TASAF guseni walengwa halisi-Waziri Simbachawene

NA LUSUNGU HELELA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George ameutaka Uongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuwa shirikishi katika mchakato wa kuwabaini walengwa halisi ambao ni maskini huku akiwasisitiza kuwatumia Maafisa Maendeleo ya Jamii katika mchakato huo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao. Wa pili kulia waliokaa ni Naibu Waziri wake, Mhe. Ridhiwani Kikwete na wa pili kushoto waliokaa ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Shedrack Mziray.

Imeelezwa kuwa licha ya TASAF kufanya kazi yake nzuri ya kukwamua kaya masikini kwenye lindi la umasikini lakini kumekuwa na minong'ono kuwa wanaopata ruzuku hiyo sio walengwa halisi.

Kauli hiyo ameitoa Julai 13, 2023 wakati wa ziara yake ya kikazi jijini Dar es Salaam, ikiwa ni muendelezo wa kuzungumza na Watumishi kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema Maafisa Maendeleo hao wa Jamii ni watu muhimu sana katika zoezi hilo kwa vile wapo katika ngazi ya Kata pamoja na ngazi ya Kijiji, hivyo wanawajua walengwa halisi.

‘’Watumieni hawa kwani licha ya kuishi na walengwa hawa lakini pia Maafisa hawa wamekuwa wakishiriki katika vikao vya Madiwani’ amesisitiza Mhe Simbachawene.

Amefafanua kuwa, TASAF msingi wake ni mpango shirikishi wa kuondoa umasikini hivyo, inatakiwa kuwashirikisha viongozi katika maeneo husika ili iweze kutimiza azma ya kuanzishwa kwake.

Hata hivyo, Mhe.Simbachawene amesema TASAF bado inahitajika sana kwa vile bila uwepo wake, umaskini ungekuwa umeongezeka kwa kiasi kikubwa sana na kusisitiza kuwa itaendelea kuzikwamua kaya zilizoko kwenye umasikini uliokithiri.

Naye Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Memejimenti ya Utumishi wa Umma, Mhe.Ridhiwani Kikwete amewapongeza watumishi wa TASAF kwa kazi nzuri wanayoifanya huku akisisitiza kuwa TASAF imesaidia ongezeko la wanawake katika shughuli za kiuchumi.

Ameongeza kuwa kutokana na uwepo wa TASAF kumesaidia kupunguza migogoro kwenye ngazi ya kaya baada ya wananchi wengi maskini kujihusisha kwenye na uzalishaji mali.

Naye, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Shedrack Mziray amesema atatekeleza maagizo yote yaliyotolewa na viongozi hao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha walengwa wa ndio wanakuwa wanufaika namba moja.

TASAF ilianzishwa kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tatu lengo likiwa ni kuondoa umasikini uliokithiri kwa wananchi katika maeneo ya vijijini na maeneo machache ya mjini kwa kuwashirikisha kwenye shughuli za kiuchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news