RC Senyamule aguswa na ufanisi Wilaya ya Mpwapwa

DODOMA-Halmashauri ya Wilaya Mpwapwa mkoani Dodoma imedhamiria kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa mwaka huu wa fedha (2023/2024) baada ya kubuni chanzo kitakachoimarisha mapato hayo kwa ukamilifu.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Mhe. Sophia Kizigo amesema hayo leo katika Mkutano Maalumu wa Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo lilijadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha unaoishia 2022/2023.

Amesema, Halmashuri ya Wilaya ya Mpwapwa imenunua kifaa maalumu cha kisasa cha kidijitali (RTK – GPS) kwa gharama ya Shilingi Milioni 37.5 kwa ajili ya upimaji wa viwanja jambo ambalo litaongeza mapato katika halmashauri hiyo na kuwezesha Wilaya hiyo kupima viwanja vingi kwa wakati mmoja.
Akizindua kifaa hicho Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule ametoa pongezi kwa Wilaya hiyo kwa kuona umuhimu wa kuwa na mkakati endelevu wa kupanga Wilaya ya Mpwapwa kupitia uuzaji wa viwanja.

“Mwaka huu wa fedha unaoisha mlikusanya mapato kwa asilimia 92 niwapongeze sana ni Imani yangu kuwa asilimia 8 iliyobaki na zaidi itakamilika kupitia mkakati huu mliobuni wenyewe kama chanzo kimojawapo cha mapato. Nimefurahi kwakuwa mmejipanga kutumia kifaa hiki cha kisasa cha RTK - GPS hii kwa shughuli za upimaji, nasisitiza upangaji na umilikishaji ufanyike ili kuleta iliyokusudiwa tija,” Senyemule amesisitiza.
Awali Mhe. Senyamule pia ameshiriki katika mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani kwa lengo la kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu za mwaka 2021/2022) kwa kila Halmashauri.

Aidha, Senyamule ameagiza Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kuhakikisha kuwa hoja zote za ukaguzi zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na zile za Mkaguzi wa ndani, zinashughulikiwa ipasavyo na kupatiwa majibu stahiki ili ziweze kuhakikiwa na kufungwa kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na maelekezo yaliyotolewa na Serikali.
“Mheshimiwa Mwenyekiti na Menejimenti ya Halmashauri hapa Mpwapwa ni lazima mje na Mkakati madhubuti wa kumaliza hizi hoja 53 zilizosalia, iwe ni agenda ya kudumu katika vikao vyenu kujua hoja ngapi zimemalizika na ngapi bado ili muweze kuwa na mkakati madhubuti wa kusimaliza,” Senyamule amesisitiza.

Senyemule ametoa rai kwa Halmashauri hiyo kuzingatia ipasavyo Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali iliyopo katika uendeshaji wa shughuli za kila siku ili kupunguza hoja za ukaguzi zisizokuwa za lazima.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news