Mheshimiwa Mpina aeleza ukweli kuhusu manunuzi ya umma nchini


MCHANGO WA MBUNGE WA JIMBO LA KISESA, MHE.LUHAGA JOELSON MPINA (MB) AKICHANGIA KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA UNUNUZI WA UMMA WA MWAKA 2023 BUNGENI DODOMA TAREHE 7 SEPTEMBA 2023.

1. UTANGULIZI

Leo ni siku uhimu, siku ambayo tunaandika upya Sheria yetu ya Manunuzi ya Umma, eneo ambalo zaidi ya asilimia 70 ya bajeti ya nchi yetu hutumika.

Tunaiandika upya sheria hii tukiwa tumeshaumizwa vya kutosha, fedha nyingi za umma zimepotea kutokana na ukiukwaji wa taratibu za manunuzi na uingiaji wa mikataba mibovu.

Hivyo leo ni lazima tuitangazie Dunia kwamba imefika mwisho wa kuchezea na kuiba fedha na raslimali za umma, tunakwenda kutunga Sheria ya Manunuzi ya Umma ambayo itaziba mianya yote ya wizi na ufisadi unaofanyika kupitia manunuzi ya umma.

Sheria ambayo itawezesha kuchukuliwa hatua kali kwa wezi wa fedha za umma ikiwemo kufidia hasara walioisababisha.

Hapa nayakumbuka maneno ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati akitangaza Azimio la Arusha tarehe 5 Februari 1967 alisema nanukuu...

“Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha na tumepuuzwa kiasi cha kutosha, unyonge wetu ndio uliotufanya tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa, sasa tunataka mapinduzi,mapinduzi ya kuondoa unyonge ili tusionewe tena, tusinyonywe tena na tusipuuzwe tena,"mwisho wa kunukuu.

Baada ya nukuu hiyo ya Baba wa Taifa naomba kuwapongeza wafuatao;

(i) Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli (Tingatinga), Rais wa Awamu ya Tano kwa uzalendo wake wa kulinda rasilimali za umma ambapo kulipelekea kutungwa kwa Sheria za Ulinzi wa Raslimali za Nchi Namba 5 na Namba 6 za mwaka 2017.

(ii) Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Awamu ya 6 na Amiri Jeshi Mkuu kwa uzalendo wake wa kutoa uhuru wa wananchi kutoa maoni juu ya Uendeshaji wa Shughuli za Serikali, hili ni jambo zuri la kupongezwa ambapo inaifanya Serikali ione maeneo yenye kasoro na kuyarekebisha, We become more alert when we hear negative words.

(iii) Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Umoja wa Viongozi wa Dini Tanzania kwa namna wanavyofuatilia na kuhakikisha kuwa raslimali za nchi zinalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho.

Baada ya pongezi hizo sasa niingie kwenye uchambuzi wa Ibara za Muswada kama ifuatavyo:-

2. MAMBO YA KIUJUMLA

(i) Baadhi ya maeneo ambayo tumekuwa tukishauri kwa muda mrefu yamezingatiwa na Serikali katika Muswada huu, lakini pia maeneo ambayo hayakuzingatiwa nimeandaa Jedwali la Marekebisho na kuliwasilisha kwako Mheshimiwa
Spika.

(ii) Muswada huu karibia kila Ibara inategemea Kanuni zitakazotungwa na Waziri, Muswada unakosa ukamilifu wake kwa kuacha kuweka mambo muhimu eti yatazingatiwa wakati wa kuandaa Kanuni, lakini pia Waziri amepewa nguvu ya kutunga Kanuni ambazo zinakinzana na Sheria Mama.

Hili jambo halikubaliki na kwa kuwa kila Sheria inapotungwa lazima iandaliwe Kanuni, kwa hivyo maneno ya kwamba ‘itazingatiwa kwenye Kanuni’ yaondolewe kwenye Muswada huu na badala yake maeneo muhimu yote yawekwe kwenye Muswada.

(iii) Muswada umeandikwa kwa lugha ya Kiswahili pekee ni jambo la kupongezwa lakini inaleta changamoto kubwa kutokana na kukosa rejea ya lugha ya Kiingereza kama ilivyozoeleka. Hapa ingeleta ufanisi zaidi kama Muswada ungeletwa kwa lugha zote mbili yaani Kiswahili na Kiingereza.

