Bodi ya Ushauri TBA yatembelea miradi ya Mji wa Serikali Mtumba

DODOMA-Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imetembelea baadhi ya miradi inayotekelezwa na TBA katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Bodi,Arch. Dkt. Ombeni Swai ameipongeza Menejimenti na timu nzima ya TBA inayotekeleza miradi katika Mji huo.

"Katika ziara yetu tumetembelea miradi mitatu ambayo ni ujenzi wa ofisi ya Wizara ya Kilimo, Wizara ya Afya na tumemaliza hapa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi Umma na Utawala Bora, 
 
"Kwa kweli ni kazi nzuri ambayo inafanywa na TBA katika miradi hii, ambayo pia inahusisha vijana ambao ndiyo wataalamu wanaosimamia miradi hii, wameonyesha uzalendo na weledi mkubwa katika kusimamia miradi hii kwa ubora unaoendana na thamani ya fedha,"ameeleza Dkt.Swai.

Aidha, Mwenyekiti Swai, ametaja mradi wa ujenzi wa ofisi ya Rais, Utumishi kuwa ni mradi unaokwenda kukamilika kwa wakati na ni mfano kwa wataalamu wengine kwenda kujifunza kupitia mradi huu ambao TBA ndiyo wajenzi.

"Vijana wengine ambao wanaingia katika kazi hizi za ujenzi wana jambo la kujifunza kutoka kwenu na hii itawapa moyo katika kufanya kazi nzuri na yenye weledi kutoka kwenu,"ameweka wazi Dkt.Swai.

Naye Mkadiriaji Majenzi Neema Kifua kutoka Idara ya Ushauri TBA, amesema katika mradi huo wa Mji wa Serikali TBA, inasimamia ujenzi wa majengo 17, ambapo majengo 13 ni ofisi za wizara na majengo 4 ni ya ofisi za Taasisi za Serikali.

Akiongea wakati wa ziara hio Meneja wa Ujenzi TBA, Manase Shekalaghe amebainisha kwamba ujenzi wa jengo la Ofisi ya Rais, Utumishi upo hatua za mwisho kukamilika.

Ziara ya Bodi ya Ushauri kutembelea Mradi wa Ujenzi wa Mji wa Serikali ni utekelezaji wa moja ya agenda ya Kikao cha kwanza cha Bodi hio kwa mwaka wa fedha 2023/24 kinachofanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia Septemba 08-09, 2023 jijini Dodoma

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news