Simba SC mguu sawa msimu mpya 2023/24

NA DIRAMAKINI

WAKATI Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam ikitarajiwa kwenda nchini Uturuki kuweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara 2023-2024, tayari imeweka wazi mastaa ambao wanaamini wataiwezesha klabu hiyo kufanya vema zaidi.
Miongoni mwao ni mshambuliaji Mcameroon, Leandre Essomba Willy Onana kutoka Rayon Sport ya Rwanda ambaye atakuwa mchezaji wake mpya wa kwanza kuelekea msimu ujao. 

Onana mwenye umri wa miaka wa 22 anatua Simba SC baada ya misimu miwili ya kucheza Rayon Sports akiibuka mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Rwanda msimu uliopita 2022/2023.

Mcameroon huyo aliwasili Kigali nchini Rwanda mwezi Septemba mwaka 2021 akiwa sehemu ya wachezaji 50 waliojitokeza kufanya majaribio Rayon Sports chini ya kocha Juma Masudi.

Aidha, ingawa kocha huyo kutoka nchini Burundi alifukuzwa kutokana na matokeo mabaya mwanzoni tu mwa msimu wa 2021/2022, aliwaacha Rayon Sports mshambuliaji huyo ambaye aligeuka lulu kwa klabu hiyo.

Onana kabla ya kujiunga na Rayon Sports kwa majaribio 2021alichezea Ending Sport FC ya kwao, klabu ambayo inasifika kwa kuibua vipaji vya chipukizi nchini Cameroon.

Pia, tayari Simba SC imemtambulisha winga wa kushoto, Aubin Kramo Kouamé kutoka klabu ya ASEC Mimosa ya nchini Ivory Coast.

Chaguo la tatu kwa Simba SC ni beki wa katí, Che Fondoh Malone Junior ambaye amepewa kanadarsi ya miaka miwili kutoka Coton Sport ya nchini Cameroon.

Malone Junior mwenye umri wa miaka 24 anatua Simba SC baada ya kuisaidia Coton kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Cameroon huku yeye mwenyewe akishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa msimu wa 2022-2023.

Pia, Malone Junior ameitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Cameroon ‘Indomitable Lions’ pamoja na timu inayoshiriki michuano ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).

Che Malone ni mchezaji mwenye uzoefu wa kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na shirikisho, ambapo Simba wanaamini atakuwa msaada mkubwa kikosini.

"Uongozi wa klabu unaendelea kuimarisha kikosi kuelekea msimu mpya wa ligi 2023/24 na lengo letu ni kuhakikisha tunarejesha mataji yetu,"ilifafanua sehemu ya taarifa ya Simba SC.

Wakati huo huo,beki mkongwe wa Simba SC, Shomari Salum Kapombe ameongeza mkataba wa kuendelea na kazi Msimbazi hadi mwaka 2025.

Pia, beki wa kushoto wa Simba SC, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ameongeza mkataba wa kuendelea na majukumu Simba SC hadi mwaka 2025.

Aidha,wamemrejesha beki wake David Kameta ‘Duchu’ kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro.

Katika hatua nyingine, wakati hayo yanajiri uongozi wa Klabu ya Simba umefikia makubaliano ya kumtoa kwa mkopo mlinzi wa kati Joash Onyango kwenda Klabu ya Singida Fountain Gate FC hadi mwisho wa msimu 2023-2024.

Uamuzi huo umefikiwa ikiwa Joash amebakiza mkataba wa mwaka mmoja na Simba Sports Club. "Uongozi wa Simba Sports Club unapenda kumshukuru sana Joash kwa mchango wake mkubwa na alikuwa na mchango mkubwa kwenye mafanikio ya Klabu yetu.

"Uongozi wa Simba Sports Club unapenda kumtakia kila la kheri Joash Ochieng Onyango kwenye majukumu yake mapya,"ilifafanua sehemu ya taarifa ya Simba SC.

Meneja

Hayo yanajiri ikiwa tayari Uongozi wa Klabu ya Simba umefikia makubaliano ya kumuajiri Mikael Igendia raia wa Kenya kuwa Meneja wa timu na Mkuu wa Sayansi ya Michezo kwa mkataba wa miaka miwili.

