Fahamu, kwa nini TanTrade ni zaidi ya Maonesho ya Sabasaba

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imesema, miongoni mwa mafanikio wanayojivunia katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ni pamoja na kufanikisha kusainiwa jumla ya mikataba 46 ya kibiashara yenye thamani ya shilingi trilioni 17.53.
Hayo yamesemwa Septemba 4, 2023 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Latifa Khamis wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini kupitia mwendelezo wa vikao vinavyoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

"Kuna mikataba ya biashara ambayo tumeifunga kupitia matukio mbalimbali, hivyo TanTrade inaendelea kufuatilia mikataba ya makubaliano ya kibiashara ambayo imesainiwa katika matukio mbalimbali.
"Ambapo jumla ya mikataba 46 yenye thamani ya shilingi trilioni 17.53 ikiwemo mikubwa ya bandari imesainiwa, lakini ile ni project ilikuwa ya miaka mitano, hata kabla ya kusaini na ni wizara kwa wizara imesaini na baada ya kukaa kwa umakini sana ndio maana imefanyika kwa mafanikio makubwa.

"Baada ya bandari, kuna miradi mingine mkubwa itakuja. Sisi ndio kazi yetu kutafuta masoko na uwekezaji. Katika mazingira ya sasa lazima tufanye PPP (Ushirikiano wa Sekta Binafsi na Umma) kwani ni muhimu sana."

Kwa nini TanTrade?

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) ilianzishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania namba 4 ya mwaka 2009 iliyofuta Sheria ya Bodi ya Biashara ya Nje namba 5 ya mwaka 1978 na Sheria ya Bodi ya Biashara ya Ndani namba 15 ya mwaka 1973.
Ni iliyopewa mamlaka ya kudhibiti shughuli zinazohusiana na biashara ya ndani na nje ambayo hapo awali ilifanywa na Bodi ya Biashara ya Nje na Bodi ya Biashara ya Ndani.

Aidha, kutungwa kwa sheria ya kuanzisha TanTrade ilikuwa ni hatua kubwa katika kuimarisha mchakato wa mageuzi ya biashara nchini Tanzania. 

TanTrade inawajibika kuendeleza biashara za ndani na nje na kudhibiti maonesho ya biashara ya kimataifa na yanayofanyika Tanzania. 
Lengo la msingi ni kukabiliana na vikwazo vinavyowakabili wafanyabiashara, wauzaji bidhaa nje na wazalishaji wa bidhaa na huduma kwa nia ya kuongeza utendaji wa sekta ya biashara katika uchumi.

Kufuatia kuzinduliwa kwake mwaka 2010, TanTrade imekuwa ikipitia michakato na jitihada kadhaa za kujipanga upya ili kukidhi majukumu mapana ya kuimarisha na kukuza biashara ya ndani na nje pamoja na kudhibiti maonesho ya biashara ya kimataifa yanayofanyika nchini ikilinganishwa na uhamasishaji wa uagizaji na uuzaji nje ya nchi. 

Bi.Latifa ameendelea kufafanua kuwa,mamlaka hiyo itaendelea kusimamia sera na miongozo mbalimbali ya kimaendeleo ili kuleta tija nchini kupitia shughuli mbalimbali.
Miongoni mwa shughuli hizo ni kuratibu maonesho ya biashara, misafara na mikutano ya wafanyabiashara, na kutafiti masoko mbalimbali kwa ajili ya kukuza thamani ya bidhaa za ndani na kuongeza ushindani na bidhaa zinazozalishwa nje ya nchi.

Pia amesema,wamefanikiwa kuratibu matukio mbalimbali ikiwemo programu za utafiti, makongamano na misafara ya kibiashara, maonesho na mikutano ya kuunganisha wazalishaji na wanunuzi ambayo yameongeza makusanyo katika mfuko wa Hazina kwa asilimia 20.15 kwa kipindi cha miaka mitano.

“Katika kipindi cha miaka mitano TanTrade ilipanga kukusanya jumla ya shilingi 52,562,298,340 na imefanikiwa kukusanya shilingi 40,004,650,548 sawa na asilimia 76.
"Ni kutoka vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ruzuku kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya mishahara na miradi ya maendeleo na vyanzo vya mapato ya ndani ikiwemo ada inayotozwa kwenye uratibu na usimamizi wa maonesho, upangaji wakati usio wa maonesho pamoja na ushiriki na viingilio vya Maonesho ya DITF.” 

