Musoma Vijijini waamua kujenga David Massamba Memorial Secondary School kumuenzi

NA FRESHA KINASA

MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara, Prof. Sospeter Muhongo na wananchi wa jimbo hilo kwa pamoja, wameamua kumuenzi marehemu Prof.David Massamba kwa kujenga Sekondari Mpya kijijini kwao.
Ni shule itakayopewa jina lake na kuitwa David Massamba Memorial Secondary School.

Hayo yamebainishwa Agosti 30, 2023 kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof.Sospeter Muhongo na kusema kuwa, ujenzi wa sekondari hiyo utaanza mwezi Septemba 2023.

"Agosti 30, 2023 ilikuwa siku ya maziko ya Gwiji la Lugha ya Kiswahili, Prof. David Massamba nyumbani kwake kijijini Kurwaki, Musoma Vijijini.

"Wataalamu wenzake wa lugha ya Kiswahili, wakiwemo wanafunzi wake wanasema marehemu alikuwa gwiji na mbobezi kwenye eneo la Fonolojia ya Kibanu, hayupo mwingine tena wa kariba yake," imeeleza taarifa hiyo.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijni, Prof. Sospeter Muhongo amewashukuru wananchi hao kwa uamuzi huo ambao utaenzi mema yote aliyoyafanya Prof. Massamba.

"Tusitegemee kwanza fedha za Serikali, sisi tuanze tukijua Serikali inaweza kutupatia au isitupatie. Hili jambo ni jipya si rahisi kusikia wananchi mnajitolea kumbe mnaheshimu sana Prof. Massamba.

"Kwa kazi alizozifanya, vitabu alivyoviandika nawapongeza sana kwa kuazimia na kupitisha jina la David Massamba Memorial Secondary School.
"Wanafamilia na nyie muwe mnakuja kuja mkisikia shule imeanza lazima mpite pite hata kama huna hela wakuone tu huyu ni familia ya Massamba.

"Furaha yangu kubwa tumekubaliana kujenga sekondari kwa heshima ya ndugu yetu kwa kazi zote hizo alizozifanya hatuwezi kumzika anapotea hivi hivi,"amesema Prof.Muhongo.

Zainabu Shadrack ambaye ni mkazi wa Kurwaki amepongeza hatua hiyo na kusema kuwa, itawafanya wanafunzi wanaosoma jimboni humo kuwa na bidii na msukumo chanya wa kufika mbali zaidi katika masomo yao kusudi waje kutoa mchango wao wa kimaendeleo katika jamii na taifa kwa ujumla.
Mmoja kati ya wanafunzi waliofundishwa na Prof. David Massamba amesema kuwa, Prof. huyo ameandika kitabu kiitwacho Historia ya Kiswahili amesema yeye atahakikisha anakihubiri Kiswahili na kukitangaza sambamba na kuwashauri watu wakitumie.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news