Rais Dkt.Samia aifanya Morocco Square ya NHC kuweka heshima mpya Tanzania

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula amesema, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inaandaa sera itakayowezesha Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) kuwekeza katika ujenzi na kununua nyumba zitakazojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na waendelezaji wengine nchini.
Dkt.Mabula ameyasema hayo Julai Mosi, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa kukabidhi nyumba 43 pamoja na maeneo 49 ya biashara kwenye mradi wa Morocco Square unaotekelezwa na NHC uliopo Halmashauri ya Manispaaa ya Kinondoni jijini humo.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kuwa na maono makubwa ambayo yameliwezesha kubuni mradi mkubwa wenye hadhi na viwango bora zaidi nchini.
Muonekano wa majiko katika moja ya nyumba iliyonunuliwa ndani ya Mradi wa Morocco Square.

"Mradi huu niwahakikishie tu, hakuna mradi mwingine mkubwa kama huu, kwa sababu katika kufuatilia inaonekana miradi ipo, lakini si miradi ambayo imebeba huduma zote sehemu moja, kwa hiyo niwapongeze kwa ubunifu wenu na namna ambavyo mmejiweka wazi katika huduma ya uendelezaji miliki, lakini pia uwekezaji ambao una manufaa.

"Morocco Square ina sifa za kipekee sana, ikiwemo kuwezesha wateja kupata huduma mbalimbali sehemu moja, lakini pia eneo hili la Morocco Square lipo katikati ya mji,na ni sehemu ambayo ni karibu sana kuweza kupata huduma zote,"amefafanua.
Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesema, mradi wa Morocco Square unamuwezesha mnunuzi, mpangaji au mteja wa nyumba na huduma katika majengo hayo kuweza kupata huduma zote karibu, kwani licha ya zile ambazo zinapatikana ndani, pia linazungukwa na miundombinu bora ya barabara na stendi karibu.

Sambamba na huduma za afya karibu, nyumba za ibada, elimu na nyinginezo ambazo mteja hatalazimika kutumia muda mrefu kutoka alipo kuzifikia.
"Wakati tunazunguka na kujionea eneo hili, nimeambiwa kwamba mradi huu umekamilika ambapo jengo la makazi,hoteli na biashara yamekamilika, na ndiyo maana tupo hapa leo ninakabidhi funguo, lakini ninafarijika sana kuwa sehemu ya kukabidhi funguo hizo.

"Niwapongeze sana sana, Shirika la Nyumba la Taifa kwa kuweza kuuza nyumba 43 kati ya nyumba 100 zilizopo hapa, kwa hiyo kwa wale ambao wanatamani, fursa zipo wanatakiwa waje kununua nyumba, lakini pia kati ya maduka au vyumba vya biashara tayari na wale wenye uhitaji pia wafike, lakini pia niwapongeze sana kwa kumpata mwekezaji wa hoteli.

"King Jada Hotels & Apartments Ltd ni wawekezaji wakubwa, na hata walipokuja kuangalia waliweza kuanza kupangilia mambo yao ili kuweza kuifanya kuwa hoteli ya nyota nne, kwa hiyo wakaanza kufanya hivyo kupandisha viwango, ili waweze kuiendesha kwa namna ambavyo wanataka wao.

"Mradi huu pia ni kielelezo cha uboreshaji wa miji, kama ambavyo tumekuwa tukizungumzia muda wote, kwamba tunayaondoa majengo chakavu, ambayo yalikuwepo na yamepitwa na wakati.Kwa dhati kabisa nimshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuukwamua mradi huu na kuwezesha kukamilika kwa majengo ya mradi huu wa Morocco Square,’’amesema Waziri Dkt.Mabula.
Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesema, mwaka jana NHC walizindua sera yake ya ubia ikiwa na lengo la kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, kujenga majengo mapya kwenye viwanja au majengo ya shirika yaliyopo katikati ya miji yaliyopitwa na wakati.

