Kwa nini Serikali iliipa kipaumbele DP World miongoni mwa kampuni saba?

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi,Mheshimiwa Prof. Makame Mbarawa amesema,licha ya Serikali kuendeleza juhudi mbalimbali za maboresho ya bandari nchini bado ufanisi katika utoaji huduma haujafikia viwango vinavyotakiwa Kimataifa.
Amesema, hali ya ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam na nyingine zinazoendeshwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) upo chini na hali hiyo inaonekana katika utendaji wa kila siku wa bandari nchini ikiwemo ukusanyaji wa mapato.

"Ufanisi huu mdogo wa Bandari ya Dar es Salaam umetokana na changamoto mbalimbali, ya kwanza ni kukosekana kwa mifumo ya kisasa ya TEHAMA (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano).

"Ya pili kutokuwepo kwa maeneo ya kutosha ndani na nje ya bandari ya kuhifadhia shehena za mizigo pamoja na maegesheo ya kutosha ya kuegeshea meli.

"Na tatu kukosekana kwa mitambo ya kutosha na ya kisasa ya kuhudumia shehena ambayo inabadilika mara kwa mara kutokana na kubadilika kwa teknolojia mpya ambayo ina gharama kubwa za uwekezaji;

Mheshimiwa Waziri Prof.Mbarawa ameyabainisha hayo Julai 14, 2023 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi baina ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

Athari

"Athari za kutokuwa na ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam ni pamoja na meli kusubiri muda mrefu nangani ambapo kunasababisha kuongezeka kwa gharama kutumia Bandari ya Dar es Salaam.

"Kwa mfano gharama za meli kusubiri nangani kwa siku moja ni takribani dola za Kimarekani 25,000 sawa na shilingi za Kitanzania milioni 58.
"Pili meli kutumia muda mrefu,kupakia na kupakua shehena kwa wastani wa siku tano ikilinganishwa na siku moja inayokubalika Kimataifa.

"Na tatu, meli kubwa kutokuja katika Bandari ya Dar es Salaam kutokana na kuchukua muda mrefu na hivyo kuongeza gharama ya kutumia Bandari ya Dar es Salaam.

"Kwa mfano kwa sasa meli zinazohudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam zina uwezo wa kuingiza meli zinazopakia makasha kati ya 2,400 mpaka 2,800.

"Meli kama hizi zinachukua takribani siku tano mpaka siku sita kama nilivyosema, bandari zetu za jirani zina uwezo wa kuruhusu meli zenye uwezo wa kubeba makasha zaidi ya 4,000, sisi meli zinazokuja hapa, makasha 2,400 mpaka 2,800.

"Kama Bandari ya Dar es Salaam tunataka iweze kuhudumia kama nchi jirani, tunahitaji meli hiyo ihudumiwe kati ya siku 10 mpaka siku 13.

"Athari kubwa sana ya uwezo mdogo wa Bandari yetu ya Dar es Salaam ni kuikosesha nchi mapato makubwa ambayo yangeweza kusaidia katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo inaendelea kutekelezwa hapa nchini."

Walipoanzia

"Ili kutoendelea na hali hii, tangu mwaka 2000 Serikali ya Awamu ya Tatu iliingia mkataba wa upangaji na uendeshaji yaani Lease and Concessions Agreement na Kampuni ya Kimataifa ya Uendeshaji wa Vitengo vya Makasha yaani Hutchison ya Hongkong nchini China ambapo hapa nchini ilikuwa ikifahamika kama TICTS (Tanzania International Container Terminal Services).

"Mkataba huo ulidumu kwa miaka 22 kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2022 na uliipa haki ya kipekee Kampuni ya TICTS kwa ajili ya kuendesha shughuli za kuhudumia makasha katika Gati namba 8 mpaka namna 11 za Bandari ya Dar es Salaam.

