CHAKO KINAKUSITIRI

NA LWAGA MWAMBANDE

AGOSTI 22, 2023 Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema, akiba ya fedha za Kigeni hadi kufikia Agosti 21, 2023 ilikuwa dola za Marekani bilioni 5.41, kiasi ambacho kinatosha kuagiza bidhaa na huduma za nje kwa miezi minne na siku 27.

Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi wa Benki Kuu, Dkt.Suleiman Missango aliyasema hayo kwa niaba ya Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba katika kikao kazi baina ya wahariri wa vyombo vya habari nchini jijini Dar es Salaam ambapo alisema, changamoto ya upungufu uliopo sasa wa fedha za kigeni ni himilivu kwa kuwa akiba ipo ya kutosha.

Pia, alitumia nafasi hiyo kuitaka jamii kutambua kuwa shughuli za kununua au kuuza fedha za kigeni nchini zinatakiwa kufanywa na taasisi za fedha zilizoidhinishwa na Benki Kuu ya Tanzania pekee.

Hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Kigeni 1992 (4), lengo likiwa ni kukabiliana na biashara haramu ya fedha za kigeni ikiwemo soko lisilo rasmi nchini na mtu anayefanya biashara ya kuuza au kununua fedha za kigeni ni kinyume cha sheria.

Ili Taifa liendelee kustawi kiuchumi na wananchi kuneemeka zaidi,Benki Kuu inatoa wito kwa wananchi kuongeza matumizi ya bidhaa na huduma zinazozalishwa hapa nchini.

Kwa mujibu wa, BoT hatua hii itapunguza mahitaji ya fedha za kigeni, kuimarisha shughuli za kiuchumi, na kuongeza kipato kwa wananchi.

Mbali na hayo, BoT inatoa wito kwa wazalishaji nchini kuongeza uzalishaji na ubora wa bidhaa na huduma zinazozalishwa ili kupunguza uhitaji wa kuagiza bidhaa au huduma kutoka nje na kuongeza mapato ya fedha za kigeni.

Aidha, mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anaendelea kusisitia kuwa,wananchi tukiendelea kuwekeza nguvu ya matumizi ya gesi asilia nchini kwa majumbani, magari na matumizi ya bidhaa za ndani itasaidia kuokoa matumizi ya fedha za kigeni zinazotumika kuagiza nishati ya mafuta kutoka nje ya nchi. Edelea;


1.Chako kinakusitiri, cha mwingine utitiri,
Hayo maneno fikiri, yana ukweli dhahiri,
Fanya bila kusubiri, utaishia pazuri,
Vitu unavyozalisha, jisikie kutumia.

2.Gesi asilia ipo, kwa nishati hiyo nzuri,
Mafuta lizeti yapo, wala hufungi safari,
Na tena masoko yapo, huduma yanasubiri,
Vitu unavyozalisha, jisikie kutumia.

3.Sasa vipi Dasalamu, na wingi huo magari,
Gesi asilia tamu, vituo vya kusubiri?
Vipi sisi wanadamu, twatumika kwa kafiri?
Vitu unavyozalisha, jisikie kutumia.

4.Dasalamu Tanzania, tukiicheki vizuri,
Hii gesi asilia, nusu magari tumia,
Wapi tutapofikia, si utamu wa futari?
Vitu unavyozalisha, jisikie kutumia.

5.Eti asubuhi chai, kitafunwa twakariri,
Tunalima mapapai, eti epo ndio nzuri,
Huko wanadai dola, za kusubirisubiri,
Vitu unavyozalisha, jisikie kutumia.

6.Ngano ya kuagizia, eti chapati ni nzuri,
Dola za kuagizia, ya Marekani fahari,
Ipo mihogo tumia, upate nguvu ngangari,
Vitu unavyozalisha, jisikie kutumia.

7.Tukizalisha wenyewe, bidhaa huduma nzuri,
Faida yetu wenyewe, yetu yabaki mazuri,
Wengine na wachachawe, sisi hatupati shari,
Vitu unavyozalisha, jisikie kutumia.

8.Kuvipenda vya kigeni, hata kama ni vizuri,
Ni kujiweka rehani, mwishoni kuwe hatari,
Wageni wana mpini, kwako makali na shari,
Vitu unavyozalisha, jisikie kutumia.

9.Sasa fedha za kigeni, kuadimika ni shari,
Sababu wala si ngeni, kwamba nakupa habari,
Pendapenda vya kigeni, mwisho twavuna shubiri,
Vitu unavyozalisha, jisikie, kutumia.

10.Tukizalisha zaidi, vile vya kwetu vizuri,
Tutakuwa wakaidi, vya kigeni vyenye shari,
Hatutapata baridi, tukikosa vya Hangari,
Vitu unavyozalisha jisikie kutumia.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news