Rais Dkt.Mwinyi ataja sekta muhimu kwa ustawi wa wananchi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, sekta za afya,maji na elimu ni muhimu kwa ustawi wa watu wa Zanzibar.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Julai 24,2023 Ikulu jijini Zanzibar alipozungumza na Kaimu Balozi wa Saudi Arabia nchini, Fahad Alharbi aliyefika kumtembelea.

Rais Dkt.Mwinyi amesema, licha ya sekta hizo kuwepo kwa kiwango kikubwa nchini, lakini zinahitaji kuimarishwa zaidi ili kuwaondoshea wananchi changamoto zinazozikabili sekta hizo, hivyo aliiomba Serikali ya Saudi Arabia kuongeza ushirikiano zaidi kwenye sekta hizo.

Aidha, Dkt.Mwinyi aliishukuru Serikali ya Saudi kwa zawadi ya tende tani 25 iliyoletwa kwa ajili ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kueleza Serikali inaweka utaratibu mzuri ili ziwafikie walengwa.

Rais Dkt.Mwinyi ameeleza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa na ushirikiano wa karibu wa maendeleo na taasisi mbalimbali za kimataifa za umma na binafsi, hivyo alizikaribisha taasisi nyingine kutoka Saudi Arabia kuisaidia Zanzibar.

Naye, Kaimu Balozi wa Saudi Arabia, Fahad Alharbi akiambatana na ujumbe wa watu wanne kutoka Taasisi ya misaada ya kibinadamu ya King Salman wa Saudi Arabia, aliahidi kuendelea kuudumisha ushirikiano wa diplomasia uliopo baina ya Zanzibar na Saudi Arabia ambao ni wa historia.

Alieleza, Serikali ya nchi hiyo imekua ikitoa misaada kwa sekta mbalimbali kwa mataifa mengi duniani.

Pia Kaimu Balozi huyo, alitumia fursa hiyo kumfikishia Rais Dkt.Mwinyi salamu za Mfalme wa Saudi Arabia, Salman bin Abdulazizi Al Saud na kueleza kuwa salamu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pia atazifikisha kwa Mfalme huyo.

Mapema, ujumbe kutoka taasisi ya misaada ya kibinadamu ya King Salman wa Saudi Arabia, ulikutana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mhe.Haroun Ali Suleiman ofisini kwake Mazizini na kumkabidhi katoni 1,200 za tende sawa na tani 25 kwa ajili ya zawadi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news