10,273 walipwa trilioni 1.03/- zilizorithiwa na PSSSF

NA GODFREY NNKO

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umelipa madai ya kiasi cha shilingi 1.03 trilioni yaliyorithiwa kutoka kwenye mifuko iliyounganishwa kwa wanufaika 10,273.

PSSSF ilianzishwa mwaka 2018 kupitia Sheria ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi, Sura 371, ambapo ni matokeo ya ya kuunganishwa kwa Mfuko wa Taifa wa Mafao ya Watumishi wa Serikali (GEPF),Mfuko wa Pensheni wa LAPF,Mfuko wa Pensheni wa PPF,Mfuko wa Pensheni wa PSPF  ili kuleta uendelevu wa mifuko.

Sambamba na kuondoa ushindani uliokuwa hauna tija kwa mifuko kushindania wanachama wachache waliokuwa wanaingia katika soko la ajira ikilinganishwa na idadi ya mifuko iliyokuwepo nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF,CPA Hosea Kashimba ameyabainisha hayo Agosti 31, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kazi na wahaariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

CPA Kashimba amesema,madai hayo yalilipwa ndani ya miaka miwili huku mfuko ukiendelea kulipa madai mapya kwa watumishi wa umma.

"Katika kutekeleza majukumu yake, mfuko kwa kipindi cha miaka mitano, umetatua changamoto nyingi na kupata mafaniko yafuatayo, kulipa madai ya kiasi cha shilingi 1.03 trilioni yaliyorithiwa kutoka kwenye mifuko iliyounganishwa kwa wanufaika 10,273.

"Madai haya yalilipwa ndani ya miaka miwili huku mfuko ukiendelea kulipa madai mapya. Pia, kulipa kiasi cha jumla ya shilingi 8.88 trilioni kwa wanufaika 262,095."

Ameendelea kufafanua kuwa, pia mfuko huo umefanikiwa kuongeza thamani ya uwekezaji kwa asilimia 23.5, kutoka trilioni 6.40 hadi trilioni 7.92 ikiwa ni wastani wa ongezeko la asimilia nne kila mwaka

"Mafanikio mengine ni kupata mapato yatokanayo na uwekezaji ya wastani wa asilimia 85 kwa mwaka, kulinda na kuongeza thamani ya mfuko kwa asilimia 27.76 kutoka shilingi trilioni 5.83 hadi shilingi trilioni 8.07, wastani wa ongezeko la asilimia 6.72 kwa mwaka."

CPA Kashimba amesema kuwa, pia mfuko huo umeweza kupunguza gharama za uendeshaji kutoka wastani wa asilimia 12 hadi tano ya michango inayokusanywa kwa mwaka ikiwa ni chini ya ukomo wa asilimia 10 kwa mujibu wa taratibu na kanuni.

Mafanikio mengine amesema, mfuko umeweza kulipa bila kukosa na kwa wakati, pensheni ya kila mwezi wastani wa shilingi billioni 67 kwa wastaafu kila ifikapo tarehe 25 ya mwezi husika.

"Hili ni ongezeko la asilimia 100 ukilinganisha na kiasi cha wastani wa shilingi bilioni 34 wakati wa kuunganishwa. Mafanikio mengine ni kupunguza muda wa kusubiri mafao, kwani mfuko unalipa ndani ya siku 60, kwa mujibu wa sheria; kabla ya mfuko wastaafu wengine walitumia zaidi ya miaka mitatu kusubiri mafao."

Pia, wamefanikiwa kuboresha huduma za wateja kwa kutumia mifumo ya Teknolojia na Mawasiliano (TEHAMA) iliyovumbuliwa, kutengenezwa na kuendeshwa na wataalamu wa ndani kwa asilimia 90.

Wakati huo huo,Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, mfuko huo umepiga hatua kubwa katika kuwaunganisha wafanyakazi wote waliotoka kwenye mifuko minne ilyokuwa na taratibu tofauti na sasa wana lengo moja la kazi za mfuko mpya.