Pia,amesema sera hiyo ya ubia ni muendelezo wa azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kufungua milango ya uwekezaji kwa kutoa fursa kwa wawekezaji mbalimbali ndani na nje ya nchi.

‘’Uwekezaji huu uwe ni wa nchi nzima na si Dar es Salaam pekee kwa kuwa NHC inayo viwanja na majengo yaliyopitwa na wakati katika miji yetu mbalimbali nchini,’’amesema Waziri Dkt.Mabula.
Amebainisha kuwa, ujenzi wa mradi huo una faida kubwa kwa kuwa unaongeza ajira, umeongeza pato la serikali kupitia kodi mbalimbali kama vile Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kodi ya ardhi na kodi ya majengo sambamba na kupendezesha mandhari ya miji.

Pia, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula ameshauri taratibu za kupata hati pacha za umiliki ufanyike mapema kwa kuwa ndiyo salama ya milki pamoja na uwezesho katika shughuli za maendeleo.

Wakati huo huo, amewataka wamiliki, na wapangaji kutunza miundombinu katika jengo hilo ili kuendelea kulinda ubora wa uwekezaji huo mkubwa zaidi nchini.

Mkurugenzi Mkuu NHC

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw.Hamad Abdallah amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt.Angeline Mabula kwa kuendelea kushirikiana nao muda wote ili kuhakikisha shirika linazidi kustawi kwa manufaa ya Watanzania na Taifa kwa ujumla. 
"Mheshimiwa Waziri tuliona ni vizuri sana kama Shirika la Nyumba la Taifa, badala ya kuuza tu nyumba na kutokuwa na forum hata ya kuwakutanisha wateja wetu, wanunuzi.

"Tukasema tuanze utamaduni mpya, pale ambapo tunawakabidhi wateja wetu nyumba basi tuwe na hafla ndogo, moja ni kwa ajili ya kutambua na kuthamini wao kuwa wateja wa shirika.

"Lakini, vile vile kuwatengenezea forum ya wao wenyewe kukutana na kufahamiana, lakini lingine katika kufahamiana kuna sheria ambayo wewe (Mheshimiwa Waziri) unaisimamia.
"Sheria ya The Unit Titles Act (Sheria ya Miliki ya Sehemu ya Majengo) ambayo wizara yako ndiyo inayosimamia, ambayo inataka majengo yote ambayo yana zaidi ya wamiliki au wanunuzi saba waweze kuunda Umoja wa Wamiliki wa Nyumba katika eneo hilo.

"Sasa forum kama hii inawafanya vile vile wanunuzi kufahamiana na hata kufikia hatua ya kuunda umoja na kuchagua viongozi wao, kwa hiyo tukaona badala ya kuwaacha kuanza kutafutana, basi tuwe na forum za namna hii.

"Lakini, vile vile kama unavyofahamu jengo hili limechukua muda mrefu kidogo, lilisimama na Watanzania wakipita barabarani kule hawajui kinachotokea ndani ya jengo hili.
"Hawajui kama kuna ujenzi ulikuwa ukiendelea, japokuwa kulikuwa na changamoto ya kusimama kwa mradi, tukaona tutumie njia sahihi ya kuwafahamisha kuwa jengo lao, kwa sababu National Housing ni ya Watanzania, kuwa jengo lao limekamilika.

"Na, leo wachache ambao wameudhuria wamekuwa mabalozi wetu wa kuwaambia Watanzania wengine, kuwa jengo limekamilika.

"Kwa hiyo, leo mbali na hayo tukasema vile vile siyo Mkurugenzi Mkuu anawakabidhi ufunguo wanunuzi wa nyumba, sasa leo uwakabidhi hawa wachache maana tukisema uwakabidhi wote itatulazimu kutumia labda siku moja kukamilisha shughuli hiyo.