Amesema kuwa, maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba ambayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka yamezidi kuongeza thamani yake kwa kipindi cha miaka mitano.

Mkurugenzi huyo amesema,kampuni za ndani na nje, washiriki, idadi ya nchi zilizoshiriki maonesho hayo, watembelea maonesho pamoja na ajira zilizozalishwa vimeongezeka na hivyo yamezidi kuongeza wigo wa biashara za ndani na nje ya nchi.

“TanTrade imekamilisha maombi ya ufadhili ya kuendeleza rajamu (branding) ya Taifa ya Viungo (Tanzania Spice Label) kwa kushirikiana na Kituo cha Biashara cha Kimataifa (ITC) pamoja na wadau wa sekta ya viungo.
"Hadi Agosti, 2023 TanTrade imekamilisha rajamu ya iliki, tangawizi, mdalasini, pilipili manga na karafuu vilevile, mamlaka inaendelea na taratibu za kukamilisha rajamu za bidhaa nyingine ikiwemo asali, korosho, kahawa na chai pamoja na mafunzo kwa wafanyabiashara 6,979 kupitia programu 26 ili kuimarisha uwezo wa kujiendesha kiushindani.”

Bi.Latifa amesema, mamlaka hiyo imeendelea kusaka masoko nje ya nchi ya bidhaa mbalimbali zinazolishwa nchini ikiwemo mazao ya biashara na madini ili ziendelee kuongeza wigo wa uzalishwaji na kuongeza thamani ya mnyororo kwa wazalishaji.

Pia, kuongeza fedha za kigeni ambapo mazao na madini hayo ni pamoja na Dhahabu, Korosho, Ufuta, Mbaazi, Kahawa, Dengu, Almasi, vifungashio vya mifuko na Pamba.
Mazao mengine ni Karafuu, Mchele, Soya, Karanga, Parachichi, Pilipili Muhogo, Mahindi, Karafuu, Asali, Mbegu Za Maboga, Korosho, Zabibu na Nyama.

“TanTrade imefanya uchambuzi wa takwimu katika mfumo wa ITC kutambua bidhaa zinazohitajika kwenye masoko mbalimbali duniani.Nchi ambazo zinahitaji bidhaa hizo ni pamoja na India, Umoja wa Falme za Kiarabu, Uswisi, Vietnam, China, Pakistani, Japani, Marekani, Oman, Qatar, Kuwait na Saudi Arabia.”

Amesema, Kampuni ya Akros Cashew ya Tanzania imeuza tani 37 za korosho zenye thamani ya dola za Kimarekani 202,700 kupitia maonesho yaliyofanyika nchini Afrika Kusini.

"Kampuni za Tanzania zilifanikiwa kufanya mauzo ya papo kwa papo yenye thamani ya dola za Kimarekani 100,000 kwa bidhaa mbalimbali za kilimo na pembejeo kupitia msafara wa Malawi.
"Pia,kampuni ziliweza kupata miadi ya mauzo yenye jumla ya thamani ya dola za Kimarekani milioni 20.3 kupitia msafara wa Malawi, lakini pia kwa sasa,taasisi inaendelea kufuatilia utekelezaji wa mikataba na makubaliano ya kibiashara iliyosainiwa katika matukio mbalimbali yaliyoratibiwa na TanTrade.”

Hawatangazi fursa ovyo

"Sisi hatutangazi fursa kama haina vigezo, mara nyingi fursa tunazozitangaza sisi zina vigezo tofauti na matangazo ya taasisi nyingine mtaona wengine wanatangaza fursa ya soko la nazi tu kamaliza, lakini TanTrade inakuwa na maelezo ya kitaalamu."

"Na kama halina maelezo ya kitaalamu hatuwezi kutangaza mpaka tumefanya hivyo kujiridhisha kabisa kikamilifu.
"Eneo hili la mapato ya Mamlaka ya Maendeleo ya biashara mwaka 2022 sisi mapato yetu yana vyanzo vitatu kuna ruzuku kutoka serikalini, hiyo ruzuku ndio tunalipa mishahara, tuna fedha za maendeleo ambazo tumeanza kuzipata mwaka 2022 ambapo tunasimamia miradi.

