TANROADS kukamilisha mzani wa kisasa Mikumi

MOROGORO-Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) ipo mbioni kukamilisha ujenzi wa mzani mpya wa kisasa wa Mikumi uliopo Barabara kuu ya Morogoro-Iringa.

Sambamba na maboresho katika mzani ya Mikese uelekeo wa Barabara ya Dar es Salaam-Morogoro kwa gharama ya shilingi bilioni 1.9, hatua ambayo itakayosaidia kumaliza msongamano wa magari katika barabara hizo.

Mwakilishi wa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Mussa Kaswahili amesema hayo Julai 18,2023 alipozungumza na vyombo vya habari kwa niaba ya Meneja wa TANROADS wa mkoa huo, Mhandisi Alinanuswe L.Kyamba mara baada kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mzani huo ambao kwa sasa umefikia asilimia 80.

Amesema, baada ya kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji na usafirishaji katika barabara ya TANZAM Highway, Serikali iliona mzani uliopo kwa sasa hautoshelezi mahitaji ya kupima magari kwa wingi, hivyo imeamua kufanya maboresho ya mzani uliopo pamoja na kujenga mzani mwingine mpya na wa kisasa ili kuendana na mahitaji ya sasa.

Amesema, maboresho yanayofanyika katika mizani hizo mbili ni pamoja na kuweka vifaa maalum (sensor) ambavyo vitafanya kazi ya kuchuja na kutoa taarifa ya uzito wa gari husika, kama limezidisha mzigo ama la na kama halikuzidisha basi linaendelea na safari moja kwa moja bila kupita katika mzani na lile lililozidisha mzigo litalazimika kupita kwenye mzani.

Mhandisi Kaswahili amemtaja Mkandarasi wa mradi huo ni Kampuni ya kizalendo CGI Construction Company Limited ya mjini Morogoro ambayo imepewa kazi hiyo mwezi Februari, mwaka huu na inatarajiwa kukamilisha mradi Septemba 30,2023.

"TANROADS inapenda kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hasaan kwa kuendelea kuwa karibu na wananchi kwa kutenga fedha na kuzileta kwa ajili ya matengenezo kwenye maeneo yenye changamoto.

"Lengo la upimaji wa magari ni kudhibiti uzito ili barabara zetu ziweze kudumu, natoa wito kwa wananchi hasa wasafirishaji kutoa ushirikiano katika kutunza na kulinda barabara zetu,"amesisitiza Mhandisi Kaswahili.

Ameongeza kuwa, TANROADS na Serikali haijivunii kuwa na tozo nyingi katika mizani, "tunavyotoza kwa wanaozidisha mzigo tunataka kuondosha magari yenye uzito mkubwa ili kulinda barabara zetu ambazo tumejenga kwa gharama kubwa kwa fedha zetu wenyewe, tunataka watu watii na kufuata sheria."

Nao baadhi ya madereva wanaotumia barabara hiyo, Ismail Madunda na Vincent Mkimbila wamesema, kukamilika kwa maboresho na ujenzi wa mzani mpya Mikumi kutasaidia kumaliza msongamano katika maeneo hayo na hivyo kuwafanya wasafiri na wasafirishaji kufika kwenye safari zao kwa wakati.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa eneo hilo, Antony Michael amesema, "Tunaushukuru uongozi wa Rais Samia kwa kutujengea mizani mpya na maboresho yanayofanyika hapa, mradi huu ukikamilika foleni hapa itakuwa byee byee na watu watafika kwenye shughuli zao mapema kabisa."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news