Ni Kombe la Shirikisho, Ligi ya Mabingwa barani Afrika

NA DIRAMAKINI

INGAWA wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Afrika, baadhi wameonekana kushindwa kuhimili kasi ya safari, bado Watanzania wana matumaini ya kusonga mbele.

Agosti 25,2023 Azam FC walitupwa nje ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika kwa mikwaju ya penalti 4-3.

Ni baada ya sare ya jumla ya 3-3 na Bahir Dar ya Ethiopia ndani ya Uwanja wa Azam Complex uliopo Kata ya Chamazi katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke,Dar es Salaam.

Watanzania walishuhudia mtanange mzuri ambao dakika 90 zilimalizika kwa Azam FC kushinda 2-1 na kufanya sare ya jumla ya 3-3 baada ya Bahir Dar kushinda 2-1 kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa Abebe Bikila jijini Addis Ababa.

Aidha, mabao ya Azam FC yalifungwa na Iddi Suleiman (Nado) dakika ya kwanza na Prince Dube dakika ya 10, wakati la Bahir Dar lilifungwa na Habtamu Tadesse dakika ya 17.

Pia, katika mikwaju ya penalti kipa wa Azam FC, Idrissou Abdulai aliokoa penalti mbili za Bahir Dar huku Azam FC waliofunga ni Yanick Bangala, Feisal Salum na Cheikh Sidibe.

Vile vile,Sospeter Bajana, Idris Mbombo na Djibril Sylla wote walikosa na kwa matokeo hayo, Bahir Dar itamenyana na Club Africain ya Tunisia.

Yanga SC vs AS Ali Sabieh (ASAS)

Wakati Azam FC wakiondoka wakiinamisha vichwa chini, kwa upande wa Mabingwa wa Tanzania,Yanga SC wamefanikiwa kwenda Raundi ya mwisho ya mchujo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.

Safari ya Yanga SC iliiva Agosti 26,2023 baada ya ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya AS Ali Sabieh (ASAS) ya Djibouti katika Uwanja wa Azam Complex uliopo Kata ya Chamazi ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Max Mpia Nzengeli dakika ya saba na 90, Hafiz Konkoni dakika ya 45, kiungo Coast Pacome Zouazoua na mshambuliaji Clement Mzize dakika ya 69 ndiyo waliimaliza ASAS ya Djibouti.

Aidha,huku Yanga SC ikivuna ushindi wa namna ya kipekee, ASAS ya Djibouti walifanikiwa kujifariji kupitia bao la Tito Mayor kwa penalti dakika ya 85.

Kwa matokeo hayo, Yanga SC inafuzu kwa ushindi wa jumla wa 7-1 baada ya kuichapa AS Ali Sabieh 2-0 kwenye mchezo wa kwanza hapo hapo Azam Complex na sasa itakutana na Al-Merreikh ya Sudan mechi ya kwanza wakianzia ugenini Septemba 15,mwaka huu na marudiano ni jijini Dar es Salaam tarehe 29 Septemba, mwaka huu.

Singida Fountain Gate vs JKU

Nayo Singida Fountain Gate imefanikiwa kwenda hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Mafanikio hayo wameyapata Agosti 27,2023 licha ya kufungwa mabao 2-0 na JKU ya Zanzibar ndani ya Uwanja wa Azam Complex uliopo Kata ya Chamazi katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke,Dar es Salaam.

Nassor Juma dakika ya saba na Gamba Matiko dakika ya 42 ndiyo waliifungia JKU ambapo kwa matokeo hayo Singida Big Stars inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3.Ni kufuatia kushinda 4-1 kwenye mchezo wa kwanza na sasa watamenyana na Future ya Misri.

KMKM vs St.George

Aidha, michuano hii inaonesha haijawaendea vema Watanzania kutoka visiwani kwani, baada ya JKU kukwama kusonga mbele, vile vile KMKM ya Zanzibar nayo imetupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.

Ni baada ya kuchapwa mabao 3-1 na wenyeji, St.George katika mchezo wa marudiano Raundi ya Awali usiku wa Agosti 28, 2023 katika Uwanja wa Abebe Bikila jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Dawit Tefera Alemu dakika ya 49, Natnael Zeleke Tadesse dakika ya 65 na mshambuliaji Abel Yalew Tilahun dakika ya 79 ndiyo waligeuza tabasamu la KMKM kuwa huzuni.

Ni licha ya KMKM kutangulia na bao la mshambuliaji wake, Salum Akida Shukuru dakika ya 24 katika mtanange huo mkali.

St.George kwa matokeo hayo wanasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-2 kufuatia kushinda 2-1 kwenye mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam na sasa watamenyana na mabingwa watetezi, Al Ahly ya Misri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news