Serikali yawakabidhi jukumu wahariri kuhusu Kiswahili

NA GODFREY NNKO

SERIKALI imesema, wahariri wa vyombo vya habari nchini wana nafasi kubwa ya kuifanya lugha ya Kiswahili kuendelea kustawi zaidi duniani, hivyo kila mmoja awajibike kuhakikisha uandaaji wa vipindi, maudhui nyingine kwa ajili ya magazeti, mitandao au majarida yanazingatia usanifu.

Hayo ameyabainisha leo Julai 4, 2023 na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdullah katika Ukumbi wa Sheikh Idris Abdul Wakil uliopo Kikwajuni jijini Zanzibar.

Mheshimiwa Abdullah alikuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Wahariri lililoandaliwa na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) ambalo liliangazia juu ya nafasi ya wahariri katika kusimamia matumizi ya Kiswahili sanifu kwenye vyombo vya habari nchini.

Kongamano hilo ni maandalizi ya kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani ambayo yatafanyika Julai 7, 2023 huku kauli mbiu ikiwa ni “Kiswahili Chetu; Umoja Wetu”.

"Napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwa uongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kunialikia kuwa mgeni rasmi katika siku hii ya leo kwa maendeleo ya lugha yetu adhimu ya Kiswahili.

"Ninawashukuru sana, tunafahamu (wahariri nchini) kuwa ninyi ni wathamini wa kupitisha na kuweka sawa mambo yote ndani ya vitabu, magazeti au majarida kwa lengo la kumuwezesha mlengwa kuweza kupata ujumbe uliokusudiwa.

"Hivyo, mna jukumu la kulinda maadili yenu katika kuyaibua mambo mbalimbali bila ya kumuonea mtu au taasisi fulani, wakati Serikali ikiendelea kutafuta fursa mbalimbali kwa wataalamu wetu wa lugha ya Kiswahili, ipo haja ya kuzingatia matumizi sahihi ya Kiswahili.

"Katika kazi zetu, kwani ni sehemu ya kukitangaza zaidi Kiswahili duniani, nimefuatilia kwenye vyombo vya habari, wengi wenu mnakitumia vizuri Kiswahili katika kazi zenu.

"Hongereni sana, hata hivyo wapo wachache ambao wamekuwa wakitia dosari lugha hii ama kwa kutokujua au kwa kutia mbwembwe zao tu,katika kufikisha habari.

"Nitumie fursa hii, kupitia mkutano huu tuweke mikakati ambayo itasaidia kuzuia hali hiyo isiendelee kwa lengo la kuitunza lugha yetu ya Kiswahili.

"Dhamana mliyobeba kuhusu lugha ya Kiswahili ni kubwa na hapana shaka kuwa ninyi ni walimu wa lugha hii kutokana na majukumu yenu.

"Bila shaka mkutano huu utasaidia kuleta mjadala wa kina katika mustakabali wa kina wa lugha na mambo mengine ya tasnia ya habari.

"Hivyo,kwa kuzingatia haya yote, jukumu la kukiendeleza Kiswahili lipo mikononi mwetu.Ninaamini kuwa, tutaendelea kuikuza lugha hii, ndani na nje ya nchi ili iweze kutumika katika vikao na majukwaa ya Kimataifa.

"Nitoe pongezi kwa mabaraza ya Kiswahili, BAKITA (Baraza la Kiswahili Tanzania) na BAKIZA (Baraza la Kiswahili Zanzibar) kwa kufanya kazi nzuri ya kusimamia matumizi na maendeleo ya Kiswahili.

"Ninafahamu kuwa, BAKIZA wameweza kusambaza kamusi za Kiswahili katika vyombo vya habari.Ninatambua kuwa, kupitia mabaraza yetu ya BAKITA na BAKIZA, Kiswahili kimesambaa na kimewekewa mikakati katika nchi za Ujerumani.

"Uholanzi, Italia,Nigeria, Nchi za Falme za Kiarabu (UAE), Malawi, Rwanda na Zimbabwe huu ni mwanzo mzuri katika kuitangaza na kuinadi lugha yetu ili itunufaishe.

"Ninaomba, mziendeleze juhudi hizi, mlizozianzisha na kwa hakika, hii itakuwa na faida kubwa kwa Taifa letu. Nitumie fursa hii kuwataka sasa kutumia jukwaa lenu hili katika kutafuta fursa za utangazaji katika vyombo vya habari vya Kimataifa ambapo hadi sasa zipo redio na vituo vya runinga za nje ya nchi zipatazo 38.

"Zinazorusha matangazo yake kwa lugha ya Kiswahili,jukwaa lenu liwe mfano katika kuangalia fursa hizo na kuwaunganisha wataalamu wa tasnia ya habari.

"Aidha, kwa kuwa kauli mbiu ya maadhimisho ya Kiswahili duniani mwaka huu Kitaifa ni "Kiswahili Chetu ni Umoja Wetu".Ninatoa wito kwa jukwaa hili kushirikiana na mabaraza katika kukizungumza Kiswahili sanifu kwenye vyombo vya habari.

"Serikali katika kuimarisha Sekta ya Habari inaifanyia marekebisho Sheria ya Habari ili iendane na mabadiliko yanayojitokeza katika Sekta ya Mawasiliano ya Habari na Teknolojia.

"Serikali kwa kufahamu umuhimu wa habari imeamua kuanzisha vitengo vya habari na uhusiano katika wizara na taasisi za Serikali ili limefanyika kwa makusudi ili kuweza kufikisha taarifa za Serikali kwa usahihi, na kwa wakati na pia kupata mrejesho kwa wananchi tunaowahudumia.

"Pia, nitoe shukurani zangu za dhati kwa viongozi wetu wakuu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa uthubutu wao na juhudi ambazo wanazichukua katika kufanikisha jambo hili muhimu, kwa Taifa letu.

"Tukienzi na kukikuza Kiswahili, ni moja ya tunu za Taifa letu,"amefafanua kwa kina Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdullah katika Ukumbi wa Sheikh Idris Abdul Wakil.
 
Novemba, 2021 Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lilipitisha Julai 7 ya kila mwaka kuwa siku ya kuadhimisha lugha ya Kiswahili kote duniani.

Uamuzi huo ulifikiwa kupitia mkutano wake wa nchi wanachama ambao ulifanyika makao makuu ya UNESCO jijini Paris, Ufaransa hivyo kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha pekee kutoka Bara la Afrika kupewa siku yake maalum ya utambulisho na kuadhimishwa duniani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news