Ukibeba mzigo mzito, unapewa na mabega ya kustahimili

NA ADELADIUS MAKWEGA

WAKRISTO wameambiwa kuwa kama kila binadamu angekuwa na moyo mwema walio nao watoto wa kuheshimu wazazi wao, basi duniani kungekuwa eneo jema na salama zaidi, maana mtoto anaamini kuwa baba,mama au mzazi wake anafahamu na ana uwezo wa kila kitu na hata kumlinda na baya lolote linalojaribu kumsogelea. 
Hayo yamesemwa na Padri Antony Ndikumulimo katika misa ya Jumapili ya 14 ya Mwaka A wa Liturjia ya Kanisa katika Kanisa la Bikira Maria, Malkia wa Wamisionari, Parokia ya Malya Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza leo Julai 9, 2023.

“Kwa desturi za watoto wa zamani akilala, usiku mzazi alikuwa akimuamsha na kumpeleka uani kwa ajili ya haja, akiwa anajisaidia alikuwa anauliza mama au baba upo?.

"Naye mama,baba au mzazi wake anajibu, mwanangu nipo, hiyo mwanangu nipo ni kauli muhimu sana, yenye maana tele, inayompa amani kubwa. Akimaliza wanarudi ndani ya nyumba, akishuhudia mzazi wake kamlinda kwa hatari zote. Hata binadamu tunapaswa tuige moyo huo wa watoto. Kwetu sote Mungu anatulinda kwa yote kama tunamtegemea kwa kumuita.” 

Padri Ndikumulimo aliongeza kuwa, katika maisha yetu, watu wengi wanakosa ujasiri wa kusimama kifua mbele na kusema kuwa jamani mjifunze kwake hata kama wana tabia njema, kuogopa kufanya hivyo kunatokana na sababu nyingi, mojawapo utaonekana kuwa unajinasibu na kujigamba mbele za watu. 
Akiendelea kuhubiri Padri Ndikumulimo kutoka jimbo Katoliki la Rulenge amesema, “Yesu anatualika tujifunze upole, unyenyekevu na ukarimu wake, maana yeye ndivyo alivyo na akaongeza ahadi kuwa ataifanya mzigo yetu mizito kuwa miepesi.” 

Padri Ndikumulimo huku akihubiri kwa mifano ya jamii halisi katika misa hiyo ya Dominika iliyoanza saa 12 ya asubuhi alisema kuwa watu wa Tabora ambayo wengi ni Wanyamwezi wanasema mzigo mzito mpe Mnyamwezi na siyo Msukuma, Wasukuma na Wanyamwezi ni ndugu na makabila jirani sana, lakini pia kuna watu wa Kagera wao wana msemo huu, 
“Mungu akikujalia mzigo mzito, anakujalia na mabega mazito ya kustahimili mzigo huo.” 

Ukiwa na mzigo mzito kichwani unautua katika mabega ambayo yanayouwezo wa kuubeba, maana yake Mwenyezi Mungu hawezi kukufungia milango unapokuwa na changamoto zako. Ndiyo maana katika injili ya dominika ya leo Yesu atatualika sote kwenda kwake wale wote wenye mizigo na yeye atatupumzisha.

Misa hiyo pia ilikuwa na nia na maombi kadhaa huku masista na mafteli wazawa wa parokia ya Malya wakijitambulisha kwa waamini. 
Kwa jumla hali ya hewa ya eneo la Malya na viunga vyake kwa juma zima ni ya baridi kiasi wakati wa asubuhi na jua kali wakati wa mchana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news