Dkt.Mabula amshukuru Rais Dkt.Samia

NA MUNIR SHEMWETA
Ilemela

MBUNGE wa Jimbo la Ilemela mkoani Mwanza ambaye ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo.
Dkt.Mabula ametoa shukrani hizo leo Julai 18, 2023 jijini Mwanza wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilemela kwa kipindi cha mwaka 2020-2022 kwenye mkutano maalum wa wajumbe wa CCM wilayani humo.

Kwa mujibu wa Dkt.Mabula, utekelezaji huo wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ni ya kipindi cha Novemba 2020 hadi Desemba 2022 ambapo taarifa ya mapokezi ya fedha imegusa kipindi cha miaka miwili ya utendaji wa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa katika utoaji wa fedha za miradi ya maendeleo katika Jimbo la Ilemela.
Sehemu ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Ilemela wakifuatilia uwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya chama hicho 2020-2022 leo Julai 18, 2023 jijini Mwanza.

"Hakika tunajivunia kuwa na rais mwenye maono mwenye kujali ustawi wa watu anaowaongoza kwa kuhakikisha huduma za jamii zinawafikia Watanzania wote kwa wakati,"amesema Dkt.Mabula.

Kwa mujibu wa Mbunge huyo wa Ilemela, katika kipindi cha miaka miwili Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela hadi kufikia Machi 2023 imepokea zaidi ya shilingi bilioni 46.089 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo. 

Ameitaja miradi ya maendeleo iliyotekelezwa kwa ufanisi katika jimbo lake kuwa ni pamoja na sekta ya ardhi, afya, elimu, maji, miundommbinu, uvuvi, pamoja na masoko na biashara.

Akielezea kuhusiana na sekta ya ardhi anayoisimamia, Dkt.Mabula amesema katika kutekeleza azma ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi kupitia fedha za mkopo zilizotolewa na Rais Samia, Manispaa ya Ilemela imekuwa mnufaika mkubwa wa fedha hizo kati ya halmashauri 58 zilizonufaika na mkopo huo nchini.

Amebainisha kuwa, kupitia mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi Manispaa ya Ilemela imepima viwanja katika maeneo ya Buswelu, Nyafla, Sangabuye,Igalagala na Ilekelo ambapo mradi umekamilika na viwanja 3,254 vimepimwa kwenye ekari 900 zilizopimwa na kugharimu kiasi cha shilingi 3,589,774,000 kutoka serikali kuu.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Sophia Mjema akizungumza mara baada ya kukabidhi pikiki zilizotolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemelia Angeline Foundation, Mhe. Dkt.Angeline Mabula (wa pili kushoto) wakati wa Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Ilemela kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho 2020-2022 leo Julai 18,2023 jijini Mwanza.

‘’Mpaka sasa manispaa imefanikiwa kuuza viwanja katika mradi husika kwa asilimia 70 na kufanikiwa kurejesha mkopo kwa asilimia 100,’’amesema Dkt.Mabula.

Kwa upande wake Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa aliyekuwa mgeni maalum kwenye mkutano huo Sophia Mjema alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Dkt. Angeline Mabula kwa kufanikisha utekelezaji Ilani ya chama hicho katika jimbo lake.

Akihutubia mkutano huo uliohudhuriwa pia na Waziri wa Ulinzi Innocent Bashungwa, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega, Naibu Waziri Kilimo Anthony Mavunde na Naibu Waziri Malisili na Utalii Mary Masanja, Mjema aliwataka viongozi wa CCM kuanzia ngazi ya shina hadi wilaya kuhakikisha wanawaeleza wananchi yote yaliyoahidiwa na kutekelezwa kupitia ilani ya CCM.

"Tunapoenda kutekeleza haya ni lazima tuwaeleze wananchi tuliyoahidi kwa kutoa taarifa tulipotoka, tulipo na tunapoelekea na hapo ndiyo tunahakikisha ilani inatekelezwa ipasavyo,"amesema Sophia Mjema.
Sehemu ya pikipiki zilizotolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela mkoani Mwanza, Dkt.Angeline Mabula kupitia Angeline Foundation wakati wa Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Ilemela kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho 2020-2022 leo Julai 18, 2023 jijini Mwanza. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).

Katika kipindi cha miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan, mbali na mambo mengine Halmashauri ya Ilemela imepata mafanikio mbalimbali kama vile kufungua shule tano mpya za sekondari, kukamilisha na kufungua zahanati tatu, kukamilisha ujenzi wa kituo cha afya kayenze pamoja na majengo muhimu ya hospitali ya wilaya na huduma za wagonjwa wa nje zinazotolewa.

Aidha, Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Dkt.Mabula kupitia taasisi yake ya Angeline Foundation alitoa pikipiki 16 kwa watendaji wa jimbo lake zilizokabidhiwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi, Sophia Mjema ambapo pia mbunge huyo wa Ilemela atatoa basi kwa ajili ya kusaidia shughuli za Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news