Dkt.Mwamba aipa changamoto jumuiya ya Kimataifa kuisaidia Afrika kutekeleza SDGs

NA BENNY MWAIPAJA
New York

BARA la Afrika limeitaka Jumuiya ya Kimataifa kuweka nguvu ya pamoja kulisaidia Bara hilo kukabiliana na changamoto mbalimbali zitokanazo na athari za UVIKO-19, mabadiliko ya tabianchi pamoja na mizozo ya kivita inayotishia ustawi wa nchi mbalimbali kiuchumi na kijamii na kukwamisha kasi ya utekelezaji wa ajenda ya Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, akihutubia wajumbe wa Jukwaa la Juu la Siasa la Umoja wa Mataifa kwa niaba ya Umoja wa Afrika, ambapo Tanzania ni Mwenyekiti wa Umoja huo kwa mwaka 2023, Jijini New York, nchini Marekani.

Wito huo umetolewa jijini New York nchini Marekani na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt.Natu El-maamry Mwamba, wakati akihutubia wajumbe wa Jukwaa la Juu la Siasa la Umoja wa Mataifa kwa niaba ya Umoja wa Afrika, ambapo Tanzania ni Mwenyekiti wa Umoja huo kwa mwaka 2023.

Dkt. Mwamba alisema kuwa changamoto hizo zimekuwa kikwazo katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 na kuwasukuma watu wengi katika lindi la umasikini na kutaka hatua madhubuti na za haraka zichukuliwe kukabiliana na hali hiyo.
Alisema kuwa Bara la Afrika limejaliwa kuwa na rasilimali nyingi za jua, upepo, maji na jotoardhi na kutolea mfano wa nishati jua ambayo inauwezo wa kuzalisha umeme wa terawatts 10 unaoweza kutosheleza mahitaji na kuwezezesha upatikanaji wa nisahati safi itakayookoa mazingira.

“Katika uhusiano huu, Bara la Afrika linasisitiza umuhimu wa kuhakikisha nishati safi na nafuu kwa wote inapatikana ambapo hamasa ya uwekezaji zaidi inahitajika katika maeneo mengi, ikiwa ni pamoja na uwekezaji kidigitali, teknolojia bunifu na sekta nyingine muhimu,” alisema Dkt. Natu Mwamba.
Aidha, alisema kuwa uwekezaji katika sekta ya maji safi na salama pamoja na usafi wa mazingira mijini na vijijini ni suala muhimu ili kujenga jamii yenye afya na ustawi na kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuweka kipaumbele katika mipango inayolenga kuimarisha huduma hiyo ya maji kwa wananchi.

Kuhusu Viwanda, Dkt. Natu Mwamba, alisema kuwa sekta hiyo ni muhimu kwa ajili ya kukuza uzalishaji wa bidhaa na huduma pamoja na kuwa chanzo cha ajira ya uhakika hususan kwa vijana na alitoa wito kwa mashirika na kampuni mbalimbali za kimataifa kuwekeza mitaji na teknolojia barani Afrika.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, akihutubia wajumbe wa Jukwaa la Juu la Siasa la Umoja wa Mataifa kwa niaba ya Umoja wa Afrika, ambapo Tanzania ni Mwenyekiti wa Umoja huo kwa mwaka 2023, Jijini New York, nchini Marekani.

“Fursa za kiuchumi zinazotolewa na sekta ya viwanda huchochea ujasiriamali na maendeleo ya biashara, mabadiliko ya kiteknolojia, na kuongeza ufanisi wenye tija, kukuza maendeleo na mageuzi ya kiuchumi yanayojiendesha yenyewe,”alisema Dkt. Mwamba

Dkt. Mwamba alisema pia kuwa kuna umuhimu wa kuboresha maeneo huru ya biashara katika Bara la Afrika ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa zitakazoongezwa thamani lakini pia kuongeza mauzo nje ya nchi, kupatikana kwa fedha za kigeni na kukuza uchumi wa nchi za Bara hilo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, (kushoto) akiwa katika Mkutano wa Jukwaa la Juu la Siasa la Umoja wa Mataifa kabla ya kuhutubia Jukwaa hilo kwa niaba ya Umoja wa Afrika, ambapo Tanzania ni Mwenyekiti wa Umoja huo kwa mwaka 2023, Jijini New York, nchini Marekani. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Eng. Anthony Sanga. 

Kuhusu Tanzania, Dkt. Mwamba alisema kuwa Serikali imejiimarisha kwa kuhakikisha kuwa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yanafikiwa kwa kishindo ifikapo mwaka 2030 ambapo juhudi kubwa zimeelekezwa katika kuimarisha uchumi; huduma za jamii pamoja na hifadhi ya jamii.

“Serikali itandelea kuweka kipaumbele katika uwekezaji katika sekta za ustawi wa kijamii, ujuzi na uwezo wa wananchi wake kujikwamua kiuchumi, hasa kwa vijana, kuendeleza haki za wanawake na wasichana na kukuza ushirikishwaji na wenye maana kwa makundi yote ya watu wakiwemo walio hatarini zaidi,” aliongeza Dkt. Mwamba.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, (kushoto) akiwa katika Mkutano wa Jukwaa la Juu la Siasa la Umoja wa Mataifa kabla ya kuhutubia Jukwaa hilo kwa niaba ya Umoja wa Afrika, ambapo Tanzania ni Mwenyekiti wa Umoja huo kwa mwaka 2023, Jijini New York, nchini Marekani. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Eng. Anthony Sanga.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha, New York, Marekani).

Dkt. Mwamba alisisitiza kuwa Serikali inatambua ipasavyo jukumu muhimu la teknolojia ya kidijitali na uvumbuzi katika kukuza ukuaji wa uchumi na hatimaye kufikia matokeo yanayotarajiwa ya SDGs. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news