NA FRESHA KINASA
KIONGOZI wa mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa kwa mwaka 2023, Abdallah Shaibu Kaim ametoa pongezi kwa Mbunge wa Jimbo la Butiama ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Jumanne Sagini,watendaji wa halmashauri hiyo na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mheshimiwa Mosses Kaegele kwa usimamizi wao madhubuti na kuhakikisha miradi ya maendeleo wilayani humo imetekelezeka kwa ubora na kwa viwango vinavyostahili kwa manufaa ya wananchi.

Aidha, Julai 6, 2023 wakati mwenge huo ukikabidhiwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kiongozi huyo wa mbio za mwenge amesema;

"Nampongeza pia Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mheshimiwa Moses Kaegele, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Mhe.Peter Wanzagi, Mkurugenzi, Bi. Aziza Baruti, Chifu Japhet Wanzagi na wengine mlioshiriki kwa namna moja au nyingine kuhakikisha miradi hii inakuwa na ubora unaotakiwa,"alisema Kaim.

Pia, Mheshimiwa Sagini amewashukuru Viongozi wa Halmashauri ya Butiama kwa ushirikiano wao wa dhati katika kuhakikisha wanawatumikia wananchi kuwaletea maendeleo.
Sagini amesisitiza Watanzania kuendelea kuiunga mkono Serikali kwa dhati kwani imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo ambayo inatija katika nyanja mbalimbali na kwamba Serikali ya Awamu ya sita imehakikisha inawagusa Wananchi kwa kuwaletea maendeleo Jambo ambalo linapaswa kupongezwa na kila mwananchi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mhe.Moses Kaegele ameeleza kuwa ,katika Mkesha wa Mwenge wa Uhuru uliofanyika katika Uwanja wa Mwenge Butiama jumla ya watu 355 walifanikiwa kupimwa maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) wanawake wakiwa 99 na wanaume 256 ambapo waliokutwa na maambukizi ni watu watatu, wanaume wakiwa wawili na mwanamke mmoja.

Kauli mbiu ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 inasema “Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Viumbe hai na Uchumi wa Taifa.”
Hata hivyo, Mwenge wa Uhuru tayari umekabidhiwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwa ajili ya kuendelea na mbio zake mkoani Mara.