"Lakini, tumeanza kufanya mikutano na wanunuzi kama nilivyozungumza awali, tuna majukumu ya kuwafahamisha matakwa ya kisheria yanayotokana na Sheria ya The Unit Titles Act, ambayo ni pamoja na kuwafahamisha kuhusiana na aina gani ya umoja wanapaswa kuunda.

"Kwa sababu kama sehemu ya makazi, tutakuwa na wakazi 100, lazima kuwe na utaratibu maalumu wa wao kuishi katika hili jengo, kuweza kuwafahamisha majengo haya yana nini, yana mifumo ya aina gani, mifumo hiyo inafanya kazi kwa namna gani,ili tukiwakabidhi nyumba baada ya mwaka mmoja nyumba isiwe katika hali iliyokusudiwa.
"Baadhi ya mifumo isiwe imehabarika, kwa hiyo tumeanza mkutano wa kwanza na tutakuwa na mfululizo wa mikutano, lakini vile vile Sheria ya The Unit Titles Act inatutaka sisi kama developer, na ni vizuri kama developers wengine walivyo kwa National Housing kutambua kuwa na jukumu la kuhakikisha wanaunda umoja wao.

"Tunawasaidia kutengeneza katiba, ya umoja wao ambayo inatakiwa kusajiliwa katika wizara yako, lakini vile vile, kuweza kuwashika mkono na kuweza kuwaonesha ni jinsi gani wanaweza kulisimamia hili jengo, wanaweza kuamua kwa sababu sheria inawataka.

"Sisi kama shirika tunafanya kazi hiyo, lakini hatuwalazimishi kufanya hivyo pale ambao wao wana uwezo wa kufanya hivyo, lakini wakati wao wanajipanga kufanya hivyo, sisi tunalibeba jukumu hilo ili kuhakikisha ukaazi wao katika majengo haya yanakuwa salama, lakini mwisho wa siku kuwawezesha kufurahia.

"Kwa sababu hapa hawajuanunua tu nyumba, wamenunua life style,ni maisha ya namna gani watakayoishi, nadhani ni maisha tofauti kidogo na Watanzania ambao hawafahamu huu mradi, huu ni wa kwanza ambao National Housing imefanya, tofauti na miradi mingine.
"Na ukiangalia kwenye strategic plan yetu tulikuwa tunazungumza,kuna miradi ambayo tutaifanya, faida ambayo inatapikana itawarudia wale Watanzania ambao hawana uwezo wa kumudu nyumba, kwa hiyo kwa namna nyingine mradi huu utakuwa unatoa ruzuku.

"Kwa miradi ile ya watu wa chini, sasa hapa sisemi kuwa, tumewauzia ghali sana lakini unaweza kuona ubora wa nyumba zenyewe zilivyo, kila kitu ukikiangalia kina ubora si kila kitu unaweza kukinunua sehemu yeyote, hapana.

"Lakini vile vile kwa upande wa shopping malls, tuna flow tatu hapa vile vile ni life style,mbali na maduka hapa tutakuwa na mabenki, tuna kumbi za sinema tofauti na kumbi zingine ambazo zinapatikana hapa mjini.

"Lakini, vile vile ukienda ghorofa ya pili kuna food points, ambayo ni ya kipekee kabisa ambapo ni zaidi ya shopping malls zingine unazoziona, design ya hapa ni zaidi ya shopping malls kama walizotembelea wenzetu kwenda Marekani, kwenda Dubai na nchi zilizoendelea.

"Kwa hiyo kuna maisha tofauti kabisa, lakini vile vile tuna hoteli ambayo ni hoteli nzuri kabisa na tayari imeshapata mteja ni kampuni ambayo inaendesha hoteli nyingine nchi kama vile India (King Jada Hotel) wameshapatikana, lakini tuna tower mbili ambazo zinaonekana kule juu ni ofisi.

