Michezo inatumika kutatua migogoro

NA ADELADIUS MAKWEGA

WANACHUO wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kilichopo jijini Mwanza wanaohitimu mwaka 2023 katika kozi za Stashahada ya Elimu ya Uongozi na Utawala katika Michezo (Ordinary Diploma in Sports Development & Administration), 
Stashahada ya Ufundishaji Michezo (Ordinary Dipoloma in Sports Coaching Education), Stshahada ya Elimu ya Michezo(Ordinary Diploma in Physical Education & Sports na Kozi ya Astashahada ya Elimu ya Michezo kwa Wanamichezo (Basic Technician in Certificate in Physical Education and Sports), wamefanya tukio la historia katika ulimwengu wa michezo nchini Tanzania.

Ni kwa kutengeneza uwanja wa mchezo wa mpira wa miguu ambapo utawanufaisha wakazi wa mikoa ya miwili Mwanza na Simiyu uliopo katika eneo la Mwanegere ambapo ni mpakani mwa Wilaya ya Kwimba na Maswa.

“Sote kwa pamoja, wanachuo wa mwaka pili 2022/2023 tuliunda kamati maalumu na kukusanya fedha kutoka katika fedha zetu tulizojibana hapa chuoni.

"Wengine wakila mlo mmoja, kubwa kuukamilisha utayarishaji wa kiwanja hicho, tukipata ushirikiano na watumishi wa chuo chetu tangu mwanzo hadi leo hii tunakukabidhi.”

Haya yamesemwa na Nyantito Petro ambaye anahitimu mafunzo yake ya michezo, huku akifundisha Shule ya Msingi Fort-Ikoma ndani ya Halmashauri ya Serengeti mkoani Mara, wakati akisoma risala yao ya kukabidhi uwanja huo mbele ya viongozi wa kata nufaika na Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, ndugu Richard Mganga.
Risala hiyo ilibainisha kuwa, fedha taslimu shilingi milioni 6 zilitumika kulifanyia usafi eneo hilo, kuondoa visiki, kuweka alama za kiwanja , kuweka magoli na kazi zingine ikiwamo gharama za wanachuo za chakula wakati za zoezi hilo hadi kinakamilika huku ufunguzi wake ukifanyika kwa mechi mbili kuchezwa na wanachuo hao.

Mashindano hayo ya ufunguzi yamefanyika tangu alfajiri ya Agosti Mosi, 2023 ambayo yalitanguliwa na mbio za mchaka mchaka, mashindano kadhaa ya michezo mingine, huku siku hiyo ikiwa na hekaheka tele.

Majira ya saa 10 ya jioni wanachuo hao walijumuika katika Uwanja wa Ndani vya Chuo hicho na kulifanyika kikao maalumu cha kumaliza kipindi cha masomo cha mwaka wa masomo 2022/2023.

Ndani ya kikao hicho mambo mbalimbali yalizungunzwa na wakufunzi na wanachuo hao wakiwa na furaha ya kumaliza mwaka wa masomo na wengine wakimaliza kozi zao baada ya kusoma hapo chuoni kati ya mwaka mmoja na miwili.

”Chuo chetu cha Maendeleo ya Michezo Malya mwaka huu kiliingia katika mtindo wa Bima ya Afya kwa wanachuo wake ili waweze kushiriki michezo vizuri, hivi tunavyokwenda kumaliza mwaka huu wa masomo, bima za walio wengi kwa mwaka wa masomo 2022/ 2023 zinakwenda kumaliza muda wake wa kutumika.

"Maana yake haziwezi tena kutumika kutibiwa, ninawaomba wanachuo wote, mnavyorudi nyumbani hakikisheni mnalipia bima hizo mapema kuepusha usumbufu. 

"Msimu tunaokuja nayo wa masomo kuanzia Oktoba kwa hapa Mwanza ni msimu wa mvua, hakikisheni mnakuwa na nguo za michezo za kutosha kama mlivyoagizwa, maana msimu wa mvua ni msimu ambao msipokuwa makini mnaweza kupatwa na magonjwa kwa kuvaa nguo mbichi kama ukiwa na nguo chache, epukeni kauka nikuvae.”

Hayo yalisemwa na Mwadili wa Wanachuo na Mkuu wa Dawati la Jinsia chuoni hapo, Epifania Bugaga ambaye pia ni mkufunzi wa kozi kadhaa za michezo.

Kikao hicho kilitoa nafasi kwa Mkufunzi wa Taaluma, ndugu Joachim Maganga na yeye alisisitiza mno wanachuo hao kufuata taratibu zote za taaluma na kusoma kwa bidii, kwani hawawezi kupata cheti kwa njia yoyote ile ya mkato.