"Wakati maeneo mengine yalikuwa yakihudumiwa na Mamlaka ya Bandarai ya Tanzania (TPA). Ukodishaji wa TICTS uliendelea hadi Serikali ya Awamu ya Tatu, Serikali ya Awamu ya Nne, Serikali ya Awamu ya Tano na mpaka Serikali ya Awamu ya Sita.

"Mwezi Desemba, mwaka jana, Serikali ya Awamu ya Sita baada ya kuona mkataba huo hauendani na matarajio ya Serikali kuhusu maslahi mapana ya nchi yetu, iliamua kusitisha mkataba huo.

"Pamoja na hatua hiyo, Serikali imeendelea kutafuta wawekezaji wengine wa kutatua changamoto zilizopo kwrnye bandari kwa ajili ya kuboresha sekta hii muhimu ya uchukuzi katika uchumi wa nchi yetu.

Hatua madhubuti

"Ili kutekeleza azima hiyo, Serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania imechukua hatua madhubuti zilizohusisha kupokea mapendekezo ya wawekezaji wakubwa kwa sekta ya uendeshaji wa bandari duniani.

"Wakiwemo Kampuni ya Hutchison kutoka huko Hong Kong kampuni ambayo ndiyo TICTS, Kampuni ya Port of Singapore Authority kutoka nchini Singapore, DP World ya kutoka UAE (Umoja wa Falme za Kiarabu),Abu Dhabi Port ya kutoka UAE, Adani Ports and Logistics kutoka nchini India.

"Kampuni ya CMA CGM (Compagnie Maritime d'Affrètement (CMA) and Compagnie Générale Maritime (CGM) kutoka Ufaransa pamoja na Kampuni ya APM (Assistant Project Manager) ya huko Denmark.

"Lengo kuu la Serikali ni kufungua masoko ya kimkakati katika eneo la bidhaa na biashara ya usafirishaji ndani ya nchi na kanda zinazotuzunguka.

"Baada ya kufanya mawasilisho wawekezaji hao, pamoja na kupitia sifa zao za Kimataifa na kufanya uchambuzi wa kina, Serikali iliamua kuanzisha majadiliano na Kampuni ya DP World."

Kwa nini DP World?

"Sababu ya kwanza, DP World ina uwezo mkubwa katika uendeshaji wa shughuli za bandari barani Afrika, Asia, Ulaya, Marekani ya Kaskazini, Marekani ya Kusini na Australia. 

"Pili, DP World ina uwezo na utaalamu wa kuchagiza myororo mzima wa usafirishaji kutoka maeneo bidhaa zinatoka mpaka kwa walaji wa bidhaa hizo.

"Na tatu, DP World inamiliki meli zaidi ya 400 za mizigo kupitia Kampuni yake ya P&O hii inaongeza ufanisi mkubwa katika usafirishaji wa mizigo, wawekezaji wengine ambao niliwataja ambao waliwasilisha mapendekezo yao.

"Hutchison ya Hong Kong, PSA Internationla (Port of Singapore Authority) ya Singapore,Abu Dhabi Port ya kutoka UAE,Kampuni ya CMA CGM (Compagnie Maritime d'Affrètement (CMA) and Compagnie Générale Maritime (CGM) ya Ufaransa,Kampuni ya APM (Assistant Project Manager) ya Denmark hazikukidhi sifa za mwekezaji mahiri ambaye anahitajika Bandari ya Dar es Salaam.

"Kwa sababu hayakuwa na uwezo wa uchagizaji wa mnyororo mzima wa usafirishaji wa mizigo kama ilivyoelezwa, kwa upande wa DP World ina uzoefu na utaalamu wa kuchagiza mnyororo mzima wa usafirishaji kutoka maeneo ambayo bidhaa zinatoka mpaka kwa walaji wa bidhaa hizo.

"Pia, ina uzoefu wa uendeshaji wa bandari sita barani Afrika na zaidi ya bandari 30 duniani kote kwa ufanisi mkubwa, vile vile DP World ina uzoefu wa uendeshaji wa logistics hub mbalimbali duniani.

