Wanachuo Malya ni mabalozi wa michezo nchini

NA ADELADIUS MAKWEGA

WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini,Mheshimiwa Balozi Dkt.Pindi Chana, Julai 14, 2023 ametembelea Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya na kukagua miradi kadhaa ya maendeleo inayoendelea kujengwa chuoni hapo, chini ya fedha za Serikali Kuu zinazotolewa kila bajeti ya kila mwaka na kusema kuwa anawapongeza sana wanachuo wa chuo hicho kwa kuchagua kusoma michezo na wao ni mabalozi wa michezo nchini. 
Akizungumza huku akishangiliwa na wanachuo hao, Waziri Dkt. Chana alibainsiha kuwa,“Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inatamka wazi kuwa michezo inapaswa kuendelezwa na kusomea michezo ni mojawapo ya maendeleo hayo. Ualimu wa michezo ni muhimu sana maana hata katika tiba unatumika pia. Juzi kuna mgonjwa amenipigia simu, akiomba namba ya mwalimu wa mazoezi ya viungo ili amsaidie maana alipewa maagizo daktari kufanya mazoezi baada ya tiba.” 

Katika kikao hicho Waziri Dkt. Chana alipata nafasi ya kujibu maswali kadhaa yaliyoulizwa na wanachuo hao ambapo Ladislausi Lunguya, Rais wa Serikali ya Wanachuo na Ndinagwe Sungura Makamu wa Rais wa Serikali hiyo ya Wanachuo waliomba kupatiwa vifaa vya michezo. 
Waziri Dkt. Chana alijibu kuwa kwa hakika hoja hiyo ya vifaa tayari alielezwa na Mkuu wa Chuo Richard Mganga katika ripoti aliyomsomea asubuhi ya Julai 14, 2023 na changamoto hizo zitapatiwa ufumbuzi.
Kwa upande wao wanachuo Lucy Malisa na Eliasi Mashenzi ambao walifunga ukurasa huo wa maswali, kwa pamoja wao walijikita katika kuomba kuondolewa kwa utaratibu wa kushushwa madaraja kwa walimu walisomea michezo pindi wanapohitimu na kurudi kazini wakiwa mafisa michezo, huku wakiomba kuongezwa kwa wakufunzi chuoni hapo maana mkufunzi mmoja anakuwa na mzigo mkubwa wa vipindi na pia wakishauri wale wanachuo wasio na ajira wanasoma chuoni hapo wapatiwe ajira wanapohitimu. 
“Tayari Wizara yangu na wizara zote zinazohusika na suala na wale walimu wanaopanda na kuwa maafisa michezo suala lao linafanyiwa kazi na tumeshafanya vikao kadhaa vya pamoja katika suala hilo.” 

Awali wakati wa kumkaribisha Waziri Dkt. Chana, Mkuu wa Chuo hiki ndugu Richard Mganga alimshukuru Waziri Dkt. Chana kwa kufika hapo na kuzungumza na wanachuo hao 261, huku akitia shime kuwa michezo inalipa na wanachuo kadhaa sasa wameshaonja utamu na matunda ya michezo kwa kujipatia fedha wakiwa chuoni hapo kwa kuchezesha mashindani mbalimbali.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini Ali Mayay Tembele alisema kuwa anampongeza Waziri Dkt. Pindi Chana kwa kujituma katika kuikamilisha adhima ya taifa ya maendeleo ya michezo nchini. Akiwa chuoni hapo pia Waziri Dkt. Chana aliweza kutazama michezo mbalimbali iliyoandaliwa na wanachuo hao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news