EWURA yatoa onyo kali, yafungia vituo vya mafuta

DAR ES SALAAM-Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imevifungia vituo vitatu vya uuzaji mafuta kwa muda wa miezi sita.

Vutuo hivyo ni Camel Oil-Gairo Petrol Station chenye leseni namba PRL 2019-164,PETCOM-Mbalizi Petrol Station chenye leseni namba PRL 2023-025.

Kingine ni Rashal Petroleum Ltd-Mkalama chenye leseni namba PRL 2019-034 huku vitatu vikiendelea kuchunguzwa kwa ajili ya hatua zaidi.

Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt.James Andilile ameyasema hayo Septemba 18, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Dkt.Andilile amesema, hatua hiyo imechukuliwa kutokana na changamoto ya uhaba wa mafuta iliyotokea Agosti na Septemba,2023.

Amesema,baadhi ya wafanyabiashara wenye vituo vya mafuta wamekuwa wakificha mafuta kwa maslahi yao kusubiria bei kupanda, hivyo wananchi kupata usumbufu wa kufanya shughuli zao za kiuchumi.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema,kutokana na ufichaji wa mafuta, EWURA imevichukulia hatua vituo hivyo ambavyo vimejihusisha na tabia ya kuhodhi mafuta ambapo Septemba 4,2023 ilivifungia vituo viwili vya CAMEL Oil Msamvu mkoani Morogoro na Matemba kilichopo Turiani.

Pia amesema kuwa, miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na mamlaka hiyo katika kudhibiti hali ya upatikanaji wa mafuta nchini ni pamoja na kupitia mifumo ya uagizaji na upangaji bei ili kuhakikisha kuna upatikanaji wa mafuta wakati wote.

Dkt.Andilile ameongeza kuwa, pamoja na kuwepo kwa mafuta nchini baadhi ya wafanyabishara wamekuwa wakichukua mafuta na kuchelewesha kufikisha vituoni huku wengine wakiwa na mafuta kwenye visima, lakini hawauzi hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Petroli sura Na. 392 Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA ), imepewa jukumu la kudhibiti masuala ya mafuta pamoja na mambo mengine.

"Lengo ni kuhakikisha kuna upatikanaji wa mafuta wakati wote na imepewa mamlaka ya kuwajibisha vituo vinavyokiuka taratibu za leseni zao,”amesema Mkurugenzi Mkuu huyo.

Wakati huo huo amewataka wafanyabiashara kutambua kuwa biashara ya mafuta siyo holela, kwani leseni zinazotolewa ili kuendesha biashara hizo kwa ustawi bora wa uchumi nchini.

Dkt.Andilile amesema, EWURA inafuatilia utekelezaji wa leseni zilizotolewa ikiwemo kwa wenye maghala,wamiliki wa vituo na wafanyabiashara wa mafuta inapotokea masharti ya leseni hayazingatiwi hatua lazima zichukuliwe.

“Hata kama tukimkuta mdau wa mafuta anafanya kinyume na taratibu za leseni yake kisheria anapewa notisi ya siku 21 ajitetee kwa maandishi na utetezi ukipokelewa wajibu wa EWURA ni kuchambua utetezi pale endapo itajiridhisha pasipo shaka hatua stahiki zitachukuliwa,"amesema Mkurugenzi Mkuu huyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news