Urusi yaonesha mwelekeo mpya wa kiuchumi Afrika, Waziri Mkuu asema haya

ST.PETERSBURG-Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Urusi imeahidi kushirikiana na Afrika kuboresha uchumi ikiwemo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na viongozi walioshiriki katika mkutano wa pili wa kilele baina ya wakuu wa nchi na serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi uliofunguliwa na Rais wa Shirikisho la Urusi, Vladimir Putin, kwenye kituo cha mikutano na maonesho cha Expo Forum kilichopo St. Petersburg, Urusi Julai 28, 2023. Waziri Mkuu Alimuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano huo.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

“Mwelekeo wa mkutano wa leo ilikuwa ni kuona namna gani tunaweza kuboresha uchumi wa nchi za Afrika kwa pamoja na Urusi.

"Wao wametoa mwelekeo wa namna ambavyo wataweza kushirikiana na nchi za Afrika kuboresha uchumi wa kila nchi na sisi tumeeleza mkakati wa kiuchumi kwenye nchi yetu ambao Rais Putin ameuridhia;

Ameyasema hayo leo Ijumaa, Julai 28, 2023 baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Pili wa Kilele baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi ambako alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mkutano huo umefanyika kwenye kituo cha mikutano na maonesho cha Expo Forum, jijini St. Petersburg nchini Urusi.

Waziri Mkuu amesema, Tanzania itaendelea kuimarisha miundombinu ya usafirishaji kwa lengo la kuboresha uchumi na biashara kwa kutumia rasilmali zake ikiwemo madini, maliasili na kilimo hasa upatikanaji wa mbolea.

“Tumesisitiza pia matumizi ya nishati mbadala kama njia muhimu ya kuwawezesha wananchi wa vijijini ili nao wamudu kutumia nishati mbadala kukuza uchumi wao,” amesema.

Amelitaja eneo jingine kuwa ni kukuza biashara ya mazao baina ya Afrika na Urusi ambapo yenyewe inaweza kuwa soko la moja kwa moja ama kwa kuwatumia marafiki zake. “Ili kufikia hayo, jitihada za kila nchi kwenye kilimo zimesisitizwa. Tanzania tumeeleza mkakati wa kukuza kilimo ikiwemo umwagiliaji. Pia tunahitaji mbolea, madawa na vitendea kazi ili tufanikiwe kwa kasi zaidi.”

Waziri Mkuu aliwaeleza viongozi hao wa Afrika juu ya Mkakati wa Rais Dkt Samia wa kutoa elimu bure na vifaa vya kufundishia kwa lengo la kuwapunguzia mzigo wazazi.

Mapema, akifungua mkutano huo, Rais wa Urusi, Vladmiri Putin alisema nchi za Afrika zimekuwa na mahusiano mazuri na ya muda mrefu na Urusi na kwamba nchi hiyo imekuwa ikiendelea kutoa misaada bila vikwazo kwenye maeneo mbalimbali.

Akitoa mfano, Rais Putin amesema nchi 40 kutoka Afrika zimenufaika na misaada ya kijeshi ikiwemo mafunzo. “Ukaribu wa mahusiano kati ya Afrika na Urusi unazidi kuongezeka. Tunatarajia kufungua balozi zetu kwenye nchi nyingine kama vile Burkina Faso na Equatorial Guinea. Pia tunatarajia kufufua vituo vya utamaduni vya Kirusi. Hivi sasa, vituo kama hivyo vinafanya kazi kwenye nchi nane tu,” alisema.

Alisema nchi hiyo itaendelea kutoa misaada kwenye sekta ya kilimo ili kuimarisha upatikanaji wa chakula. “Jana ndiyo maana nilitoa ahadi ya kuzipatia nafaka nchi sita tani kati ya 25,000 hadi 50,000 na kwamba zitasafirishwa bure.”

Nchi hizo ni Mali, Burkina Faso, Zimbabwe, Jamhuri ya Kati, Eritrea na Somalia. Alisema Urusi imepanga kutoa dola za marekani milioni 90 kwa nchi za Afrika kulingana na maombi ambayo yamepokelewa kutoka Umoja wa Afrika (AU).

Akichangia mada kwenye mkutano huo, Rais wa Comoro, Azali Assoumani ambaye pia ni Mwenyekiti wa AU na Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano huo alisema vijana wa kiafrika wana umahiri katika fani mbalimbali na wanahitaji kupata programu za kuwawezesha kimitaji (start-ups programmes).

“Kuna suala la utoaji mafunzo na teknolojia za kidijitali ambalo Urusi imejaliwa kuwa nalo. Tunahitaji tuwe na mpango madhubuti ambao utawezesha kuwajengea uwezo vijana wengi wa Kiafrika tulionao,” alisisitiza.

Naye Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alisema mwishoni mwa mkutano huo watoke na tamko la kisera ya kwamba mataifa ya nje yanapaswa kununua kutoka Afrika bidhaa zilizosindikwa badala ya mazao ghafi.

“Napendekeza tutoke na tamko la kisera kwa nchi zote kwamba wakija kwetu wanunue chokoleti badala ya kakao, kahawa iliyosindikwa badala ya ghafi na bidhaa za chuma zilizosanifiwa badala ya chuma ghafi,” alisisitiza Rais huyo.

Alisema, Bara la Afrika linahitaji zaidi kupata teknolojia ya kilimo cha umwagiliaji na uzalishaji wa mbolea ili liwe na uhakika wa kuzalisha chakula. “Kitu kingine kikubwa tunachohitaji ni kupata uhakika wa masoko ndani ya bara la Afrika na nje ya mipaka yetu. Tukijenga viwanda vya kuongeza thamani za mazao na bidhaa zetu, tutafanikiwa kuondoa tatizo la ajira kwa vijana wetu,” alisema.

Kwa upande wake, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa alisema umefika wakati wa mataifa mengine kukubali kuwa nchi za Afrika zimeanza kutengeneza hatma yao na kwamba anaunga mkono hoja ya Rais Museveni ya kutouza bidhaa ghafi nje ya nchi zao.

Ili kuhakikisha kuwa maamuzi ya kikao hicho yanafanyiwa kazi kwa haraka, Rais Ramaphosa alipendekeza kuwa ni lazima waandae mpango wa ufuatiliaji na tathmini. Alitumia fursa hiyo kuwaalika viongozi wenzake washiriki Mkutano Mkuu wa 15 wa BRICS unaotarajiwa kufanyika Afrika Kusini, Agosti 22-24, mwaka huu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news