"Kwa mfano kwa sasa DP World inaendesha Kigali Logistics Platform nchini Rwanda, makubaliano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai ni matokeo ya maamuzi ya Serikali kuamua kuvutia wawekezaji mahiri nchini.

"Ambapo wakati wa maonesho ya Dubai Expo 2020 ambayo yalifanyika tarehe 27 Februari 2022 hati za makubaliano yaani Memorandum of Undastanding (MoU) 30 zilisainiwa baina ya taasisi za Serikali za Tanzania na taasisi za Dubai.

"Ikiwemo MoU baina ya TPA na DP World iliyolenga kuanzisha ushirikiano wa uboreshaji, uendeshaji na uendelezaji wa bandari nchini.

"Baada ya hatua hiyo, Serikali iliunda timu ya wataalamu ambayo iliendelea na mazungumzo hadi kusainiwa kwa makubaliano hayo, kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizopo.

"Lengo la makubaliano haya ni kuweka msingi wa makubaliano yaani framework agreement baina ya nchi na nchi ili kuwezesha kuanza kwa majadiliano na kuingiwa kwa mikataba mbalimbali, kama vile mikataba ya nchi wenyeji, upangishaji na uendeshaji wa maeneo ya bandari nchini.

"Aidha, kwa mujibu wa masharti ya makubaliano hayo yanapaswa kuridhiwa na Bunge la Jmahuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Ibara ya 53 (3) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

"Ili utekelezaji wake uweze kuanza, hivyo Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ilianza mchakato wa kupata ridhaa ya Serikali ya kuwasilisha makubaliano haya bungeni kwa ajili ya kuridhiwa."

"Kwa mujibu wa Ibara ya Pili ya Makubaliano haya baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai, lengo lake ni kuweka msingi wa ushirikiano baina ya Serikali mbili kwa maeneo mahususi yaliyoainishwa ndani ya makubaliano hayo husika.

"Rejea kiambatanisho namba moja cha makubaliano,ambayo utekelezaji wake utafanyika kupitia mikataba mahususi baina ya taasisi zilizoainishwa katika makubaliano hayo, kama taasisi tekelezi ambazo ni TPA na DP World.

Serikali ipo huru

"Hivyo, makubaliano haya hayana masharti yanayoifunga Serikali kuhusu maeneo ya ushirikiano yaliyoainishwa pasipokuwepo na mikataba mahususi ya utekelezaji wa miradi itakayojadiliwa na kukubaliwa na pande zote mbili.
"Makubaliano hayo yameainisha awamu mbili za ushirikiano. Awamu ya kwanza, maeneo ya ushirikiano yatajumuisha kuanza kusimamia na kuendesha baadhi ya magati, gati namba moja mpaka namba saba katika Bandari ya Dar es Salaam.

"Kuboresha gati la majahazi na gati la abiria katika Bandari ya Dar es Salaam ili kuvutia vyombo vikubwa zaidi na meli za kitalii kutia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam.

"Pili, kuwekeza katika maeneo yaliyotengwa bandari kavu na maeneo maalumu ya kuhifadhia mazao ya matunda na mazao mengineyo yanayosafirishwa nje ya nchi, kwa sasa mazao ya matunda yanasafirishwa kupitia bandari za nchi jirani.

"Tatu, kufanya uwekezaji katika mifumo ya kisasa TEHAMA ya kuendeshea shughuli za kibandari ili kuongeza ufanisi wa bandari zetu.

"Na, nne kuwajengea uwezo watumishi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ili waweze kutekeleza shughuli za bandari na ufanisi katika maeneo mengine ya bandari nchini."

Awamu ya Pili

"Awamu ya pili ya maeneo ya ushirikiano ni kuongeza thamani ya bidhaa katika maeneo ya viwanda na miundombinu mingine itakayoongeza ufanisi katika kusafirisha bidhaa kutoka nchini.