"Kiufupi katika ofisi hizo kuna vitu ambavyo vinapatikana na havipatikani katika majengo mengine Tanzania, ni suala la usalama, lakini moja ya tower ilikuwa inaruhusu helikopta kuweza kutua juu ya jengo, ukiwa na ofisi yako hapa unataka kuwahi airport, helikopta inakuja inatua juu ya jengo inakuchukua inakupeleka airport.

"Lakini vile vile kutokana na ofisi za ubalozi karibu, tukasema tuweze kuweka baadhi ya mambo sawa ili wasije kusema kuna helikopta imetua kuna masuala ya kiusalama, kwa hiyo majengo haya yanaruhusu mambo kama hayo kwa hiyo ni majengo bora zaidi, ni jengo kubwa nzuri na chini ya ardhi tumeenda flow mbili kwa ajili ya maegesho, umeme wa TANESCO ukikatika tuna jenereta za kutosha.

"Za kuweza kuendesha jengo nzima bila tatizo, tuna mifumo ya kuzima moto ya kisasa, lakini vile vile ya kubaini moto, tuna mifumo ya kisasa yaani cctv.
"Hawezi kuja mwizi hapa hakatoka salama, ambapo muda wote anakuwa monitor, si shopping malls lakini pia katika upande wa makazi, maana yake watu wanakuwa salama.

"Kwa hiyo, kwa kifupi Mheshimiwa Waziri, niseme tu kwamba tupo katika mradi wa kipekee sana na wanunuzi au wapangaji vile vile wamepata sehemu sahihi, sehemu hii ya shopping malls nikutoe shaka Mheshimiwa Waziri, almost imejaa na tuna mahitaji kuna sehemu ndogo tu ya food points na tulikuwa tunataka aina mbalimbali za vyakula.

"Lakini otherwise eneo lote limejaa na kuna orodha kubwa ya watu ambao wanasubiria kuona kama kuna mtu atashindwa waweze kuchukua, lakini kuna makampuni mengine imebidi tuwaombe wapunguze maeneo yao ili tuweze kuwapatia wapangaji wengine, kwa hiyo ni mradi wenye tija sana kwa nchi.

"Lakini kwa kipekee Mheshimiwa Waziri, nimshukuru sana Mkandarasi wa hili jengo Estim Construction kuna baadhi ya maeneo alienda mbali zaidi na kuboresha bila nyongeza ya gharama, lakini vile vile alituvumilia sana wakati ule ambao tulipitia baadhi ya changamoto kwa hiyo nimshukuru kwa kipekee Estim Construction kwa kazi nzuri.

"Vile vile niwashukuru wanunuzi na wapangaji, nao wametuvumilia sana, wamesubiri muda mrefu sana, lakini vile vile walituelewa changamoto ambazo tulikuwa tunazipitia na mpaka leo hii tupo nao.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mkuu wa NHC amezishukuru taasisi mbalimbali za kifedha zikiwemo benki ambazo zimewezesha wanunuzi na wapangaji kupata huduma ya nyumba katika shirika hilo.
Licha ya nyumba za Morocco Square kuwa katika hadhi ya Kimataifa na ubora wa hali ya juu, wanunuzi wengi wakiwa katika makazi yao watakuwa na nafasi ya kuona taswira kubwa ya jiji ikiwemo Bahari ya Hindi wakiwa barazani.

"Na bahati nzuri, nyumba hii inaweza kukupa dhamana benki, maana yake unaponunua nyumba kwetu unapewa unit title, na tayari Mheshimiwa Waziri nikuhakikishie tumeshaanza hatua kwa ajili ya kuwapatia wanunuzi wa hizi nyumba unit titles zao, kwa sababu zinawasaidia kutambulika kuwa ni wamiliki wa haki zote kama alivyo mmiliki mwingine wa nyumba. Na nyumba tunayokuuzia yenyewe ni dhamana benki.

"Zamani hakukuwa na hizi unit titles, ukienda Upanda developers wa kwanza walikuwa wanatoa long terms lease, long term lease si nzuri sana na wizara imetambua hilo ndiyo maana sasa inakupwa haki ya umiliki wa nyumba,hivyo unit titles hizo Mheshimiwa Waziri tutazitoa mapema tu,"amefafanua kwa kina Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw.Hamad Abdallah.

