yuko hai.

8.Lile gazeti Majira, nchi ilitikisika,
Business T. kwa bora, uchumi ulichambuka,
Dar Leo lipe kura, alasiri likitoka,
Bwana Rashidi Mbuguni, amezikwa yuko hai.

9.Ni BTL Kampuni, makubwa iliyaweza,
Uchapaji kiwandani, ajira iliongeza,
Ya kwake na ya kigeni, magazeti liburuza,
Bwana Rashidi Mbuguni, amezikwa yuko hai.

10.Masuala ya uchumi, tafiti aliziweza,
Yeye kwa wake usomi, mengi aliendeleza,
Midahalo ya kisomi, kwa kweli alichagiza,
Bwana Rashidi Mbuguni, amezikwa yuko hai.

11.Maisha unawaona, watu wengi wanaweza,
Kikazi walipambana, kuwalipa aliweza,
Historia taona, vema wanavyomweleza,
Bwana Rashid Mbuguni, amezikwa yuko hai.

12.Tuige mfano wake, kwa mazuri kueneza,
Tuzifwate nyayo zake, kwa yetu kujiongeza,
Na wengine wainuke, wakizidi kujiweza,
Bwana Rashidi Mbuguni, amezikwa yuko hai.

13.Pole sana familia, kweli kifo chatuweza,
Nao wenye tasnia, kweli mmejieleza,
Twaridhika tunalia, baba mwendo kamaliza,
Bwana Rashidi Mbuguni, amezikwa yuko hai.

14.Matarajio makubwa, mikoba wataiweza,
Watoto sasa wakubwa, ya baba kuendeleza,
Maeneo ya kukabwa, yote ya kuyamaliza,
Bwana Rashidi Mbuguni, amezikwa yuko hai.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news