Igendia mwenye umri wa miaka 36 anachukua nafasi ya Patrick Rweyemamu ambaye amekuwa Mkuu wa Programu za soka la vijana.

Ujio wa Igendia unatajwa unaongeza ufanisi katika benchi la ufundi kwakuwa yupo vizuri pia kwenye utimamu wa mwili pamoja na utawala wa timu.

Igendia amewahi kufanya kazi na Gormahia FC, timu ya Taifa ya Kenya (Harambee Stars) pamoja na timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars).

Uongozi wa klabu hiyo, umetaja kuwa, uwepo Igendia kwenye kikosi ni sehemu ya kuliboresha benchi lao la ufundi kuelekea msimu mpya wa Ligi 2023/24.

Mbali na hayo pia, imemtambulisha Mnyarwanda Corneille Hategekimana kuwa kocha wake mpya wa Fiziki akifuatiwa na kocha wa Makipa, Mspaniola Daniel Cadena ambaye msimu uliopita alikuwa Azam FC.

Hategekimana mwenyeumri wa miaka 47 amejiunga na Simba SC akitokea AS Kigali ya nchini kwao Rwanda. Hategekimana amefuzu mafunzo ya kozi mbalimbali za viungo kwa wachezaji, ana Diploma ya Uongozi wa Michezo, Mkufunzi wa viwango (GPS) kwa wachezaji, Kozi ya juu ya Viungo inayotolewa na FIFA aliyopata Oktoba 2018 Johannesburg, Afrika Kusini.

Wasifu wa Hategekimana kabla ya kutua Simba SC

🔸Agosti 2022 hadi sasa, Kocha wa Viungo AS Kigali, ambapo ameshinda taji la Super Cup.

🔸2021-2022 Kocha wa Viungo Polisi Rwanda.

🔸2021 Kocha wa Viungo wa timu ya Taifa ya Wanawake ya Rwanda.

🔸2019-2021 Kocha wa Viungo wa AS Kigali.

🔸2018 Kocha wa Viungo wa timu ya Taifa ya Rwanda chini ya umri wa miaka 23.

🔸2017-2018 Mkurugenzi wa Ufundi na Kocha wa Viungo wa Rayon Sports, na ameshinda taji la Ligi pamoja na kufika Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

🔸2016-2017 Kocha wa Viungo ISONGA Academy FC.

🔸2015 mpaka sasa ni Mkufunzi wa CAF katika Sayansi ya Viungo.

🔸2007-2017 Mwalimu wa Viungo IFAK Secondary School.

🔸 2009-2018 Mkurugenzi wa Ufundi katika Shule ya Gasabo.

🔸2014-2015 Kocha wa Viungo wa Kiyovu FC.

Kocha wa Makipa

Kwa upande wake, Cadena mwenye umri wa miaka 45 raia wa Hispania ana leseni ya Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA) na uzoefu wake ni mkubwa.

Cadena ana wasifu mkubwa ambapo amezifundisha timu mbalimbali barani Ulaya, China pamoja na Falme za Kiarabu kabla ya kuja Afrika.

Cadena amejiunga na Simba akitokea Azam FC alipodumu kwa mwaka mmoja kabla ya mkataba wake kumalizika. Cadena amewahi kukinoa kikosi cha timu ya vijana Sevilla FC ya Hispania msimu wa 2018-2019.

Cadena anachukua nafasi ya Chlouha Zakaria raia wa Morocco ambaye tumeachana naye mwezi uliopita.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa za awali timu ya Simba SC itaondoka na kikosi kamili walichokisajili kwa msimu ujao wa ligi chini ya kocha Roberto Oliviera ‘Robertinho’ na benchi zima la ufundi.

Wachezaji wapya walioasajiliwa wa ndani na wale wa kimataifa nao watakuwa sehemu ya kambi hiyo nchini Uturuki.

Kambi ya Uturuki ni mapendekezo ya benchi la ufundi ambao wanaamini wachezaji watapata utulivu na kuyashika mafundisho watakayopewa.

Kikiwa nchini Uturuki, kikosi hicho kinatarajia kitapata mechi kadhaa za kirafiki ili benchi la ufundi lijue mapokeo ya mafunzo wanayowapa nyota wao kabla ya kurejea nchini mwishoni mwa mwezi huu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news