"Miongoni mwa miradi tunaoufanya ni master Plan ya Uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere, tunapaswa kwenda sambamba na mabadiliko ya ulimwengu, hatuwezi kuendelea kubakia na uwanja ule ule, mabadiliko yamekuwa watu ni wengi tunaendelea na master plan yetu."

"Kwa baadaye itauzwa kama project, watu waje kuwezesha kuwekeza kama mmesikia Rais wa Tanzania ameruhusu PPP, kwangu mimi nasapoti sana hilo wazo."

"PPP ikifanya kazi tutaweza kupata faida kwa sasa tuna document plan kwenye master plan yetu na vyanzo vya mapato ya ndani ni Sabasaba cash cow wetu ni chanzo kikubwa cha mapato, tunavyo vingine vidogo vidogo hatuna OC, lakini tunajiendesha kwa vyanzo hivi vidogo vya mapato tuna advocacy, tafiti."

Vyombo vya habari

Wakati huo huo, TanTrade imeviomba vyombo vya habari nchini kufanya kazi kwa ushirikiano na taasisi hiyo ili kuweza kusaidia kukuza sekta ya biashara.

Lengo ni kuifanya sekta hiyo iwe na tija ikiwemo kutangaza fursa za masoko na bidhaa mbalimbali zinazozalishwa hapa nchini na upatikanaji wa masoko yake kimataifa zijulikane ili wafanyabiashara watumie fursa hizo kujiimarisha kiuchumi na pia kukuza uchumi wa nchi. 

"Kuna umuhimu mkubwa kwetu sisi mamlaka kuendelea kufanya kazi kwa pamoja na vyombo vya habari ili kuweza kuwafikia watu wengi zaidi.

"Na wajue kazi zetu na mambo ambayo tunafanya katika kukuza biashara kitaifa na kimataifa. Kwani, bado usambazaji wa taarifa ni mdogo katika kuwafikia wananchi."
"Tunajua sekta ya habari ni muhimu sana katika kusaidia kuimarisha sekta ya bishara. Kuna kwingine tunaenda tunakuta bado hawana taarifa tunashangaa. 

"Tunatambua kwamba zitakufa sekta nyingine, lakini sekta ya habari haifi itaendelea kuishi, hivyo ni muhimu tukafanya kazi kwa ushirikiano.

"Mmekuwa mnaibua vitu vingi ambavyo vinapaswa kufanyiwa kazi katika kuleta tija na ufanisi, ninyi ni tochi yetu (TanTrade) wahariri na waandishi wa habari mtusaidie katika hili pia ninyi ni tochi ya Serikali hili halina ubishi.

"Uwekezaji wa viwanja vya Sabababa kwa maana ya uwanja mpya kama nilivyosema unaendelea na uko hatua nzuri.Zipo bidhaa na fursa mbalimbali ambazo kupitia vyombo vya habari zitajulika ikiwemo bidhaa kama asali ambayo inafanya vizuri. 

"Tunawakaribisha wote kwenye sekta hii ambayo inafanya vizuri tunashirikiana na ITC, ni mradi ambao unafanya vizuri kibiashara.

Utapeli

Kuhusiana na changamoto ya utapeli ambayo imekuwepo kwa sasa, Bi.Latifa amesema, mamlaka hiyo inalisimamia jambo hili kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuweza kudhibiti zikiwemo mamlaka za kiserikali, lakini pia na vyombo vya habari ameviomba visaidie kutoa elimu kwa umma.
"Suala la utapeli lipo, lakini tunakabiliana nalo kwa kushirikiana na mamlaka zingine za usajili kuhakikisha kama mtu anafanya biashara awe na leseni haya ni mapambano ya kweli, nanyi wanahabari katika hili mtusaidie.

"Pia, bidhaa za Tanzania nje ya nchi zinakabiliwa na changamoto ndogo ndogo kama nilivyosema mtu anapata oda anaipeleka mara tatu ikishafika mara tatu tu anakimbia.

"Shida mtu hana uwezo ni peke yake anakuwa mchoyo, badala ashirikishe na wengine hawezi lazima tushirikiane kuimarisha biashara kupitia taaluma yenu.