3. UCHAMBUZI WA MUSWADA

3.1 Ibara ya 30, inayohusu uwasilishaji wa taarifa ya mwaka ya tathmini ya utendaji kazi wa ununuzi wa umma na thamani halisi ya fedha kwa Mheshimiwa Rais na Bunge.

Tunaipongeza Serikali kwa kulileta suala hili ambalo tumekuwa tukiliomba kwa muda mrefu, taarifa ya Ukaguzi ya Manunuzi inayofanywa na PPRA inapokabidhiwa kwa Mheshimiwa Rais iletwe Bungeni ijadiliwe kupitia kamati za kibunge na baadaye kuamliwa kupitia Bunge zima kama inavyofanyika kwa Taarifa ya CAG.

Taarifa ya PPRA ni Muhimu sana katika kuona namna ya Fedha za Umma zilivyotumika katika Taasisi za Serikali eneo la Manunuzi, ukaguzi ambao unatuwezesha kupata thamani ya fedha katika maeneo ya Manunuzi na ugavi. 
 
Taarifa ya PPRA inatuwezesha kuona namna uzingatiaji wa haki,ushindani, uwazi, uendelevu, Uwajibikaji, Matumizi mazuri ya fedha, ufanisi na uadilifu katika ununuzi na ugavi. Lakini pia inatupatia taarifa ya uzingatiaji wa Sheria katika taasisi nunuzi.

Kitendo cha taarifa hii kutokuingia na kuamuliwa Bungeni tunajikosesha na kujinyima wigo mpana wa kusimamia Fedha za Umma. Ili kuliwezesha Bunge kuwa na nguvu ya kuisimamia Serikali katika Matumizi ya Fedha na raslimali za umma.

Ni lazima Taarifa ya PPRA na Taarifa ya CAG ziwasilishwe na kujadiliwa kupitia Kamati za Bunge na baadaye kuamliwa na Bunge zima.

Muswada ulivyoandikwa kwamba Rais aweza, maana yake ni hiari hii tuikatae na kuweka ulazima wa taarifa hii kuwasilishwa Bungeni na kuweka utaratibu wa kujadiliwa na kuamuliwa sambamba na Taarifa ya CAG.

Kufanya marekebisho katika Ibara ya 30 kwa kufuta Ibara ndogo ya (2) na kuandika upya kama ifuatavyo:-
 
“Mara baada ya kupokea taarifa chini ya kifungu kidogo cha (1), Rais atamwelekeza Waziri kuwasilisha taarifa hiyo bungeni katika kikao cha Bunge kitakachofuata baada ya kupokea taarifa hiyo na Bunge litajadili taarifa hiyo baada ya kuiwasilisha kwenye kamati husika.”

3.2 Ibara ya 79, inayoruhusu ununuzi wa vichwa na mabehewa ya treni, ndege na meli zilizotumika.

Kuifuta Ibara yote ya 79 kwa kuwa Serikali haiwezi kununua vitu chakavu tena kwa vyombo vinavyohusu maisha ya watu na vyenye gharama kubwa.

Vyombo vichakavu haviwezi kuhakikiwa uimara na ubora wake ukizingatia matapeli yametapaa kila kona ya dunia. Vyombo vichakavu ni vigumu kupata thamani halisi na havina guarantee ya uimara na ubora.

Ni mfumo gani utakaotumika kufanya uhakiki wa uimara na ubora, nani muuzaji wa ndege, meli, vichwa vya treni na mabehewa chakavu na kwa nini yeye aliacha kuvitumia atuuzie sisi.

Tunafanya maamuzi haya kwa sababu hatuna fedha ya kununua vyombo vipya viwandani au shida ni nini? Ni hatari sana kwa taifa kuingia kununua vyombo vya usafiri wa umma vichakavu na ambavyo havina guarantee ya ubora na uimara na hivyo hakuna uthibitisho kama vyombo hivi havitaharibika, kulipuka moto, kuzama, kuanguka na kusababisha ajali na vifo, nani atalipa damu ya watanzania itakayokwenda kumwagika, nani atakayelipa fedha za watanzania zinazokwenda kupotea?.

