Mgogoro wa ardhi uliodumu miaka 22 kati ya KKKT na wanakijiji Njombe watatuliwa

NA MUNIR SHEMWETA
WANMM Njombe 

SERIKALI imehitimisha rasmi mgogoro uliodumu zaidi ya miaka 20 baina ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Njombe na wananchi wa Kijiji cha Magoda na Mtaa wa Lunyanywi katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe mkoani Njombe.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akizungumza katika kikao cha kutatua mgogoro kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Njombe na wananchi wa Kijiji cha Magoda na Mtaa wa Lunyanywi mkoani Njombe Agosti 9, 2023.

Uamuzi huo unafuatia maridhiano yaliyofikiwa baina ya pande zote za mgogoro baada ya timu iliyoundwa na kuhusisha wawakilishi kutoka kwa wadai na wale wa KKKT,wataalam wa ofisi ya ardhi mkoa na halmashauri, TAKUKURU, Polisi na ofisi ya usalama mkoa kuwasilisha ripoti yake.

Akihitimisha mgogoro huo Agosti 9,2023 mkoani Njombe, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula alisema, katika kuhitimisha mgogoro huo wananchi wanaodai wanatakiwa kupokea viwanja 400 kama kifuta jasho pamoja na urasimishaji wa makazi kwa wale walioingia kwenye eneo lenye mgogoro bila kufuata taratibu.
Sehemu ya washiriki wa kikao cha kutatua mgogoro kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Njombe na wananchi wa kijiji cha Magoda na mtaa wa Lunyanywi mkoani Njombe kilichoongozwa na Waziri wa Ardhi, Dkt.Angeline Mabula, Agosti 9, 2023. 

‘’Pokeeni urasimishaji kwa wale walioingia bila utararibu kama kifuta jasho kwa kuwa mmeingia bila kufuata taratibu,’’alisema Dkt.Mabula.
Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini, Deo Mwanyika akizungumza kwenye kikao cha kutatua mgogoro kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Njombe na wananchi wa Kijiji cha Magoda na Mtaa wa Lunyanywi mkoani Njombe kilichoongozwa na Waziri wa Ardhi, Dkt.Angeline Mabula Agosti 9, 2023.

Aidha, Waziri wa Ardhi amelitaka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisis ya Kusini Njombe kuhakikisha linalinda maeneo yake na kubainisha kuwa, hakuna wa kuwalindia maeneo yake na itakapotekea maeneo ya kanisa hilo kuvamiwa basi suala hilo lipelekwe katika vyombo vya sheria na si Wizara ya Ardhi.
Awali wananchi wa Kijiji cha Magoda na Mtaa wa Lunyanywi walimueleza Waziri wa Ardhi masikitiko ya kuwa na kilio cha muda mrefu kuhusu mgogoro huo uliodumu kwa takribani miaka 22 bila kupatiwa ufumbuzi.

Walieleza kuwa, mgogoro huo una sura mbili na kuzitaja kuwa ni maeneo waliyodai kumiliki ndani ya scheme na maeneo ambayo wakati Kanisa la KKKT linapima ili kupata hati lilivuka na kuingia kwenye maeneo ya watu binafsi.

Aidha, wananchi hao wametaka kutambuliwa kama wamiliki wa maeneo hayo na si wavamizi na kutaka kulipwa fidia kwa mujibu wa sheria.
Diwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe akitoa maelezo wakati wa kikao cha kutatua mgogoro kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya kusini Njombe na wananchi wa Kijiji cha Magoda na Mtaa wa Lunyanywi mkoani Njombe kilichoongozwa na Waziri wa Ardhi, Dkt.Angeline Mabula Agosti 9, 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).

Utatuzi wa mgogoro baina ya Kanisa la KKKT na wananchi wa Kijiji cha Magoda na Mtaa wa Lunyanywi mkoani Njombe umekuwa ukiendelea kufanyika katika ngazi mbalimbali chini ya usimamizi wa Mkuu wa Mkoa wa Njombe na kufikia maamuzi kuwa, KKKT itoe viwanja vya kifuta jasho kwa walalamikaji ili kumaliza mgogoro pamoja na kumega eneo la chuo lililojengwa nyumba na walalamikaji ili waendelezaji wabaki na maeneo waliyojenga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news