"Mfuko umepata hati safi za Hesabu za Mfuko toka uanzishwe na pia kupata tuzo za uandaaji na uwasilishaji bora wa Mahesabu kutoka NBAA kwa miaka miwili mfululizo 2020/21 na 2021/22.

"Na mwaka 2020/21 mfuko ulishika namba moja kwa taasisi za Serikali kwa kupata matokeo ya 94 ya ukaguzi ya kuzingatiaji wa miongozo ya manunuzi ya umma. Vile vile, tumefanikiwa kuandikisha wanachama wapya 140,162 kwa wakati.

"Hawa ni waajiriwa wa Serikali na taasisi zake ikiwemo kuandaa na kusimamia utekelezaji wa mifumo na miongozo ya ndani ya usimamizi wa rasilimali watu kwa kuzingatia utawala bora."

Mbali na hayo amesema,mfuko huo ulipata alama 95 katika ukaguzi wa uzingatiaji wa miongozo ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2021/22.

"Mfuko umepokea tuzo mbalimbali kutoka Shirikisho la Kimataifa la Hifadhi ya Jamii maarufu kama ISSA, lakini pia tuzo mbalimbali kutoka taasisi nyingine hapa nchini."

Katika hatua nyingine, CPA Kashimba amesema kuwa, mfuko huo umeendelea na shughuli za uwekezaji katika miradi ya ubia ili kujiongeza mapato.

Pia, amesema uwekezaji huo utaongeza fursa ya kuongeza ukwasi katika taasisi za fedha na kuwezesha wananchi kupata mikopo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo na kiuchumi, kuongeza ajira, kodi serikalini na kukuza mitaji

Miongoni mwa miradi ya ubia na wawekezaji wengine kwenye sekta ya viwanda ni pamoja na Kiwanda cha Kimataifa cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro kilichopo Moshi mkoani Kilimanjaro.

Katika kiwanda hicho wana umiliki wa hisa asilimia 86 na Jeshi la Magereza asilimia 14 ambapo awamu ya kwanza ya kiwanda hicho ilizinduliwa Oktoba, 2020.

Aidha, kuna Machinjio ya Kisasa ya Nguru Hills ambapo wana hisa asilimia 39, Eclipse Investment LLC asilimia 46 na Busara Investment LLP asilimia 15.

Kiwanda cha kuchakata Tangawizi cha Mamba Myamba amesema, PSSSF ina hisa asilimia 65 na Ginger Growers Rural Cooperative Society (MGGRCS) asilimia 35 na Kiwanda cha Chai cha Mponde wana hisa asilimia 42 huku WCF wakiwa na asilimia 42 na Ofisi ya Msajili wa Hazina asilimia 16.

CPA Kashimba amesema, mafanikio ambayo mfuko umeyapata kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na nia ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.

"Kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini wa Mfuko, namshukuru Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uthubutu wake wa kuamua kulipa deni la michango la shilingi trilioni 4.6 la wanachama wa uliyokuwa Mfuko wa PSPF ya kabla ya mwaka 1999.

"Uamuzi huu umewezesha mfuko kulipwa kiasi cha shilingi trilioni 2.17 kupitia hatifungani maalum.Serikalil pia imelipa shilingi bilioni 500 katika deni la shilingi bilioni 731.4 la mikopo ya miradi ambayo mifuko iliyounganishwa iliikopesha Serikali.

"Ni ili kutekeleza miradi ikiwemo ujenzi wa Jengo la Bunge, Chuo cha Serikali cha Hombolo, Nelson Mandela Istitute of Science and Technology na Chuo Kikuu cha Dodoma. Huu wote ukiwa ni sehemu uwekezaji wa mfuko.

"Jambo la kulipa madeni ya Serikali katika mfuko, hususani lile la michango ya kabla ya mwaka 1999 lilichukua muda mrefu, takribani miaka 20. Hata hivyo, kupitia uongozi madhubuti wa Serikali ya Awamu ya Sita, jambo hili limewezekana,"amefafanua CPA Kashimba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news