TFRA yatakiwa kutathmini manufaa ya mbolea ya ruzuku

MBEYA-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kufanya tathmini ya manufaa ya ruzuku ya mbolea iliyotolewa kwa wakulima kwa mwaka 2022/2023. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan (katikati) akisikiliza maelezo ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA- hayupo pichani) alipotembelea banda la mamlaka  leo siku ya kilele cha maonesho ya sikukuu ya wakulima (Nanenane) jijini Mbeya.

Ameitaka kuhusianisha kiasi cha mbolea kilichofikishwa kwa wakulima na hali ya uzalishaji ili kujiridhisha endapo mbolea imetumika katika mashamba ya wakulima na hivyo kuongeza tija kwenye uzalishaji au vinginevyo.

Rais Dkt. Samia ametoa wito huo leo alipotembelea banda la mamlaka ikiwa ni siku ya kilele cha sikukuu ya wakulima maarufu kama Nanenane yaliyofanyika Kitaifa katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Amesema, mbolea ikisambazwa kwa wakulima na isioneshe matokeo yenye tija italeta maswali mengi, lakini kukiwa na takwimu zinazoonesha kiasi cha mbolea kilichowafikia wakulima na kiasi cha mazao yaliyopatikana baada ya kutumia mbolea itaonesha dhahiri kuwa kazi inayofanywa ni nzuri.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Anthony Diallo (katikati), Mkurugenzi wa Mamlaka, Dkt. Stephan Ngailo (kushoto) na mwenyekiti wa ruzuku ya mbolea taifa, Louis kasera wakiwa katika picha katika banda la Mamlaka walipotembelewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa kilele cha maadhimosho ya sikukuu ya wakulima ( nanenane) katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya tarehe 8/8/2023.

"Atleast nione ongezeko kwenye uzalishaji,"Dkt. Samia alisisitiza. Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa mbolea za ruzuku kwa msimu wa kilimo 2022/2023 na kuendelea kwa msimu huu wa 2023/2024.

Ameeleza kuwa, tathimini ya awali iliyofanyika imeonesha ongezeko la uzalishaji kutoka junia moja bila kutumia mbolea mpaka junia tisa baada ya kutumia mbolea kwa ekari moja.

Waziri Bashe amesema, kiasi cha shilingi bilioni 200 kimetegwa kugharamia ruzuku ya mbolea kwa msimu wa kilimo 2023/2024 huku matumizi kwa msimu huu wa kilimo yakikadiriwa kuwa tani laki sita na nusu (650,000)
Watumishi wa TFRA wakiwa katika picha ya pamoja siku ya kilele cha maadhimisho ya sikukuu ya wakulima yaani nanenane katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Dkt. Stephan Ngailo ameeleza kuwa, matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka tani laki tatu na sitini na tatu (363,000) kwa msimu wa kilimo wa 2021/2022 na kufikia tani laki tano na elfu themanini (tani 580,000) msimu wa kilimo 2022/2023 huku tani laki tatu na themanini (380,000) zikinunuliwa kwa mfumo wa ruzuku na kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 368.

Aidha, Dkt. Ngailo ameahidi kufanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news