Simba aliyetaka kumuua askari auawa huko Iringa

IRINGA-Kikosi cha kutafuta simba kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) kilichokuwa Kijiji cha Ilamba Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa kimefanikiwa kumuua simba dume mmoja.

Tukio hilo limetokea Julai 16,2023 ambapo simba huyo anadaiwa alimvamia askari na kumjeruhi wakati akidhibitiwa kwa kulazwa usingizi ili arudishwe hifadhini.

Afisa Uhusiano Mkuu wa TAWA,Vicky Kamata amesema, “Simba hawa walikuwa wawili ambapo mmoja alikimbia akabaki mmoja.

"Katika harakati za kumdhibiti ili wamchome sindano ya usingizi na kumrudisha Hifadhi ya Ruaha, simba huyo alitoka vichakani kwa hasira na kumvamia askari CR III Charles Mafuru na kumjeruhi kichwani na mkono.

“Askari mwingine alilazimika kumpiga risasi ya moto simba huyo baada ya kuona amemuangusha Afande Charles na amekaa juu yake akijiandaa kumshambulia shingoni na kumuua.

"Baada ya askari kumuua simba walimpeleka mgonjwa Hospitali ya Wilaya ya Kilolo ambako alipewa matibabu na kuruhusiwa, hali yake inaendelea vizuri.

“Washiriki wa doria hiyo iliyofanikisha kumuua simba ni Dkt.Mwakyusa kutoka TAWA, Dkt.Emmanual kutoka TAWIRI, CR III Charles Mafuru kutoka TAWA, CR III Dologo Nkolo kutoka TAWA, CR III Paul Masatu kutoka TAWA na CR III Daniel Isangya kutoka TAWA.

“Matukio ya simba kuua mifugo kwa mara ya kwanza yalijitokeza Juni 13, 2023 eneo la Kalenga Iringa Vijijini na tangu muda huo wamesababisha vifo vya ng’ombe 36, nguruwe 10, mbuzi 12 na kondoo watano, hakuna tukio la mwananchi kuvamiwa na simba hao.

“Zoezi la kuwasaka simba hao linaendelea ambapo jana kulionekana alama za simba na mtoto wake eneo la Ihemi, ufuatiliaji ulibaini wameelekea Ifunda huko Wilaya ya Mufindi,"amefafanua kwa kina Afisa Uhusiano Mkuu wa TAWA,Vicky Kamata.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news