"Ya pili kuwekeza katika bandari zingine za bahari na maziwa, kama itakavyopendekezwa na Serikali kupitia TPA kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa.

"Tatu, kuwekeza katika vyombo vya usafirishaji wa mizigo ya shehena yaani matishari katika maziwa makuu ili kuunganisha bandari zetu za maziwa makuu na bandari za nchi jirani, kama itakavyopendekezwa na Serikali kupitia TPA.

Wawekezaji wengine

"Ili kutoa fursa kwa wawekezaji wengine, maeneo yafuatayo hayamo kwenye makubaliano kwanza maeneo ya Gati No.8 mpaka Gati No.11 ya Bandari ya Dar es Salaam hayapo, Gati la Mafuta Kurasini namba moja, Gati la Mafuta Kurasini namba mbili na boya la kupokelea mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam hayapo katika makubaliano hayo.
"Tatu, maeneo yote ya awamu ya kwanza ambayo hayatafikiwa muafaka katika majadiliano hayatakuwepom katika mpango huu na mwisho makubaliano haya hayatahusisha Bandari ya Tanga, Mtwara na Bagamoyo.

"Pia, mikataba itakayoandaliwa itaweka bayana kipindi cha utekelezaji wake na ukomo wake, pili muda wa marejeo utawekwa bayana kila mkataba wa mradi husika, hii itategemea mradi husika.

"Tatu, viashiria vya ufanisi vya kiutendaji vitaainishwa kwenye mikataba miradi husika. Nne, uandaaji wa mikataba ya miradi utaandaliwa chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuingatia maslahi mapana ya Taifa.

"Tano, mikataba itakayoandaliwa italinda ajira za wafanyakazi wazawa na kuwajengea uwezo wafanyakazi hao. Sita, mifumo ya TEHAMA itakayosimikwa na DP World itasomana na mfumo wa Serikali.

"Saba, taasisi mahususi za Serikali pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama vitaendelea na utekelezaji wa majukumu yake katika maeneo yote ya bandari nchini."

Manufaa

"Manufaa tutakayoyapata baada ya kuingia makubaliano hayo, kwanza ni kupunguza muda wa meli kukaa nangani muda wa siku tano mpaka saa 24.

"Hii itapunguza gharama za utumiaji wa bandari yetu, matokeo yake itaongeza idadi ya meli zitakazokuja Bandari ya Dar es Salaam kutoka meli 1,569 zinazohudumiwa mwaka 2021/22 mpaka kufikia meli 2,950 ifikapo mwaka 2032.

"Pili,kupunguza muda wa ushushaji wa makasha kutoka siku nne mpaka siku tano za sasa hadi siku mbili. Tatu, kupunguza muda wa uondoshaji wa mizigo bandarini kutoka saa 12 hadi sasa 1 kutokana na uboreshaji wa mifumo ya TEHAMA.

"Nne, kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo kutoka nchi za nje kwenda nchi jirani, kwa mfano kutoka dola za Kimarekani 12,000 mpaka kufikia dola 6,000 kwa kasha moja kwa mizigo inayokwenda Malawi, Zambia au DRC.

"Hii italeta watumiaji wengi kwenye bandari yetu ya Dar es Salaam. Tano, kuongezeka kwa shehena inayohudumiwa kutoka tani milioni 18.4 za mwaka 2021 hadi kufikia tani milioni 47.57 mwaka 2032 sawa na ongezeko la asilimia 158.
"Sita, kuongezeka kwa mapato ya Serikali yatokanayo na kodi ya forodha inayokusanywa kwa shehena inayopitishwa bandarini kutoka trilioni 7.76 za mwaka 2021 hadi kufikia trilioni 26.7 za mwaka 2030 sawa na ongezeko la asilimia 244.

"Saba,kuongezeka kwa ajira zinazotokana na shughuli za bandari kutoka ajira 28,990 za mwaka 2021/22 hadi kufikia ajira 70,907 ifikapo mwaka 2032/33 sawa na ongezeko la asilimia 144.

