Mambo binafsi kumng'oa Patrick Aussems ndani ya AFC Leopards

NA DIRAMAKINI

KOCHA Patrick Aussems maarufu kama ‘Uchebe’ ambaye aliwahi kuwa Kocha Mkuu wa Simba ya jijini Dar es Salaam ametangaza kuwa, hataongeza mkataba wake ndani ya AFC Leopards kutokana na sababu zake binafsi.

Awali uvumi ulikuwa umeenea kuhusu mustakabali wa Aussems na klabu hiyo, ripoti zikionesha kwamba Leopards inadaiwa fedha na kwamba alidai kulipwa kabla ya kusaini mkataba mpya.

Uamuzi wa Aussems unamaliza muda wake wa mafanikio katika klabu hiyo ya Abaluhya Football Club Leopards Sports Club (AFC Leopards) ya jijini Nairobi nchini Kenya.

"Kwa sababu zangu binafsi sitaweza kuongeza mkataba wangu na AFC Leopards, shukrani kwa wachezaji wangu, wafanyakazi wenzangu, mashabiki wa kipekee kwa miaka miwili iliyopita. Nawatakia Ingwe kila la heri! Asante sana," Aussems ameandika kupitia ukurasa wake rasmi wa Twitter Julai 10, 2023.

Katika kipindi chake akiwa AFC Leopards, klabu hiyo haikuweza kusajili wachezaji mara kwa mara kutokana na kufungiwa kwa uhamisho.

Aussems aliiongoza timu hiyo kumaliza katika nafasi ya saba msimu huu, huku msimu uliopita ikishika nafasi ya sita. Katika msimu wa 2020/21, timu ilifanikiwa kumaliza katika nafasi ya nne.

Kocha Aussems alipokea sifa kwa kuingiza mtindo wa kuvutia wa uchezaji na kubadilisha njia ya Leopards kuukabili mchezo ikiwa dimbani.

Aidha, kabla ya kuinoa AFC Leopards, Aussems alikuwa na taaluma nzuri ya ukocha katika vilabu na timu za kitaifa katika mataif mbalimbali duniani.

Akiwa mbobezi katika ukufunzi wa soka, Aussems aliwahi kufundisha timu kama vile The Capricorn in Reunion na Beaucaire nchini Ufaransa.

Pia aliwahi kuwa mkufunzi Chuo cha Michezo cha Kadji nchini Cameroon kabla ya kujiunga na wafanyakazi wa kitaaluma wa SCO Angers.

Mwaka 2006, Aussems alikuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa CIFAS Benin huko Cotonou na baadaye akachukua jukumu la Mkurugenzi wa Kitaifa wa Ufundi wa Shirikisho la Soka la Benin na mkufunzi wa kitaifa mnamo 2007.

Chini ya uongozi wake, Benin ilishiriki katika michuano mitatu mfululizo ya Kombe la Mataifa ya Afrika, na kurekodi mafanikio ya kipekee kwa taifa hilo dogo la Afrika Magharibi.

Mwaka 2009, Aussems alichukua nafasi ya ukocha katika Klabu ya Évian Thonon Gaillard Football Club nchini Ufaransa, akiongoza timu hiyo kuwa bingwa wa Kitaifa na kupandishwa daraja hadi Ligue 2 na baadaye Ligue 1.

Kisha alianza kazi ya ukocha nchini China, kwanza akiwa na Shenzhen Ruby FC katika Ligi Kuu ya China na baadaye na FC Chengdu Blades katika Ligi ya Kwanza ya China.

Mwaka 2014, Aussems alijiunga na AC Leopard Dolisie huko Congo-Brazzaville, ambako aliiongoza timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi ya Congo akiwa na rekodi ya kuvutia ya alama 13 mbele, bila kupoteza, na kufungwa bao moja pekee.

Pia aliiwezesha AC Leopard kutinga nusu fainali ya Kombe la AFC 2014. Aussems baadaye alikaa kwa muda mfupi na AL Hilal ya Sudan kabla ya kujiunga na Simba SC ya Tanzania mwaka 2018.

Aidha, akiwa Simba SC, Aussems alilenga kuipandisha daraja timu hiyo na kuwa miongoni mwa klabu tano bora barani Afrika.

Kocha huyo aliiongoza Simba SC kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2018/19 na kuiwezesha kutinga robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika, na kufungwa na TP Mazembe.

AFC Leopards ilithibitisha kuteuliwa kwa Aussems kama kocha mkuu Februari, 2021 na kuondoka kwake inatajwa kutaacha pengo ndani ya klabu hiyo.

Mbali na hayo, uongozi wa AFC Leopard sasa utakuwa na jukumu la kutafuta mtu mwingine anayefaa ambaye anaweza kuendeleza mafanikio ya Aussems na kuendeleza maendeleo ya timu.(pd/diramakini)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news