Salamu za Jumapili, Tupende uzima

NA LWAGA MWAMBANDE

UKITAFAKARI neno la Mungu kupitia Biblia Takatifu utaona kuwa, Mungu aliwapa Israeli uchaguzi juu ya uzima na mema, mauti na mabaya. Aidha, Bwana Mungu aliwaamuru kushika maagizo yake, wakienenda katika njia zake ili wapate baraka.

Picha na spiritandtruthonline.

Matokeo ya kutoshika mausia haya ni kuangamia, na kutopata siku nyingi hapa duniani.Mungu anatuita kulishika neno lake katika maisha yetu, ametuwekea mbele yetu kuchagua kati ya uzima na mauti, baraka na laana.

Pia, Mungu anatuita kuchagua uzima, ili tuwe hai, sisi na uzao wetu. Rejea,Kumbukumbu la Torati 30:19, "Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako."

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, kila mmoja wetu apende uzima kwa kuwa, huo ndiyo uchaguzi sahihi katika maisha. Endelea;


1.Ninaleta mashahidi, ni hizi nchi na mbingu,
Maisha kuyafaidi, kama apendavyo Mungu,
Au kuwa wakaidi, kinyume cha kwake Mungu,
Kuna uzima mauti, baraka pia laana.

2.Kuna uzima mauti, baraka pia laana,
Mwenyewe una tiketi, kwenda utakakoona,
Kiko mbele yako cheti, upandacho utavuna,
Bora chagua uzima, kwako na vizazi vyako.

3.Bora chagua uzima, kwako na vizazi vyako,
Kwake Mungu kusimama, yanenavyo maandiko,
Nanyi mzidi kuvuma, mkijawa na upako,
Maneno ya kinywa chako, mwamuzi wa kesho yako.

4.Maneno ya kinywa chako, mwamuzi wa kesho yako,
Kubariki kesho yako, kulaani kesho yako,
Kwa hiyo ni juu yako, mpini huo ni wako,
Yale unasema leo, majibu ya kesho yako.

5.Yale unasema leo, majibu ya kesho yako,
Wataka maendeleo, ukijaze kinywa chako,
Ili ufike upeo, yote hiyo juu yako,
Amka usinziaye, nuru inakumulika.

6.Amka usinziaye, nuru inakumulika,
Mungu wako yeye ndiye, ufaaye kumshika,
Kwamba wongozwe na yeye mwisho mwema utafika,
Wewe utabarikiwa, na wajao bada yako.

7.Wewe utabarikiwa, na wajao bada yako,
Vile umefanikiwa, katika maisha yako,
Nao watafanikiwa, hao wa kizazi chako,
Hebu wapende wa kesho, inampendeza Mungu.

8.Hebu wapende wa kesho, inampendeza Mungu,
Usifanye ya michosho, kesho wawe kwenye pingu,
Uishi kimaonesho, ujiwekee kiwingu,
Mabaya ya Hezekia, kutojali kesho yake.

9.Mabaya ya Hezekia, kutojali kesho yake,
Mungu hakufurahia, alofanya mambo yake,
Adhabu mtamkia, ila si wakati wake,
Yeye akafurahia, watajijua wa kesho.

10.Yeye alifurahia, watajijua wa kesho,
Peke lijiangalia, siyo kizazi cha kesho,
Vibaya nakuambia, kuwa nao huo mwisho,
Hakikisha leo yako, wa kesho hawaumii.

11.Hakikisha leo yako, wa kesho hawaumii,
Leo maamuzi yako, kesho hawayajutii,
Ili na uwepo wako, wafurahi wautii,
Kupenda kizazi chako, ni kujipenda mwenyewe.

12.Kupenda kizazi chako, ni kujipenda mwenyewe.
Kama maamuzi yako, si kujijali mwenyewe,
Bali wataokuweko, baada yako mwenyewe,
Mungu utusaidie, kwamba tupende uzima.

13.Mungu utusaidie, kwamba tupende uzima,
Tena utusaidie, ya mauti yakikoma,
Ili sote tufikie, kwenye wa milele wema,
Ni baraka si laana, ndizo twazitaka kwako.
(Kumbukumbu la Torati 30:19, Isaya 39:1-8, 2 Wafalme 20:12-19)

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news