"Nane, kufanyika kwa maboresho ya maeneo ya kuhudumia shehena za makasha na kuweka mitambo ya teknolojia ya kisasa.

"Tisa, kuendeleza eneo la kuhifadhia mizigo bandari kavu kwa kuweka miundombinu ya kisasa ya kuhudumia aina zote za shehena.

"Kumi, kufanyika kwa maboresho ya magati ya majahazi na magati ya abiria ili kuongeza meli nyingi za kitalii, na kusimika mifumo ya kisasa kwa ajili ya shughuli za bandari na kuunganisha wadau wote wa bandari,"amefafanua kwa kina Waziri Prof.Mbarawa.

Hamza Johari

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Majadiliano kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai juu ya uwekezaji bandarini, Hamza Johari ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafri wa Anga Tanzania (TCCA) amesema,DP World hatamilikishwa ardhi ya Tanzania na badala yake atakodishiwa sehemu ya bandari ili kuongeza ufanisi.

Pia amesema,kwa sasa bado mkataba wa bandari haujasainiwa na kilichopo sasa ni makubaliano ambayo yanajenga msingi wa mkataba ambao utaandaliwa kwa ajili ya kuongoza ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Dubai.
Amesema, iwapo mkataba huo ukianza utekelezaji kwenye Bandari ya Dar es Salaam, italeta mapinduzi makubwa ya kiuchumi kwa manufaa ya Watanzania kupitia mwekezaji huo.

Amesema, suala la uwekezaji wa Kampuni ya DP World halipo kwenye mambo ya muungano wa nchi zinazounda Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), hivyo katiba yao imetoa haki kwa moja ya nchi wanachama kuingia kwenye ushirikiano na nchi yoyote.

Abu Dhabi, Dubai, Ajman, Fujairah, Ras al Khaimah, Sharjah na Umm al Quwain ni falme saba zinazounda UAE ambazo zinadumisha kiwango kikubwa cha uhuru wake.

Mwenyekiti huyo amesema majadiliano hayo tayari yameridhiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuyalinda, hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi.

Katika hatua nyingine, Johari amebainisha kuwa, DP World kabla hajaanza kazi hapa nchini itasajili kampuni ya kitanzania na asilimia 35 za hisa atatoa kwa wazawa.

Amesema, katika Ibara ya 13 ya mkataba wamekubaliana kuwa ni lazima DP World iwaajiri wafanyakazi atakaowakuta na itoe kipaumbele kwa kampuni za ndani na kusaidia kujenga vyuo vya mafunzo. "Awali alikataa tukasema kama hawataki basi, tulifanya hivi ilikuwa lazima tumtishe, lakini baadae alikubali.
 
“Sisi tumeweka kifungu kwamba atakapokuja DP World kwakuwa yeye teknolojia yake ya juu asituletee habari kwamba anapunguza wafanyakazi tumesema lazima ahakikishe anawatunza wafanyakazi atakaowakuta, hivyo Bunge limelinda kwa kuridhia hawawezi kutufanyia kama walivyofanya Djibout.

“DP World hatoleta mitambo chakavu kwa sababu tumeweka viwango vya mitambo na akienda kinyume tutambana, kuhusu kodi tunatarajia TRA akusanye trilioni 26 kwa mwaka, kwani mifumo mingi itaimarishwa na kuonekana,”amesema Johari.

Ameongeza kuwa, katika mkataba wa makubaliano, kuna vipengele vinavyoelekeza DP World kusitishiwa mkataba endapo shughuli zake hazitaendeshwa kwa ufanisi au kukiuka mkataba.

Mwenyekiti huyo amefafanua kuwa,haiuzwi bali inakodishwa kwa DP World kwa muda ambao utawekwa katika mikataba ya utekelezaji itakayoingiwa hivi karibuni ambapo yeye DP World atapewa asilimia nane ya sehemu ya Bandari ya Dar es Salaam na si bandari yote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news