“Jamani mimi ninawashukuru sana, ninachoweza kusema kwenu nyote muhakiishe mnatumia talanta zenu, ukiificha talanta zako tambua na wewe utakuwa umefichwa. 

"Katika muda mliyokuwepo hapa chuoni niliwasitiza kuwa na mitando na watu mbalimbali, usipokuwa na mtandao katika maisha hilo nalo ni kosa, ndani ya mtandao wako hapo unaweza kupata fursa mbalimbali.”

Kwa upande wake Alex Mkenyengea ambaye ni Makamu Mkuu wa chuo hiki alitumia nafasi hiyo kuwaomba wanachuo wanaohitimu na wanaobaki kujitahidi sana kuwa mawakala wazuri wa chuo hicho popote walipo.

Ndugu Alex Mkenyenge ambaye anafundisha pia kozi kadhaa za michezo alimkaribisha Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, ndugu Richard Mganga.

Ndugu Mganga katika kikao hicho alianza kwa kupiga kipenga cha hotuba yake ya kumaliza mwaka wa masomo 2022/ 2023 kwa wanachuo wake kwa kusema kuwa,

“Tanzania ina shule za msingi 19,000 na shule za sekondari karibu 5000 na kidogo , jumla tuna shule karibu 24,000, wanachuo waliohitimu Chuo cha Malya ni 808, hapo kuna mahitaji makubwa ya wataalamu wa michezo.
"Kwa maana hiyo fursa zipo tele, bado katika wizara na taasisi zingine za michezo. Jamani fursa bado zipo, lakini kikubwa lazima mwanachuo unapokuwa mafunzoni usome kwa bidii na tuone unapokuwa hapa unafanya nini?.

"Kwa wanaohitimu tunatambua mtafanya vizuri na jina la Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya litakuwa bora zaidi na jamii ya Tanzania itanufaika zaidi na zaidi, nyinyi mtakuwa matunda bora, mmepata elimu sahihi mkaitumie vizuri.”

Akiendelea kuongea katika hotuba yake Mkuu wa Chuo Mganga alisema bayana kuwa anawapongeza sana wanachuo wake kwa kufanikisha shughuli zote walizofanya katika kipindi hiki cha masomo, huku akisema kuwa maendelea ya chuo chao ni maendeleo ya wale wote waliosoma chuoni hapo na maendeloe ya kila Mtanzania mpenda michezo.

“Hatua moja inakupeleka kwenye hatua nyingine, kwa nyie mnaohitimu mmefanya kazi kubwa sana, nawapongeza tena na tena kwa ubunifu wenu.
"Mmekuwa wabunifu sana, kwa kupitia wakufunzi wenu, mmetutengenezea uwanja ule,uwanja wa soka,hiyo ni alama ya kwenu, ni alama ambayo imeachwa chuoni kwetu. 

"Lile ni eneo la Wilaya ya Maswa na huku tupo Kwimba,panawezekana eneo lile lilikuwa na migogoro ya hapo awali, baina ya Kwimba na Maswa, sasa mmetengeneza ule uwanja, tambueni kuwa michezo inatumika kama kitu cha kinachosaidia kutatua migogoro.

"Pale mmetengeneza pahala ambapo kutaleta suluhisho baina ya hayo maeneo mawili. Nawashukuru sana na nawatakia maisha mema kwenu nyote.”

Hapo Mkuu wa chuo hiki cha michezo alipiga kipenga cha kumaliza mchezo.Akizungumza kandoni ya shughuli hiyo, Makamu Rais wa Serikali ya Wanachuo, Ndinagwe Sungura alisema kuwa, anawashukuru wakufunzi wote na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwapatia huduma zote muhimu wakiwa chuoni na kutembelea chuo hiki kila mara kwa Katibu Mkuu ndugu Saidi Yakubu na Waziri Balozi, Dkt.Pindi Chana.
Huku akiongeza kuwa,“Kaka na dada zangu waliohitimu nawatakia maisha mema katika kuendeleza michezo ya taifa letu. Ninawaomba wao watangulie wakatutengenezee njia, kwa kuwa mfano bora katika Ulimwengu wa Michezo.”

Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kwa sasa bado kinapokea maombi ya wanachuo wanataka kujiunga na kozi nne za michezo ambazo ni Stashahada ya Elimu ya Uongozi na Utawala katika Michezo (Ordinary Diploma in Sports Development & Adrminstration), 
Stashahada ya Ufundishaji Michezo (Ordinary Dipoloma in Sports Coaching Education), Stshahada ya Elimu ya Michezo(Ordinary Diploma in Physical Education & Sports na Kozi ya Astashahada ya Elimu ya Michezo kwa Wanamichezo (Basic Techinician in Certificate in Physical Education and Sports),

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news