Yanga SC yazawadiwa milioni 405/-

NA DIRAMAKINI

KLABU ya Yanga imezawadiwa shilingi milioni 405 kutoka kwa mdhamini wake mkuu Sport Pesa Tanzania ikiwa ni zawadi kwa kutwaa Ngao ya Jamii.

Pia, ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC, Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) na kufika Fainali Kombe la Shirikisho Afrika.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Sportpesa Tanzania,Mheshimiwa Tarimba Abbas amesema, wanajivunia kuendelea kuwa wadhamini wakuu wa klabu hiyo yenye mafanikio na uongozi imara.

"Tunajivunia kuendelea kuwa wadhamini wakuu wa klabu hii kubwa yenye mafanikio na uongozi imara. Mafanikio wanayoyapata Young Africans SC yanakuja kutokana na kufanya kazi kwa weledi na kuendesha klabu hii kisasa,"amefafanua Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi Sportpesa Tanzania, Mheshimiwa Tarimba Abbas.

Rais wa Yanga SC, Mhandisi Hersi Said amesema, wanajivunia kwa mafanikio waliyoyapa msimu uliopita huku wakiishukuru Sportpesa kwa kutambua jitihada zao.

Mafanikio hayo yanakuja ikiwa ni siku chache zimepita baada ya Klabu ya Yanga kuzindua jezi zake rasmi za msimu wa 2023-24 jijini Lilongwe nchini Malawi kwa kuwakabidhi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan na mwenyeji wake, Rais wa Malawi Dkt.Lazarus McCarthy Chakwera.

Yanga SC ilikuwa nchini Malawi kwa ajili ya mchezo wa kirafiki na wenyeji, Nyasa Big Bullets katika Uwanja wa Bingu Mutharika jijini Lilongwe kuadhimisha miaka 59 ya Uhuru wa nchi hiyo.

Mabingwa hao wa soka nchini, walilazimishwa sare ya bila kufungana na wenyeji, Nyasa Big Bullets mchezo uliohudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan na mwenyeji wake, Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera Rais wa nchi hiyo ambao walitazama mchezo kwa kipindi cha kwanza pekee.

Aidha, Yanga SC ilipata pigo katika mchezo huo baada ya winga wake chipukizi, Dennis Nkane kuumia dakika ya 21 na kushindwa kuendelea na mchezo, hivyo kukimbizwa hospitali kwa gari maalum la wagonjwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news