Jaji Mkuu awahimiza wananchi, wadau kusoma sheria za kazi

NA INNOCENT KANSHA
MAHAKAMA

JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa rai kwa wananchi na wadau mbalimbali nchini kuendelea kujielimisha ili waweze kuzifahamu kwa ufasaha sheria zinazotumika kutatua migogoro ya kazi.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (mwenye tai nyekundu) akizinduzi wa Mfumo mpya wa sheria za kazi kiganjani ‘Labour Law Mobile App’, wakati wa hafla hiyo iliyofanyika leo tarehe 29 Septemba, 2023 katika ukumbi wa mikutano Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi. Wengine wanaoshuhudia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (wa pili kushoto), Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara Mhe. Cyprian Mkeha (wa pili kulia), Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam Mhe. Salma Maghimbi (watatu kushoto), Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Prof. Kennedy Gastorn (wa kwanza kushoto) na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi Mhe. Enock Matembele.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mfumo wa sheria za kazi kiganjani ‘Labour Law Mobile App’, Juzuu ya Maamuzi ya migogoro ya kazi ya Mahakama ya Rufani ‘Court of Appeal Labour law Report’,

Sambamba na uzinduzi wa machapisho ya sheria na kanuni za kazi ‘A compilation of Labour statutes and regulations’, Mhe. Prof. Juma amesema, unapomwezesha mwananchi kuzipata sheria zote za kazi kiganjani ifahamike kuwa mawasiliano ya kisheria ni nguvu.

Amesema, hii itaonesha kwamba Mahakama inamjali mwananchi na kusaidia kukuza imani ya wananchi kwa chombo chao cha utoaji haki vilevile inamwezesha kuipata haki hiyo kwa ukaribu zaidi.

“Siku zote mawasiliano ya kisheria ni nguvu, unapomwezesha mwananchi wa kawaida kupata taarifa muhimu kuhusu mashauri na sheria unampa nguvu kwa sababu silaha ya kwanza ya kupigania haki yako ni uelewa.
Muonekano wa Mfumo mpya wa sheria za kazi kiganjani ‘Labour Law Mobile App’ uliopakiwa sheria zote za kazi hapa Tanzania, Mikataba ya Kimataifa ya sheria za kazi, Sheria za Usalama Mahali pa Kazi (OSHA) pamoja na Sheria za Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).

"Kama unaelewa wa sheria na taratibu, unaelewa wa wapi pa kufungua shauri lako, ndani ya muda gani, kuna utaratibu gani unaotumika huo ndiyo uwezeshaji mkubwa kwa mwananchi,”aliongeza Jaji Mkuu.

Aidha, Prof. Juma alisema , kama taarifa hizo zote za msingi zinapatikana kiganjani zimewezeshwa kwa mwananchi wa kawaida na kwamba kabla ya kukimbilia mahakamani mwananchi anatambua mipaka ya haki zake iko wapi.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Juzuu ya Maamuzi ya migogoro ya kazi ya Mahakama ya Rufani ‘Court of Appeal Labour law Report’ na pia uzinduzi wa machapisho ya sheria na kanuni za kazi ‘A compilation of Labour statutes and regulations’ akishudiwa na Viongozi mbalimbali walihudhuria hafla hiyo (hawapo pichani). Wengine ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (wa kwanza kushoto), Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara Mhe. Cyprian Mkeha (wa pili kulia), Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam Mhe. Salma Maghimbi (watatu kushoto), na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi Mhe. Enock Matembele aliyeshika kisemeo.

Pia, kupima uwezekano wa kushinda ama kutoshinda, uwezeshaji wa namna hiyo unakupa uhuru na uwezo wa kufanya maamuzi ambayo ni muhimu sana juu ya jambo husika.

“Kutokana na zoezi hili naona tunamwezesha mwananchi wa kawaida kupata taarifa zote kiganjani wake na tunapomwezesha kuelewa haki zake vilevile tunapunguza mrundikano wa migogoro katika taasisi zinazotoa haki.

"Kwa sababu mwananchi tayari atakuwa na uelewa, mathalani katika mgogoro wa namna flani sina haki, hivyo hakuna haja ya kuendelea kung’ang’ania kuendelea na mgogoro husika,”aliongeza Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akinyoosha Juzuu hilo juu kuashiria uzinduzi wa Juzuu ya Maamuzi ya migogoro ya kazi ya Mahakama ya Rufani ‘Court of Appeal Labour law Report’ na pia uzinduzi wa machapisho ya sheria na kanuni za kazi ‘A compilation of Labour statutes and regulations’ akishudiwa na Viongozi mbalimbali walihudhuria hafla hiyo (hawapo pichani). Wengine ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (wa kwanza kushoto), Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara Mhe. Cyprian Mkeha (wa pili kulia) na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam Mhe. Salma Maghimbi (wa pili kushoto).

Jaji Mkuu Mhe. Prof Juma aliongeza kuwa, uwezeshaji wa namna hiyo unaleta usawa kwani wanasheria wanapata fedha zao hasa mawakili kutokana na kuuza taarifa za kisheria mfano, pale ambapo mwananchi anatatizo akakutana na mwanasheria na kupewa kiini cha tatizo, atamwambia hilo ni tatizo jepesi sana na kumtaka alipe kiasi Fulani cha fedha ili aweze kusaidia kulitatua.

Jaji Mkuu amesema, mwananchi anapowezeshwa kufahamu sheria inayotumiwa na mawakili, wanasheria na Mahakama inamuweka katika mizani sawa na wanansheria hivyo basi inampa nguvu ya kujiuliza kwa nini amlipe mwanasheria ili apate taarifa ambayo anauwezo wa kuipata kiganjani.