Lakini pia itaongeza gharama na usumbufu mkubwa kwa wananchi kushindwa kupata huduma bora iliyotarajiwa.
 
Kama tunalalamika baadhi ya ndege mpya tulizonunua kiwandani kuwa na dosari itakuwaje kwa chakavu, leo tunapata wapi ujasiri wa kununua ndege, vichwa na mabehewa ya treni na meli chakavu kwa manufaa ya nani na tunataka kumfurahisha nani?. Nashauri waheshimiwa wabunge tusikubali mpango huu.

3.3 Ibara ya 57, inayohusu kufanya upendeleo wa kipekee kwa watu au Kampuni za ndani.

Kufanya marekebisho Ibara ya 57 (1) kwa kufuta maneno “Ukomo ulioanishwa katika kanuni” yaliyomo katika Ibara ndogo ya (1) na badala yake kuweka maneno “Shilingi Bilioni Mia Moja”

Hivyo hapa napendekeza zabuni zenye thamani ya kiwango cha chini ya Tsh. Bilioni 100 wapewe upendeleo makampuni ya ndani na ya wazawa ili kuongeza ushiriki wa wazawa katika ujenzi wa taifa, sehemu kubwa ya manunuzi kuchukuliwa na makampuni ya ndani hali itakayoongeza ajira,kupunguza matumizi ya Dola yasiyo na sababu na hivyo kuchochea maendeleo na ukuaji wa uchumi nchini.

Ibara hii ya Muswada inasema ukomo utawekwa kwenye kanuni, hii hapana hili ni jambo kubwa haliwezi kuachwa mikononi mwa Waziri akafanye uamuzi kwa anavyoona yeye inafaa ni lazima tuweke ukomo hapa na ikizangatiwa kuwa Serikali kwa muda mrefu imekuwa ikitoa zabuni zaidi kwa wageni badala ya wazawa.

Tumechezewa sana na hatujasahau miradi ya TEHAMA ya TANESCO inayojengwa na Kampuni ya Tech Mahindra ya India (Bilioni 70), Ukarabati wa Kivuko cha Mv Magogoni (Bilioni 7.5), Mradi wa ETS, Barabara ya Mchepuko Maswa (Bilioni 11), Miradi ya Maji, Miradi ya REA, Boti za Uvuvi,Uzalishaji wa Mbegu nk kazi zote hizi kwa sehemu kubwa zinafanywa na wageni.

Fedha ni za Watanzania zinatumika kulipa makampuni ya nje na kuyaacha makampuni ya ndani, vijana wa kitanzania kukosa ajira huku fedha za nchi yao zikitumika kuajiri vijana wa nchi nyingine hili linauma sana.

Waheshimiwa wabunge tutumieni nafasi hii kwa kuweka upendeleo kwa makampuni ya ndani kwa zabuni zenye thamani ya Tsh. Bilioni 100.

3.4 Ibara ya 68, inayohusu kukubaliwa kwa zabuni na Mikataba kuwa na nguvu ya kisheria,Katika Ibara ya 68 kuongeza ibara ndogo ya (16) baada ya ibara ndogo ya (15) kama ifuatavyo:-

“Kabla ya Kuanza utekelezaji, Mkataba wenye thamani inayozidi Tsh Bilioni hamsini utawasilishwa Bungeni kwa ajili ya uhakiki na Kamati ya Bunge inayoshughulikia Mikataba ya Ununuzi ya Umma.”

Marekebisho haya yataweka ulazima wa Mikataba yote inayozidi Tsh. Bilioni 50 kuwasilishwa Bungeni kwa ajili ya uhakiki kupitia Kamati ya Bunge itakayo shughulikia mikataba ya ununuzi wa umma.

Hii itasaidia kuwepo kwa jicho la Bunge katika hatua za awali za Manunuzi badala ya kusubiri fedha zipotee, itaongeza Umakini na Uwajibikaji kwa baadhi ya maafisa wa Serikali ambao wamekuwa wakiingia Mikataba Mibovu kwa malengo ya kujinufaisha binafsi.

