Ufugaji samaki unalipa, jikiteni huko-Mheshimiwa Mhagama

RUVUMA-Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma ameshauri watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea kuanza kutenga maeneo yatakayosaidia wananchi kujishughulisha na utengenezaji wa mabwawa ya ufugaji wa samaki ambayo yatachochea uchumi na kuongeza wigo wa mapato kwa halmashauri.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Peramiho akitembelea eneo la mradi ili kujionea hatua za ujenzi wa eneo la Mradi wa Shamba Darasa la Ukuzaji wa Viumbe Maji katika Kijiji cha Mpitimbi B.

Ameitoa wito huo Julai 14,2023 wakati alipotembelea kujionea Mradi wa Shamba Darasa la Ukuzaji wa Viumbe Maji unaoendelea kujengwa na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Kata ya Mpitimbi Halmashauri ya Wilaya ya Songea.

Waziri Mhagama ameridhishwa na hatua ya ujenzi wa shamba la darasa la ukuzaji wa viumbe hai, amesema, "tunaweza kutumia mabwawa ya ufugaji wa samaki kama chanzo cha ajira na uchumi kwa wananchi wa Mpitimbi B.

“Mhe. Rais, Dkt, Samia Suluhu Hassan ana maono ya mbali sana, ametupatia mradi ambao utasaidia kuzalisha mbegu na mafunzo, tunatakiwa tuanze kujiandaa kwa kutengeneza mabwawa.”

Amefafanua mradi utakapokamilika, wananchi wawe na miundo mbinu yao ya mabwawa ya ufugaji wa samaki tayari, ili mafunzo yatakapokuwa yanafanyika wawe wanachukua vifaranga na kuweka kwenye mabwawa yao.

"Tunaweza tukatumia mikopo ya Halmashauri kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kuweza kutengeneza mabwawa yao ya ufugaji wa samaki.
“Tunapaswa tuwe na mabwawa mengi ya samaki kushoto na kulia mwa eneo la mradi yatakayomilikiwa na vijana, akinamama na wazee ambayo samaki watafugwa kisasa na watakuwa na uzito mzuri," alisema Waziri Mhagama.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Mhe.Menas Komba amesema,halmashauri inaanda andiko la kimkakati kwa ajili ya kupata fedha ya kuendeleza lambo kubwa la maji lilopo katika kijiji cha Mpitimbi B ambalo linahitaji fedha zaidi ya shilingi milioni 500.

Amefafanua kwamba, ujenzi wa lambo hilo utaenda sambamba na Halmashauri kutaratibu kupitia Halmashauri ya kijiji maeneo ambayo wananchi watajenga mabwawa ya kufugia samaki.
Awali katika taarifa Mhandisi Msimamizi wa Mradi, kutoka Halmashauri ya Songea, Bi.Flora Tairo alisema, mradi uko katika hatua ya ukamilishwaji, kwa majengo na upandaji nyasi kwenye kingo za mabwawa.

Ameongeza kuwa, mradi utakapokamilika utakuwa na mabwawa manne, uzio, darasa la mafunzo, stoo pamoja na maliwato. 

Akieleza umuhimu wa mradi, Bi, Agatha Mapunda mkazi wa Mpitimbi B amesema, wanamshukuru Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mradi na wamejiandaa kupokea mafunzo

Amesema, mradi utawasaidia kupata lishe bora na fursa za biashara zitakazojitokeza wakati wa uzalishaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news