Kariakoo

"Kwa kipekee nitambue kuna wawakilishi wa wafanyabiashara wa Kariakoo, Mheshimiwa Waziri ulikutana na wafanyabiashara wa Kariakoo wiki mbili zilizopita, ulikuwa ni mkutano mzuri sana, na jana nilikuwa na mkutano mwingine mzuri na wafanyabiashara wa Kariakoo.

"Lakini, nikasema niwakaribishe leo waje wajionee tunaposema National Housing tunaendeleza maeneo yetu, wajue tunaendeleza kitu gani.
"Zamani eneo hili lilikuwa linakaa watu wawili, familia mbili tu, tumeendeleza tumeweza kupata majengo yote haya, lakini tukasema tuliendeleze eneo hili kwa sababu wakati zinakaa familia mbili, tija yake ilikuwa ndogo, lakini vile vile tunawanyima fursa watanzania wengine kuwa wanunuzi au wapangaji katika eneo hili.

"Lakini, vile vile Kariakoo, wameridhia kabisa suala la kuendeleza, sasa hivi tunazungumza tu uendelezaji utafanyika siku gani, lakini vile vile baada ya uendelezaji kitu gani kitafanyika kwa wao, na tulishatoa maelekezo kuwa, kwa wale wapangaji wazuri wa Kariakoo tungependa kuwa nao kama wapangaji baada ya uwekezaji.

"Lakini vile vile tunataka tuwatambulishe katika mazingira tofauti kuwa, kuwa biashara si lazima tu zifanyike Kariakoo, kuna fursa nyingine kama hizi za Morocco Square, lakini kuna fursa nyingine tutawaonesha Up Town Towers kule Tanganyika Packers.

"Tusiwafanye watu wanaotoka Tegeta kwenda Kariakoo, tu kwa hiyo hii Mheshimiwa Waziri nikasema niwakaribishe waje kuangalia hizi fursa, kwani tunaweza kufanya Kariakoo nyingine nje ya Kariakoo,"amesisitiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw.Hamad Abdallah.

Shukurani

Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya wanunuzi na wapangaji wa nyumba katika Mradi wa Morocco Square, Aboubakar Ally Aboubakar amesema, wataendelea kuunga mkono jitihada za shirika na Serikali kwa ujumla kwa ajili ya kuendelea kuboresha makazi bora nchini.
‘’Ni wajibu wa sisi wananchi kushirikiana na Serikali kwa kwenda pamoja ili tupate maendeleo na NHC imekuwa wasikivu na nimeridhika na kazi inayofanywa na shirika hilo,’’amesema.

Ameongeza kuw,a jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuboresha makazi nchini kupitia Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) zinawapa moyo na wamejionea wenyewe matunda ya utekelezaji wa mradi huo wa Morocco Square.

Meneja

Awali, Meneja Mradi wa Morocco Square, Mhandisi Samuel Metili akitoa taarifa fupi kuhusu mradi huo amefafanua kuwa, mradi huo ambao umegharimu shilingi bilioni 137.5 umekamilika kwa asilimia zote, kilichobaki tu ni kufanya ukaguzi mdogo mdogo katika baadhi ya mifumo.

Licha ya nyumba za Mradi wa Morocco Square kuwa katika hadhi ya Kimataifa na ubora wa hali ya juu, wanunuzi wengi na wapangaji wakiwa katika makazi yao watakuwa na nafasi ya kuona taswira kubwa ya jiji ikiwemo Bahari ya Hindi wakiwa barazani.

Mhandisi Metili amesema, mradi huo wa aina yake nchini unajumuisha nyumba za makazi, ofisi, hoteli na maeneo ya biashara ambapo mteja akifika hapo atakuwa anapata huduma zote kwa wakati mmoja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news