Mheshimiwa Spika, tumechezewa sana, hili suala la Mikataba Mibovu limekuwa likijidhihirisha katika Taarifa ya CAG na hata Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amekuwa akilalamika hadharani kwamba nchi yetu tunaiua wenyewe kwa tamaa zetu kwa kuingia Mikataba Mibovu, kutokulindwa maslahi ya umma, kushindwa kesi Mahakamani na nchi yetu kulipa matrilioni ya fedha.

Hatujasahau malipo ya Symbion (Bilioni 360), IPTL/Escrow (Bilioni 342), Kukamatwa kwa Ndege yetu aina ya Airbus,Miradi yenye Kashfa kubwa ya Rushwa na Ufisadi ya Mradi wa SGR (Trilioni 4),

Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere (Bilioni 926) nk. Hivyo ni lazima kupitia marekebisho haya ya Sheria tuzibe mwanya huu na kuchukua hatua kali kwa wahusika.

Katika Bunge la Mwezi Februari 2023 tuliomba Serikali iweke wazi Mikataba iliyoingia yenye thamani ya Tsh. Trilioni 91 kuishia Februari 2023 lakini hadi leo hakuna utekelezaji ukiacha Mkataba wa Bandari ambao ulikuwa ni takwa la kisheria kuletwa Bungeni.

Waheshimiwa wabunge ni lini tutachukizwa na mambo hayo tuamue leo kuondoa usiri wote unaowekwa katika Mikataba inayohusu fedha na raslimali za umma.

Hivyo kwenye Ibara hii iongezwe Ibara ndogo ya 16 na upande wa Kamati za Bunge ianzishwe Kamati mpya ya Bunge itakayoshughulikia Manunuzi na Mikataba.3.5 Ibara ya 10, inayohusu majukumu ya Mamlaka ya PPRA

3.5.1 Kufanya marekebisho Ibara ya 10 (j) kwa kuongeza baada ya aya (iv) kwa kuanzisha aya ya (v) ambayo inaipa Mamlaka PPRA kama ifuatavyo:-“Ukaguzi wa taasisi zinazosimamia biashara za sekta binafsi katika ununuzi wa bidhaa za mafuta, gesi, mbolea,mazao na mbegu”

Marekebisho haya yataiwezesha PPRA kufanya ukaguzi katika Taasisi za Umma zinazosimamia biashara za sekta binafsi kama, EWURA, PBPA, PURA, TFRA, CPB, ASA nk. ambazo zinazoratibu Manunuzi yanayofanywa ya bidhaa na huduma nyeti (Sensitive Products) kama nishati ya mafuta,gesi, mbolea, ngano, mazao, mbegu, mafuta ya kula nk.

Kwa muda mrefu tumekuwa na matatizo yanayoshamiri kila uchao bila ufumbuzi huku watanzania wakipata usumbufu na matatizo makubwa.

(i) Kupanda bei na uhaba wa nishati ya mafuta, bei za nishati ya mafuta zinaongezeka kila siku na hakuna uthibitisho wa ongezeko hilo.

Hivi sasa kuna ongezeko la bei ya mafuta la takribani Tsh 700 kwa lita kutoka Julai hadi Septemba 2023 miezi miwili tu na mbaya zaidi mafuta yameadimika na hayapatikani kiurahisi sehemu zingine wananchi wakinunua hadi
Tsh. 10,000 kwa lita moja,

Tayari ndani ya mwezi huu wa Septemba 2023 imeripotiwa kutokea kifo cha mwananchi mmoja huko Mkoa wa Mara kwa kupigwa risasi wakati wakigombea nishati ya mafuta huku shughuli za kijamii na kiuchumi zikiathirika kwa kiwango kikubwa na kuchokea mfumko mkubwa wa bei na kupanda kwa gharama za maisha.

Bei za mafuta anazotangaza EWURA kila mwezi zinauhalisia gani na zinahakikiwa na nani? Maana nchi yetu na watanzania wasije wakawa wanawekewa bei feki ili kufanikisha madili ya baadhi ya watumishi wasio waaminifu ndani ya serikali.

(ii) Kuanzishwa kwa mifumo ya usambazaji wa mbolea na bei za mbolea ambazo hazijahakikiwa na kupelekea wakulima zaidi ya Milioni 2 kukosa mbolea.Bei za mbolea anazotangaza TFRA zinauhalisia gani na zinahakikiwa na nani?.

