Huyu ndiye mgeni wetu, karibu nchini Rais Novák kutoka Hungary

NA GODFREY NNKO

LEO Julai 17, 2023 Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajia kupokea ugeni muhimu wa Rais wa Jamhuri ya Hungary, Mheshimiwa Katalin Éva Veresné Novák.

Rais wa Hungary,Mheshimiwa Katalin Éva Veresné Novák (katikati) akila kiapo Machi 10,2022 wakati wa hafla ya kuapishwa kwake katika kikao cha wajumbe wote cha Bunge la Hungary jijini Budapest, Hungary.(Picha na MTI/Szilard Koszticsak).

Ujio wa Mheshimiwa Rais unatazamwa kwa jicho pana zaidi la diplomasia ya uchumi kati ya Tanzania na Hungary kutokana na namna ambavyo taifa hilo lilivyopiga hatua mbalimbali kupitia rasilimali kadhaa ilizonazo.

Hungary haina rasilimali za madini na mafuta, lakini inajivunia uzoefu wake mkubwa katika kilimo, elimu, maendeleo ya rasilimali watu, sayansi, teknolojia,uvumbuzi na sekta ya utalii.

Ziwa Balaton, linalochukua zaidi ya kilomita za mraba 598, ni moja wapo ya vivutio vikubwa vya watalii nchini humo. Kina cha wastani cha ziwa ni mita mbili hadi tatu, hivyo maji hupata joto haraka wakati wa kiangazi zikiwemo hifadhi 10 maarufu za Taifa hilo.

Miongoni mwa hifadhi hizo ambazo ni vivutio vikubwa vya utalii duniani ni Hortobágy National Park,Kiskunság National Park,Bükk National Park,Aggtelek National Park,Fertő-Hanság National Park,Danube-Drava National Park.

Nyingine ni Körös-Maros National Park,Balaton Uplands National Park,Danube-Ipoly National Park na Őrség National Park.

Taifa hilo ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya tangu mwaka 2004 na mwanachama wa Eneo la Schengen tangu mwaka 2007, Hungary ina idadi ya watu wapatao 9.71 milioni (2021) kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia.

Schengen ni nini?

Eneo la Schengen ni kundi la nchi za Ulaya ambazo zimefuta mipaka yao. Hii ina maana kwamba unaweza kusafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine bila kuonesha hati yako ya kusafiria mara kwa mara.

Aidha, kupitia mfumo huo unaweza kusafiri kwa urahisi kutoka nchi moja hadi nyingine, mfumo ambao unakuwezesha kusafiri kupitia Ulaya kwa urahisi.

Wanachama wa nchi za Schengen walikubaliana juu ya harakati huru za watu. Hii ina maana kwamba udhibiti wa mipaka ya kitaifa ndani ya eneo la Schengen umefutwa, ili watu wasio na visa au hati nyingine za kusafiri waweze kusafiri kihalali kutoka nchi moja hadi nyingine ndani ya eneo la Schengen.

Mkataba wa Schengen ulitiwa saini na nchi tano mwaka 1985 na tangu wakati huo imepanuka hadi nchi 27 za sasa huku nchi mpya zaidi ya Schengen ni Croatia.

Taifa hilo lilijiunga na eneo la Schengen Januari Mosi,2023. Wakati nchi katika ukanda wa Schengen zikihifadhi mamlaka yao, zinashiriki majukumu fulani ya usalama na uhamiaji kwa ustawi bora wa ukanda huo.

Novák ni nani?

Huyu ni mwanasiasa wa Hungary anayehudumu kama rais wa sasa wa Hungary, baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi wa urais wa 2022.

Novák ndiye mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa urais, pamoja na rais mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya Hungary, aliyechaguliwa akiwa na umri wa miaka 44.

Rais huyo alizaliwa Septemba 6,1977 akiwa ni mwanachama wa Chama cha Fidesz, kabla ya urais, Mheshimiwa Novák aliwahi kuwa Mbunge wa Bunge la Kitaifa kuanzia mwaka 2018 hadi 2022, na Waziri wa Mambo ya Familia katika ya Awamu ya Nne ya Viktor Orbán kutoka 2020 hadi 2021.

Rais huyo ambaye kitaaluma ni mchumi na mwanasheria akiwa na uwezo wa kuzungumza kwa ufasaha lugha ya Kifaransa,Kiingereza, Kijerumani na Kihispania ni mama wa watoto watatu.

Mumewe ni mwanauchumi István Veres, ambaye ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Soko la Fedha na Fedha za Kigeni katika Benki Kuu ya Hungary (MNB).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news