Halmashauri zitambue mahitaji ya walimu wa michezo

NA ADELADIUS MAKWEGA 

WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Balozi Dkt. Pindi Chana amesema kuwa sasa halmashauri zote nchini na waajiri wote wanayo fursa kubwa ya kuwapata wataalamu wa michezo wanaohitimishwa kila mwaka katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kilichopo Kwimba mkoani Mwanza. 
Hayo yamesemwa na Balozi Dkt. Chana alipohudhuria mahafali ya 12 ya Chuo hicho Julai 15, 2023 ambapo alikuwa mgeni rasmi.

“Naziomba halmashauri zote zitambue mahitaji ya walimu wa michezo katika maeneo yao, ili mahitaji hayo yawasilishwe mamlaka husika na nafasi hizo ziweza kujazwa mapema mara baada ya mawasilisho yao.” 
Akiendelea kutoa hotuba yake Waziri. Dkt. Pindi Chana aliwataka wahitimu hao wakaitumie elimu hiyo ya michezo ipasavyo ambayo hivi sasa imekuwa bidhaa kwa Watanzania na wizara yake itaendelea kutoa ushirikiano wote kwa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya na wahitimu wake popote walipo kwa ushirikiano na wadau wote wa tasnia ya michezo. 
“Mara kwa mara nimeendelea kuwashukuru wafadhili wa vilabu vyetu vyote vikubwa na vidogo akiwamo MO na GSM na niendelee kusema kuwa tunavyo vilabu vingi katika mikoa na tunayo michezo mingi katika wilaya zetu, hivyo wizara inatoa wito kwa sekta binafsi tushirikiane tuone kwa namna gani tunakuza tasnia hii ya michezoi nchini.” 

Waziri Chana alisema kuwa Bajeti ya 2023/2024 imepitishwa na Bunge letu, hivyo kubwa ni kuimarisha michezo, huku akitoa wito kwa Halmashauri zote nchini kulinda maeneo yote ya michezo ili kutoa nafasi ya Watanzania kuweza kushiriki katika michezo, maeneo hayo lazima yawe na hati na kuwe na programu mbalimbali za michezo kila siku.
Wakizungumza mara baada ya kupokea vyeti vyao katika mahafali hayo mhitimu Isidori Israel ambaye amehitimu Stashahhada ya Michezo amesema, 

“Naashukuru sana kwa kumuona Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana kwa kuwa mgeni rasmi katika mahafali haya na hilo litabakia katika historia ya maisha yangu. Uwepo wa Waziri Chana una maana kubwa kwangu, una maana nzito kwa tasnia niliyosomea na maana kubwa kwa taifa langu la Tanzania.” 
Kwa upande wake mhitimu Lucy Malisa alisema, “Nashukuru kwa kuhitimu kwangu Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, huko kumefungua milango mingi kwangu na katika michezo, hivyo nashukuru Mungu kwa kuhitimu salama na ninatarajia kujiendeleza zaidi katika tasnia hii ya michezo kwa ngazi ya shahada.”

Mahafali hayo yalihudhuriwa na viongozi kadhaa akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini na viongozi wengine wa chama na serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news