(iii) Wananchi wanauziwa mbegu za mahindi Tsh. 6,500 kwa kilo huku kilo ya mahindi ikiuzwa kwa Sh. 500, hizi bei zinauhalali gani na zinahakikiwa na nani.

PPRA itafanya utafiti na ufuatiliaji wa usahihi wa bei, uimara na ubora kwa wazalishaji wa kitaifa na kimataifa kama ilivyoanishwa katika Ibara ya 10 (p) (q) ya Muswada na ni imani yangu hizi taasisi zikisimamiwa kikamilifu bidhaa hizo nyeti zitapatikana kwa wingi na bei nafuu.

3.5.2 Ibara ya 10 kwa kuongeza aya (q) baada ya aya (p) kama ifuatavyo:-“Kufanya tathmini ya zabuni zilizotolewa kwa kampuni za ndani na kampuni za nje.”

Marekebisho haya yanaipa Mamlaka PPRA kufanya tathmini ya Manunuzi na Ugavi zinazotolewa kwa kampuni za ndani na kampuni za nje, hii itatuwezesha kama nchi kupata taarifa na takwimu za uhakika kuhusu uwiano wa Manunuzi kwa Makampuni ya ndani na Makampuni ya nje ya nchi.

Kwa muda mrefu zabuni nyingi zimekuwa zikitolewa kwa makampuni ya nje hata kwa kazi zinazoweza kufanywa na watanzania. Takwimu hizi zitatuwezesha kama nchi kujitathmini ni kwa kiwango gani tunavyowashirikisha wazawa katika keki ya taifa.

3.6 Ibara ya 94, inayohusu mabadiliko na marekebisho (variations)

Kufanya marekebisho kwa kufuta neno Thelathini iliyopo katika Ibara ndogo ya (1) na badala yake kuweka maneno kumi na tano, pia kuongeza maneno mara baada ya aya (b) katika Ibara ndogo ya (1) aya ifuatayo (c) yamepata kibali
cha Mamlaka.

Marekebisho haya yataiwezesha PPRA kutoa kibali cha mabadiliko na marekebisho (variations) kwa taasisi nunuzi, hivyo taasisi nunuzi haitaruhusu variations bila kibali cha PPRA.

Hivyo itawezesha kudhibiti variations holela zinazoruhusiwa na taasisi nunuzi. Variations imekuwa chanzo kikubwa cha rushwa na upendeleo katika zabuni, kuongeza gharama za mradi kwa minajili ya kujinufaisha binafsi.

Pia marekebisho haya yatapunguza kiwango cha Variations kilichowekwa kwenye Muswada cha 30% hadi 15%. Kitendo cha kuruhusu kiwango kikubwa cha Variations ya 30% ni kuondoa maana nzima ya mchakato wa zabuni na kuendelea kuruhusu ubadhirifu wa fedha za umma.

Ili kuweka ulinzi kiwango cha variations kisizidi 15% na Manunuzi hayo yasifanyike bila kupata kibali cha PPRA.
 
3.7 Ibara ya 74, inayohusu uchaguzi wa njia za Manunuzi Kufanya marekebisho kwa kufuta maneno “kwa kuzingatia taratibu zilizoanishwa katika Kanuni” yaliyomo katika Ibara Ndogo ya (2) na kuongeza mara baada ya Ibara ndogo ya (4) Ibara ndogo ifuatayo “Taasisi nunuzi zitahakikisha zinafanya zabuni kwa njia ya ushindani zikiepuka Matumizi ya njia ya kununua kutoka kwa mzabuni mmoja isipokuwa kwa kibali cha Mamlaka.”

Marekebisho haya yatazuia Matumizi ya njia ya kununua kwa mzabuni mmoja (Single Source) bila kibali cha PPRA,Taasisi nyingi nunuzi zimekuwa zikitumia njia ya Single Source ili kufanikisha mipango yao binafsi ya upendeleo,rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma.

Taarifa ya CAG inathibitisha taasisi nunuzi nyingi zimekuwa zikifanya ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma kwa kisingizio cha Single Source, hivyo marekebisho haya yataongeza jicho la usimamizi na kuziba mianya ya upotevu wa fedha za umma.

