NSSF yarekodi faida ya Trilioni 1.01/- mwaka 2021/22

DAR ES SALAAM-Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umepata faida ya zaidi ya shilingi trilioni 1.01, kulingana na hesabu zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika mwaka wa 2021/22, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba amesema.
Amesema sambamba na hilo pia mapato yatokanayo na uwekezaji nayo yameongezeka na kufikia shilingi bilioni 745.

“Hii haijawahi kutokea katika historia ya NSSF,” amebainisha Mkurugenzi Mkuu wakati akitoa tathmini yake baada ya kupokea taarifa ya watendaji wa mfuko walioshiriki kuhudumia wanachama na wananchi kwenye Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yaliyofikia kilele Julai 13, 2023.

Mshomba ametaja sababu za mafanikio hayo kuwa ni pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye mara tu baada ya kuingia madarakani alikuja na mpango wa “Kuifungua Nchi” akilenga kuwaalika wawekezaji kuja kuwekeza nchini lakini pia kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko Tanzania kupitia filamu ya “The Royal Tour”.

“Kichocheo kikubwa ni Mheshimiwa Rais alivyoweza kuwavuta wawekezaji, kumekuwa na ongezeko kubwa la waajiri na waajiriwa, suala zima la uchangiaji limeongezeka, vipato vya wafanyakazi vimeongezeka na haya yote yamechangia kuongeza michango na kufanya kipato cha Mfuko kutokana na uwekezaji kuongezeka pia,” alifafanua Mshomba

Alisema, sababu nyingine ni juhudi kubwa zilizowekwa na Mfuko katika kuboresha mifumo ya TEHAMA ambayo imesaidia kuboresha utoaji wa huduma.

“Kulingana na Mpango wetu wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao unaishia Juni 2026, thamani ya Mfuko itafikia zaidi ya trilioni 11.5, na yote haya yanatokana na msukumo wa kuongeza waajiri na waajiriwa wanaochangia katika Mfuko lakini pia kazi nzuri inayofanywa na Mfuko,”alifafanua.

Kwa sasa thamani ya Mfuko wa NSSF ni trilioni 7.1, hivyo Mkurugenzi Mkuu amewahimiza Watanzania hususan kutoka sekta binafsi kujiunga kwa wingi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news