“Wananchi wote wakiweza kuiishi sheria, kuviishi vifungu vya Katiba hapo ndipo tutakuwa na amani ya kudumu kwa sababu kila mtu atakuwa anaelewa mipaka yake, haki zake na kuelewa wajibu wake, hivyo hiki ni kielelezo muhimu sana kutokana na uzinduzi huu,”alisisitiza Mhe. Prof. Juma.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Divisheni hiyo.

Jaji Mkuu Mhe. Prof. Juma akataja faida nyingine za uzinduzi huo kama kielelezo cha kusaidia usuluhishi wa utatuzi wa migogoro mathalani ukichukulia mzigo mkubwa wa migogoro ya kazi inafanywa kwa kiasi kikubwa katika ngazi ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi ‘Commission for Mediation & Abitration’ (CMA).

“Hawa wana kazi kubwa sana ya kutatua migogoro ya kazi kwa kuangalia takwimu kama haya mabaraza upatanishi yasinge kuwepo Mahakama pekee zisingeweza kutatua migogoro ya kazi kwa sababu migogoro mingi inaishia kwenye mabaraza hayo,”alisisitiza Jaji Mkuu.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimpongeza mbunifu wa kuandaa Mfumo mpya wa sheria za kazi kiganjani ‘Labour Law Mobile App' Bi. Lightness Kabaju wakati wa hafla hiyo.

Mhe. Prof. Juma amesema, migogoro ya kazi pamoja na mambo mengine inatoa taswira ya urahisi wa kufanya biashara katika maeneo husika kwa sababu nchi yenye migogoro mingi ya kazi hakuna mwekezaji atapenda kwenda kuwekeza mtaji wake, wala hakuna mfanyabiashara atakae kwenda kuwekeza biashara katika mazingira ambayo siku zote yamegubikwa na migogoro.

Hivyo mabaraza hayo yanasaidia sana katika usuluhishi na upatanishi vilevile wananchi wakipata uelewa wa sheria na taratibu za migogoro ya kazi, kazi za mabaraza zitakuwa nyepesi zaidi kwa kusaidia kuondosha migogoro hiyo, hii itapelekea kujenga taswira chanya na kuimarisha imani ya wananchi na kwa wawekezaji wa ndani na nje.

“Ombi langu ni kwamba tuishi namna sheria inavyoelekeza kwa sababu kuna uwezekano tukawa na sheria nzuri kabisa lakini tabia zetu na mienendo yetu ikawa tofauti kabisa na sheria zilivyo na mara nyingi watu wa nje wanatuangalia kwa kusoma sheria zetu zinasemaje kuhusu migogoro ya kazi na kuziona ni zuri sana ila wanafika wanaona tabia zetu na mienendo yetu haiendani na sheria zetu moja kwa moja wanatudharau, kwamba hatuna utamaduni wa kuheshimu sheria”, aliongeza Jaji Mkuu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi Mhe. Dkt. Yose Mlyambina kitoa historia fupi ya namna watumishi walivyoshiriki ubunifu wa kuandaa Mfumo mpya wa sheria za kazi kiganjani ‘Labour Law Mobile App' pamoja na ubunifu wa uandaaji wa Juzuu na Machapisho mengine.

Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi Mhe. Dkt. Yose Mlyambina ametoa shukrani za dhati kwa Majaji, Wasajili na watumishi wote wa Mahakama Divisheni ya Kazi kwa kushirikiana bega kwa bega kuhakikisha mfumo huo wa wa sheria za kazi kiganjani ‘Labour Law Mobile App’ unakamilika na kuzinduliwa rasmi ikiwa ni ubunifu wa kumsaidia mwananchi kuzifahamu vema sheria za kazi.

“Uazishwaji wa mfumo wa sheria za kazi kiganjani ‘Tz Mobile App’ ni wazo lililotokana na hamasa ya kuibua vipaji vya watumishi wa Divisheni ya Kazi niliyoitoa katika kikao changu cha kwanza tarehe 9 Februari, 2023 katika kikao hicho niliagiza kila mtumishi mwenye wazo zuri lenye manufaa kwa Mahakama na kwa Taifa aandike kwenye ukurasa mmoja wa karatasi au afike ofisini kwangu kunieleza”, amesema Jaji Mfawidhi Mhe. Dkt. Mlyambina

Mhe. Dkt. Mlyambina anasema, katika kikao hicho aliwapa matumaini kuwa Mahakama ipo tayari kuwaunga mkono kwa kila namna ikiwezekana kwa kutoa zawadi kwa mtumishi yoyote ambaye angejitokeza na wazo jipya na chanya hasa kwenye eneo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

“Mwanafunzi wetu wa ndani anayejitolea katika kitengo cha TEHAMA anayeitwa Bi. Lightness Kabaju alifika ofisini akiwa na wazo la kuanzisha Mahakama ya Kazi Kiganjani baada ya mazungumzo niliona ni wazo zuri nikanuia kulitekeleza na sote tulilipokea na kulitekeleza kwakuwa tuliona linalenga kusaidia wadau wetu Mahakama na jamii kwa ujumla ili kupata sheria za kazi kwa pamoja na kwa urahisi zaidi,”ameongeza Jaji Mlyambina.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa kwenye picha ya pamoja na Wadau wa muhimu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi waliohudhuria hafla hiyo.(Picha na Innocent Kansha-Mahakama).

Jaji Mlyambina anasema, mfumo huo mpya wa kiganjani umepakiwa sheria zote za kazi hapa Tanzania, Mikataba ya Kimataifa ya sheria za kazi, Sheria za Usalama Mahali pa Kazi (OSHA) pamoja na Sheria za Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).

Hivyo kwa kupita mfumo huo unaweza kupatikana kupitia simu janja ni wazi kuwa kila mdau anayetafuta sheria za kazi ataweza kuzipata kwa njia rahisi zaidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news