ADF wauawa Bonde la Mwalika

KAMPALA-Operesheni Shujaa ambayo inajumuisha Jeshi la Wananchi nchini Uganda (UPDF) na Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) siku ya Alhamisi wamemuua mmoja wa makamanda wa kundi la waasi linaloshirikiana na Islamic State (IS) la Allied Democratic Forces (ADF).
Baadhi ya wanajeshi wa UPDF. (Picha na Mtandao).

Serikali ya Jamhuri ya Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimekuwa zikiwafuatilia wanamgambo hao pamoja kwa karibu miaka miwili.

Miongoni mwa waliouawa ni Kamanda Fazul ambaye anatajwa kuhusika na kundi hilo lenye mafungamano na wanamgambo wa IS nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo alikuwa akiendesha operesheni zake katika Bonde la Mwalika.

Vyombo mbalimbali vya habari nchini DRC na Uganda vimemnukuu Afisa Mawasiliano kwa Umma wa Mountain Division/Operetion Shujaa, Meja Bilal Katamba akisema kuwa, Fazul aliuawa na wenzake wa ADF katika maeneo ya Alungupa huko Mkoa wa Kivu Kaskazini.

"Kuhusiana na hilo, Jumatano, Agosti 24,2023, vikosi vya pamoja chini ya Kikosi cha 3 cha Milima cha UPDF katika eneo la jumla la Kanana, Makisabo, Mkoa wa Kivu Kaskazini, viliwaua wapiganaji wawili wa ADF na kupata SMGs mbili, magazini nne, vifaa 84 vya mawasiliano na redio ya kijeshi," alisema Kalamba huku akisisitiza kuwa,vikosi vya pamoja vinaendelea kuwasaka magaidi hao kutoka kila pembe ya misitu.

"Vikosi vya pamoja, hata hivyo, vinawaomba wapiganaji wa ADF kujisalimisha na kufaidika na msamaha wa Serikali ya Uganda ambao bado unatumika kwa wale wanaoamua kujitoa katika uasi," aliongeza.

Operesheni Shujaa ambayo inatajwa kuleta matokeo makubwa licha ya changamoto za hapa na pale tangu ilipozinduliwa Novemba 2021, inalilenga kundi la ADF ambalo limekuwa likihusishwa na vitendo mbalimbali vya kikatili, ugaidi, mashambulizi na utekaji huko Uganda na DRC.

Waasi wa ADF wamekuwa wakiendesha shughuli zao kwenye misitu Mashariki mwa Kongo kwa miaka kadhaa na wamekuwa wakifanya mashambulizi ndani ya nchi hiyo na wakati mwingine nchini Uganda.Kundi hilo halikutoa taarifa yoyote ya haraka kuhusu kifo cha kamanda huyo.

ADF ni nini?

ADF, ambalo awali lilikuwa kundi la waasi lenye makao yake nchini Uganda, lilianzisha mashambulizi yake katika miaka ya 1990 Magharibi mwa nchi hiyo, lakini hivi karibuni lilitimuliwa na Jeshi la Uganda ambalo liliwapeleka wapiganaji wake mpakani hadi Congo DRC ambako wamekuwa wakiishi huko.

Aidha, mara nyingi wamekuwa wakianzisha mashambulizi ndani ya Kongo na wakati mwingine katika mpaka wa Uganda.(LM/Agencies)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news