Rais Dkt.Mwinyi afunga Maonesho ya 47 ya Sabasaba, atoa wito

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amezitaka taasisi zinazosimamia biashara kuhakikisha zinaondoa urasimu na kuwawezesha wafanyabiashara nchini kwa kuwekea mazingira rafiki ya biashara zao.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Julai 13, 2023 wakati akifunga Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) katika ukumbi wa Rashid Mfaume Kawawa uliopo uwanja wa Maonesho wa Mwalimu Julius Nyerere ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Rais Dkt.Mwinyi amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zitashirikiana katika kuhamasisha ukuaji wa biashara na uwekezaji kwa kufanyia kazi maoni ya wafanyabiashara nchini.

Pia kwa kuboresha mazingira ya biashara kwa kuwezesha taasisi za Serikali kuwa na mifumo inayosomana itakayoweza kupunguza gharama zisizo za lazima na kuondoa utitiri wa tozo katika biashara nchini.

Maonesho hayo ya 47 kwa mwaka huu yameshirikisha jumla la kampuni 3500, kampuni 267 ni kampuni za nje ya nchi kutoka nchi 17 duniani huku yakitembelewa na wananchi takribani milioni tatu.

Aidha, maonesho hayo ambayo yalianza Juni 28, 2023 hadi Julai 13, 2023 ndani ya viwanja vya Maonesho ya Biashara vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (SabaSaba) vilivyopo Barabara ya Kilwa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam yameratibiwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade).

Maonesho hayo yameongozwa na kauli mbiu ya "Tanzania Mahali Sahihi kwa Biashara na Uwekezaji" ikiwa inaenda sambamba na utekelezaji wa majukumu ya TanTrade.

TanTrade, hii ni taasisi ya umma iliyoundwa kwa Sheria ya Bunge Na. 4 ya mwaka 2009 yenye majukumu ya kuishauri Serikali kwenye masuala ya kuunda, kuendeleza, kusimamia na kutekeleza sera na mikakati za biashara nchini, kudhibiti na kutangamanisha maendeleo ya soko la ndani ya nchi na nje ya nchi.

Pia TanTrade ina majukumu ya kuzijengea uwezo Jumuiya za Wafanyabiashara juu ya namna bora ya kusimamia shughuli za biashara ya ndani na nje ya nchi, kuanzisha, kutunza na kuendeleza Kanzidata ya taarifa za biashara nchini pamoja na kuandaa na kuratibu Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yakiwemo maonesho ya viwanda, misafara na mikutano ya wafanyabiashara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news