Tunatamani Kiswahili kizungumzwe duniani kote-BAKITA

NA GODFREY NNKO

KATIBU Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Bi.Consolata Mushi amesema,ni matarajio yao kuona lugha ya Kiswahili inazungumzwa duniani kote siku zijazo.

Pia amesema, Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani mwaka huu (MASIKIDU 2023) ni ya pili ambapo kwa mara ya kwanza yalifanyika mwaka jana.

Mushi amesema hayo Julai 4, 2023 katika Kongamano la Wahariri lililoandaliwa na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) ambalo liliangazia juu ya nafasi ya wahariri katika kusimamia matumizi ya Kiswahili sanifu kwenye vyombo vya habari nchini.

Kupitia kongamano hilo, mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdullah ambapo limefanyikia Ukumbi wa Sheikh Idris Abdul Wakil uliopo Kikwajuni jijini Zanzibar.

Aidha, kongamano hilo ni maandalizi ya kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani ambayo yatafanyika Julai 7, 2023 huku kauli mbiu ikiwa ni “Kiswahili Chetu; Umoja Wetu”.

"Haya ni maadhimisho ya pili ya Siku ya Kiswahili Duniani ambayo tumeyafupisha na kuyaita MASIKIDU, yanafanyika duniani kote tarehe saba Julai mwaka 2023,kwa hapa Tanzania yatafanyika Zanzibar.

"Maadhimisho haya yanatokana na uamuzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) wa Novemba 2021 kuwa tarehe saba ya kila mwezi Julai kuwe na Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani.

"Na, Kiswahili kimekuwa lugha ya kwanza Afrika kupewa hadhi na heshima hiyo, uamuzi huo ulitolewa wakati wa mkutano wa 41 wa nchi wananchama wa shirika hilo, uliofanyika jijini Paris nchini Ufaransa.

Aidha, maadhimisho haya yanafanyika kwa mara ya pili, kwani baada ya uamuzi huo wa UNESCO wa Novemba 2021 Maadhimisho ya Kwanza ya Siku ya Kiswahili Duniani yalifanyika mwaka 2022.

"Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yameandaliwa na wizara zote mbili yaani Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kupitia mabaraza yake yaani Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA).

"Aidha, maadhimisho haya yameandaliwa na taasisi na idara zinazojihusisha na lugha ya Kiswahili na wadau wa lugha ya Kiswahili kwa ujumla.

"Vile vile, maadhimisho haya yamefanikiwa kutokana na jitihada na michango ya wadau mbalimbali wanaounga mkono lugha ya Kiswahili, mwaka huu tutakuwa na wageni kutoka nchi mbalimbali.

"Na mwaka huu wametia fora kwa sababu tutapokea wageni wengi sana wakiwemo mabalozi mbalimbali,lakini leo ni siku maalumu kwa ajili ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

"Kwa nini Jukwaa la Wahariri, kabla ya kufikia kilele cha Siku ya Maadhimisho ya Kiswahili Duniani yaani tarehe 7 Julai, 2023 wadau wa Kiswahili watashiriki katika matukio mbalimbali yanayohusu maendeleo ya lugha ya Kiswahili duniani.

"Leo tunashirikiana na wahariri, tukiamini kwamba wao wamebeba silaha kubwa, katika kusimamia matumizi ya lugha na matumizi ya hayo ni matumizi fasaha na sanifu ya lugha ya Kiswahili.

"Tumekusanyika hapa tuweze kujadiliana, kuangalia namna ambavyo tutaweza kuitumia silaha hiyo kusogeza mbele zaidi Kiswahili chetu, leo tunasema ni lugha kubwa kabisa duniani, lakini tunatamani miaka miwili mitatu ijayo, kiwe Kiswahili cha Dunia.

"Wahariri watapata fursa ya kujadiliana kuhusu uhariri katika lugha ya Kiswahili, kuwapatia wahariri maarifa kuhusu matumizi fasaha na sanifu ya lugha ya Kiswahili. Lakini, kutambua jitihada zinazofanywa na wahariri katika maendeleo ya Kiswahili na pia kujadiliana kuhusu chanagmoto za uhariri kwa Kiswahili na tupate utatuzi wake.

"Matarajio ni kuwa na mabadiliko katika matumizi ya Kiswahili fasaha na sanifu ambapo vyombo vingi vya habari vinatarajiwa kuwa na matumizi bora zaidi ya Kiswahili, matarajio mengine ni kupungua kwa makosa katika vyombo vya habari.

"Na, pia kuundwa kwa Jukwaa la Pamoja kati ya Wahariri na Wataalamu wa Lugha ya Kiswahili kwa ajili ya kutatua chanagamoto zinazokabili taaluma ya uhariri kwa Kiswahili,"amefafanua kwa kina Katibu Mtendaji wa BAKITA.

BAKITA

Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ni Shirika la Umma ambalo kwa kawaida huwa chini ya wizara yenye dhamana ya Utamaduni.

Baraza liliundwa kwa Sheria ya Bunge Na. 27 ya mwaka 1967 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 1983 na 2016. Sheria hii inalipa baraza mamlaka ya kusimamia na kuratibu shughuli za wadau wote wanaokuza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news