Askofu Dkt.Malasusa aibuka kidedea tena KKKT

ARUSHA-Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 21 wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wamemchagua kwa kishindo Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dkt.Alex Malasusa kuwa mkuu mteule mpya wa KKKT kupokea nafasi ya Askofu Dkt.Frederick Shoo aliyestaafu baada ya kumaliza muda wake wa uongozi.

Mwenyekiti wa uchaguzi huo uliofanyika Arusha, Askofu Amon Mwenda amesema, Askofu Malasusa ameshinda kwa kura 167 sawa na asilimia 69.3 ya kura zote 241 zilizopigwa huku Askofu Abednego Kesho Mshahara akipata kura 73 sawa na asilimia 30.3.

Askofu Malasusa anarejea kwenye nafasi hiyo tena,nafasi ambayo alikwishaitumikia kwa uongozi kati ya mwaka 2007 hadi 2015 alipomaliza muda wake na kumkabidhi Dkt.Shoo.

Historia inaonesha kuwa, Askofu Malasusa alizaliwa Aprili 18, 1961 katika Kijiji cha Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya.

Ni mtoto wa pili katika familia ya watoto nane ya marehemu Mchungaji Gehaz Japhet Malasusa na Subilaga Timoth Malasusa.

Pia, alisoma katika shule mbalimbali za msingi kutokana na kuhama kwa wazazi. Mwaka 1976 alihitimu Shule ya Msingi Bungo Morogoro na baadae kujiunga na masomo ya sekondari katika Shule ya Kigurunyembe mwaka 1977.

Baada ya masomo ya sekondari alijiunga na Chuo cha Uongozi wa Biashara na baadae alijiunga na masomo ya uhasibu.

Askofu Malasusa alifanya kazi katika mashirika mbalimbali likiwemo Shirika la Akiba la Taifa kwa miaka minne na baadae kujiunga na masomo ya Theolojia.

Katikati ya masomo hayo, alipata fursa ya kusoma vyuo vingine vya nje katika mpango wa kubadilishana wanafunzi na kuhitimu mwaka 1995.

Masomo na mafunzo mengine aliyowahi kupata ni pamoja na usimamizi na utawala, pia mafunzo ya dinimbali mbali.Askofu Malasusa alibarikiwa kuwa Mchungaji katika Dayosisi ya Mashariki na Pwani Septemba 3, 1995.

Mwaka 1996 alifunga ndoa na Ericah Simon Nkonoki na kubarikiwa watoto watatu, Miriam, Michael na Mercy.

Pia Askofu Malasusa amefanya kazi za kikuhani Chuo Kikuu (Udsm), Usharika wa Mburahati, Usharika wa Yombo, Usharika wa Msasani na kuwa Mkuu wa Jimbo la Kinondoni (sasa Kaskazini). Pia Askofu amepata kuwa Msimamizi wa Kiroho (Chaplain) wa Seminari ndogo Kisarawe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news