3.8 Ibara ya 75, Manunuzi ya raslimali za ndani (Force Account)

Kufanya marekebisho ya kufuta aya ya (b) ya Ibara ndogo ya (3) kwa kuiandika upya kama ifuatavyo:-“(b) thamani ya ujenzi iliyokadiriwa inavuka shilingi Milioni hamsini” na kufuta Ibara ndogo ya (6) Marekebisho haya yatapunguza ujenzi wa miradi kwa kutumia Force Account na pale inapolazimu kiwango cha gharama za mradi kisizidi shilingi milioni 50, hii itapunguza changamoto zinazojitokeza kwa miradi inayotekelezwa kwa njia ya Force Account.

Tumeshuhudia miradi inayotekelezwa kwa Force Account ambayo mingi imeishia njiani, kujengwa chini ya viwango, kuwepo kwa gharama moja nchi nzima, fedha kupotea,walimu na madaktari kuacha shughuli zao za msingi na kubaki kusimamia manunuzi.

Hivyo marekebisho haya yatapunguza kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa miradi ya shule, zahanati, vyoo, vituo vya afya ambayo imetelekezwa na hata inapotokea kujengwa chini ya viwango na gharama kuongezeka anakosekana wa kuwajibika.

3.9 Ibara ya 76, inayohusu Manunuzi ya Dharura

Pamoja na udharura uliowekwa katika Ibara hii, Manunuzi yasifanyike bila kupata kibali cha PPRA.3.10 Ibara ya 77, inayohusu ununuzi wa moja kwa moja kutoka kwa mzalishaji Marekebisho katika Ibara hii kwa kufuta Ibara ndogo (2) na kuandika upya kama ifuatavyo:-

“(2) bidhaa na huduma zitakazonunuliwa kwa mujibu wa kifungu kidogo cha (1) zitakuwa zile tu ambazo zinapatikana kwa muuzaji au mtoa huduma mmoja pekee”

Marekebisho haya yataiwezesha Sheria Kusimama yenyewe badala ya kutegemea Kanuni zitakazowekwa na Waziri, lakini pia itaondoa rushwa, upendeleo na kuwezesha kupatikana kwa bidhaa na huduma kwa bei halisi (Value for Money).

Kwa ilivyo Ibara hii taasisi nunuzi zimepewa mamlaka ya kufanya Manunuzi na ugavi kwa mtoa huduma mmoja hata kama wapo watoa huduma wengine.Hii ni kinyume na msingi wa Sheria ya Manunuzi ambao unataka ushindani katika kumpata mzabuni.

3.11 Ibara ya 78, viwango vya ununuzi vilivyoidhinishwa Kufuta Ibara ndogo ya (3) ambayo inasema “bila kujali kifungu kidogo cha (1) Waziri anaweza kutengeneza Kanuni za Manunuzi wa bidhaa fulani kwa Matumizi ya Serikali bila viwango vya Manunuzi vilivyoidhinishwa”

Marekebisho haya yataondoa mamlaka aliyopewa Waziri ya kutunga Kanuni zinazokinzana na Sheria Mama, na Waziri hawezi kupoka Mamlaka ya Bunge hivyo Ibara hiyo ndogo ya 3 ifutwe.

Mwisho, Waheshimiwa wabunge utatuzi wa matatizo ya nchi yetu uko mikononi mwetu, tuna kila sababu na tunao uwezo wa kuyatatua na kuyamaliza we have the mood, we have the momentum to sustain, we have the ability and applications to overcome it.

Ninawaomba mniunge mkono marekebisho haya yafanyike ili kuwezesha kutungwa sheria yenye nguvu ya kulinda fedha na raslimali za umma, ikawe chachu ya maendeleo na mageuzi makubwa ya uchumi wa nchi yetu, kuhakikishia ustawi wa watu na maisha bora kwa watanzania na ikawe mwanzo na mwisho nchi yetu kugeuzwa Shamba la Bibi.

Nawasilisha,
…………………………
Luhaga Joelson Mpina (Mb)
Mbunge wa Jimbo la Kisesa

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news