Watumishi saba mbaroni kwa kuhujumu uchumi

KATAVI-Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Katavi imewafikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi watumishi saba kwa tuhuma za wizi wa fedha kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 1. 23.

Kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 5 ya mwaka 2023, imetajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Gway Sumaye na mwendesha mashtaka Gregory Mhangwa.

Amesema, watuhumiwa hao wanashitakiwa kwa makosa matatu ya kujihusisha na genge la uhalifu, uhujumu uchumi na wizi.

Mhangwa ameeleza kuwa, washitakiwa hao walishirikiana kutenda makosa hayo kati ya Novemba 1, 2022 hadi Agosti 11, 2023 huko katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe.

Ni kwa kudanganya kuwa, walikuwa wakiwalipa wakandarasi waliofanya kazi katika halmashauri hiyo kiasi cha shilingi 1,232,408,689 na kuisababishia hasara halmashauri.

Canuthe Matsindiko (41), ambaye ni Ofisa TEHAMA kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Michael Katanga (31), Mhasibu wa Halmashauri ya Mpimbwe, Tamaini Misese (47), aliyekuwa Ofisa TEHAMA Mkoa wa Katavi na Maira Samson Olumba (38), Ofisa Manunuzi wa Halmashauri ya Mpimbwe.

Emmanuel Damas Saranga (37) Mhasibu katika Halmashauri ya Mpimbwe, Masami Andrew Mashauri (49) Mhasibu katika Halmashauri ya Mpimbwe na Laurent William Sunga (33) Mhasibu katika Halmashauri ya Mpimbwe ndiyo wanaotuhumiwa kuhusika na uhalifu huo.

Hata hivyo, washitakiwa wote hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na washitakiwa wote wamerudishwa rumande hadi Septemba 4, 2023 kesi hiyo itakapotajwa tena katika Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news