Wakulima, wafugaji Bugwema waishukuru Serikali

NA FRESHA KINASA

WAKULIMA na wafugaji katika Kata ya Bugwema Halmashauri ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara, wametoa shukurani zao za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Sita kufuatia hatua yake ya kuridhia ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji katika Bonde la Bugwema.

Hatua hiyo, wamesema itasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula kutokana na kuwa na uhakika wa mavuno badala ya kutegemea kilimo cha mvua ambacho kimekuwa na changamoto nyingi ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi.

Nyafuru Thomas amesema kuwa, ni faraja kubwa na neema kwa wakazi wa Bugwema na Musoma kwa ujumla kuona mapinduzi chanya yanafanyika kwa kuzalisha kwa tija kupitia kilimo cha umwagiliaji ambacho kitaleta tija kwa wananchi.

Fabian Jonathan amesema kuwa,wananchi wanashauku kubwa ya kuingia katika uzalishaji wa mazao ya chakula kwa njia ya kisasa kutokana na miundombinu ambayo itajengwa kuwasaidia wakulima wakubwa na wadogo.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof.Sospeter Muhongo amesema kuwa,"hakuna mwananchi atakayehamishwa na pia wananchi muwaruhusu wataalamu waje wafanye tathimini na Serikali itusaidie kupata miundombinu.

"Na miundombinu ni ya wakulima wote wakubwa na wadogo, kwa hiyo hakuna atakayehamishwa muwe na mshikamano."amesema Prof Muhongo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini siku ya Agosti 20, 2023 imeeleza kuwa, "Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan alipokea na kukubali ombi la kufufua kilimo cha umwagiliaji kwenye Bonde la Bugwema la Musoma Vijijini,"imesema na kuongeza kuwa.

"Ombi hilo la Wana-Musoma Vijijini liliwasilishwa kwa Mhe Rais na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof.Sospeter Muhongo.

"Hii ilikuwa Februari 6, 2022 siku ambayo Mhe Rais aliweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Bomba la Maji la Mugango-Kiabakari-Butiama (lenye thamani ya shilingi bilioni 70.5).

"Serikali iliyoongozwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ilianza kujenga miundombinu ya umwagiliaji kwenye Bonde hilo Mwaka 1974. Mradi ukasimama, na sasa unafufuliwa!"

UKUBWA WA BONDE LA BUGWEMA.

"Bonde hili ni kubwa mno ambapo vijiji vyote vitatu kwa Kata ya Bugwema vimo ndani yake. Vijiji hivyo ni Bugwema, Masinono na Muhoji. Hili eneo pekee lina ukubwa wa zaidi ya Hekta 6,000 (elfu sita).

"Baadhi ya maeneo ya Kata jirani za Bugoji, Nyambono na Murangi ni sehemu ya Bonde hili kwa upana na urefu wake, ambapo kwa ujumla wake Bonde linakadiriwa kuwa na ukubwa wa zaidi ya Hekta 10,000 (elfu kumi)."

MAZAO YANAYOLIMWA NDANI YA BONDE LA BUGWEMA

"Mpunga, mahindi, alizeti, dengu na pamba ndiyo mazao makuu yanayolimwa ndani ya bonde hili."

BAJETI 2023/2024-TUME YA TAIFA YA UMWAGILIAJI

"Tume hii imetoa kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu (feasibility study & design) wa Bonde la Bugwema kwa Kampuni ya Ms MHANDISI CONSULTANCY LTD. Kazi zinaanza mwezi huu (Agosti 2023)."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news