"Mbali na hilo, biashara yetu huko nje imekabiliwa na utapeli, kuna baadhi ya watu wanapeleka bidhaa zinakuwa hazina ubora sana mfano zina mawe.

"Lakini, kama mamlaka tumekuwa tunakaa nao lengo letu ni ku-protect image ya nchi yetu iwe nzuri ili bidhaa zetu ziweze kuuzika na kuthaminika.

"Tuna mfumo mama ambao tunao ni vyema mkautumia pia kupata taarifa, changamoto nyingine inayotukabili katika soko la nje ni kutimiza kiwango cha oda mtu anatimiza mara moja mara mbili, mtu akipata pesa anaenda ku-enjoy pesa yake anaachana na biashara bila ninyi kutoa elimu watu hawataweza kubadilika tushirikiane katika hili."
"Najua kuna wahariri upande wa makala za biashara naomba muendelee kutoa elimu juu ya masuala ya utapeli, watu waache wawe waaminifu na waadilifu. Pia, wajenge uzalendo kwani utasaidia sana kuimarisha mahusiano yetu katika biashara mbalimbali.

"Tutaendelea kufanya transformation kwa wale ambao wanafanya vizuri, kwa hiyo atakaye loss...siri ya kazi ni kuwajibika na kujituma."

Tantrade kwa mwaka wa fedha 2023/2024 imejipanga kufanya mambo mbalimbali ikiwemo; kuendelea kuratibu shughuli za utafutaji masoko na ukuzaji biashara ili kuunganisha wazalishaji, kuendelea na taratibu za uanzishwaji wa Dawati la Waambata wa Kibiashara kwenye Ubalozi mbalimbali wa kimkakati wa Tanzania nje ya nchi.

Sambamba na kuendeleza ushirikiano na Ubalozi nje ya Nchi katika kutangaza fursa za masoko ya bidhaa na mazao yanayozalishwa nchini, kuratibu ushiriki wa Tanzania kwenye Maonesho ya Expo 2025 Osaka, Japani.

"Tuna vipaumbele kuhusu Japan kila wizara, kila sekta inaandaa kipaimbele chake, tuna kamati ambayo ni kubwa zaidi, kwani dunia yote itakuwa pamoja katika kijiji kimoja.

"Sisi katika kuji-expor lazima tuwe na mikakati ambayo mpaka sasa tumeiandaa kila wizara itatupa kipaumbele chake, muonekano wa banda la Tanzania utaonekana kwa vipaumbele na mwelekeo wa nchi.

"Anayeingia anaona nini tunakwenda Japan wenzetu wemeendelea sana, tutakuwa na bidhaa za kipaumbele, sekta miradi na project au innovation."

TEF

Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ambaye ni mjumbe wa kamati tendaji wa jukwaa hilo, Nevile Meena amesema kuwa, waandishi wa habari wataendelea kushirikiana na mamlaka hiyo, kwani jukumu lao ni kuujuza umma uweze kutambua. 
"Kwa mfano kuna utapeli umefanyika, mamlaka ina jukumu la kuwaita waandishi wa habari mnawaeleza kile ambacho kimefanyika ama ,amlaka imefanya kudhibiti.

"Wakati wa maonesho nawaomba TanTarade mfanye training ya editors na waandishi, tunapokuwa tunaelekea huko sio mikutano ya nusu siku siku, nazungumzia training muwape elimu wanahabari wawe na uwezo zaidi.

"Katika training mtatueleza mnalenga nini katika maonesho hayo, wanakuja kina nani, mna mpango gani, mnawaandaa wanakuwa na ulewa mzuri wanapokwenda kupeleka ujumbe kwa jamii juu kile kinachofanyika uwe na maana zaidi."
"Kuna kuwa na waandishi ambao watakwenda kutangaza maonesho positively na impact ionekane kwamba ina tija, jambo hili lina umuhimu mkubwa, kwani litaleta ufanisi ambao ndio msingi.

"Nafikiri sana kuna ukaribu kati ya maonesho ya Sabasaba na Nanenane, kuna haja ya kuunganisha mawazo hayo kunapokuwa na maonesho muwaoneshe wakulima fursa ya TanTrade kuweza kuimarisha zaidi kile ambacho kimekusudiwa,"amesema Meena.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news