Waziri Mkuu:DMO simamia ujenzi wa Kituo cha Afya Mkunwa

MTWARA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemtaka Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara, Dkt. Matayo Malaika ahakikishe anasimamia ujenzi wa Kituo cha Afya Mkunwa ili kikamilike ifikapo Oktoba, 2023.

Ametoa agizo hilo Julai 8, 2023 wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Mkunwa mara baada ya kukagua ujenzi wa kituo hicho, kilichopo Halmashauri ya Mtwara Vijijini mkoani Mtwara.

“Nimekagua ujenzi wa kituo hiki cha afya, nimekuta vifaa vimejaa humo ndani, rangi, masinki ya mikono, vyoo, gutters, marumaru, saruji, vyote vipo na vinataka kuharibika. Mganga Mkuu simamia huu ujenzi na umshauri vizuri Mkurugenzi. Nataka hatua zote zilizobakia zikamilishwe na hapa ni lazima pawe na watu sababu kuna mali za umma.

“DMO mnakaa sana ofisini badala ya eneo la ujenzi, simamia kituo cha afya hiki kikamilike, una vituo vya afya vitatu na hiki ni cha nne, milango imekaa tu, jengo lipo kwa nini usiweke hii milango kwenye maeneo yake?,” alisisitiza na kuhoji Waziri Mkuu.

Amemtaka Mhandisi wa Halmashauri hiyo ashirikiane na Mganga Mkuu huyo kuandaa mapitio ya mradi na wapeleke maombi yao Ofisi ya Rais TAMISEMI ili waweze kupatiwa fedha za kukamilisha majengo ya kituo hicho ambacho amesema kinapaswa kuwa na hadhi ya hospitali ya Halmashauri kutoka na umaalumu uliopo.

“Kwa sababu hapa kuna vyumba vingi, angalieni uwezekano wa kuwa na chumba cha upasuaji cha wagonjwa wa kawaida tofauti na kile kilichopo kule kwenye jengo la akinamama. Pia katika mapitio yenu, wekeni wodi tatu ikiwemo wodi ya wanaume, wodi ya wanawake na ya magonjwa mchanganyiko,” amesisitiza.

Amewataka wakamilishe ujenzi huo kwa sababu tayari Serikali ilishatenga sh. milioni 300 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya kituo hicho.

Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi kwa Waziri Mkuu, Dkt.Malaika alisema mradi huo ukikamilika utahudumia vijiji sita vya kata ya Mkunwa na kata jirani za Mayanga, Muungano na Dihimba.

Alisema Septemba, 2021 Halmashauri ilipokea shilingi milioni 250 kwa ajili ya jengo la wagonjwa wa nje (OPD), maabara na kichomea taka. “Juni, 2022, Halmashauri ilipokea fedha za awamu ya pili shilingi milioni 250 kwa ajili ya wodi ya wazazi na jengo la upasuaji, njia ya kutembelea na jengo la kufulia yenye hadhi ya kituo cha afya.”

Alisema kutokana na maamuzi ya kuhamishia hospitali ya wilaya kwenya kata ya Nanguruwe, Halmashauri iliomba kibali cha kubadilisha matumizi ili kuendeleza ujenzi wa wodi ya wazazi na jengo la upasuaji vyenye hadhi ya Hospitali ya Wilaya ambapo ujenzi wake ulianza Novemba, 2022.

“Kwa sasa ujenzi upo hatua ya ukamilishaji na kazi zinazoendelea ni skimming, ufungaji wa gypsum boards, uwekaji wa fremu za milango na ujenzi wa marumaru.”

Majengo mengine ambayo yalianza kujengwa na yako kwenye hatua ya msingi ni jengo la mionzi, la maabara na la kufulia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news