Kiswahili hadi Cuba,kamusi ya Kiswahili na Kihispaniola kutengenezwa

HAVANA-Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Cuba zimesaini Hati za Makubaliano ya kushirikiana kupitia elimu ya juu kwa kubadilishana wakufunzi na wanafunzi, kufundisha lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Havana nchini Cuba na kutengeneza kamusi ya Kiswahili na Kihispaniola.
Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato na Waziri wa Elimu ya Juu wa Cuba Mhe. Dkt. Walter Garcia wakisaini hati ya makubaliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba kupitia elimu ya juu.

Makubaliano hayo yamesainiwa wakati wa hafla ya uzinduzi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Cuba iliyofanyika jijini Havana na kushuhudiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba Mhe. Salvador Valdes Mesa.
Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato na Waziri wa Elimu ya Juu wa Cuba Mhe. Dkt. Walter Garcia wakionesha hati ya makubaliano ya ushirikiano katika elimu ya juu waliyosaini kati ya Tanzania na Cuba wakati wa hafla ya uzinduzi wa Ubalozi wa Tanzania Havana, Cuba.

Makubaliano hayo yamesainiwa na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato kwa niaba ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Waziri wa Elimu ya Juu wa Cuba Mhe. Dkt. Walter Garcia.

Makubaliano mengine yaliyosainiwa ni kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salam kilichowasilishwa na Makamu Mkuu wa chuo hicho Prof. William Anangisye na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Havana Prof. Miriam Garcia.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam Prof. William Anangisye na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Havana Prof. Miriam Garcia wakisaini hati za makubalino ya ushirikiano kati ya vyuo hivyo katika hafla ya uzinduzi wa Ubalozi wa Tanzania iliyofanyika jijini Havana, Cuba tarehe 14 Septemba 2023.

Katika makubaliano hayo Tanzania na Cuba zimekubaliana kushirikiana katika masuala ya kubadilishana ujuzi na uzoefu kupitia wahadhiri, wanafunzi, masuala ya utafiti, sayansi, teknolojia, kufundisha lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Havana na kutengeneza kamusi ya lugha ya Kiswahili na Kispaniola ili kusambaza matumizi ya lugha ya kiswahili nchini Cuba na nchi nyingine zinazozungumza lugha ya kispaniola.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano hayo Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Cuba Mhe. Humphrey Polepole amesema Ubalozi wa Tanzania Havana unajivunia kusainiwa kwa makubaliano hayo ambayo yanatoa mwongozo maalum wa jinsi ya kutekeleza mpango wa kufundisha lugha ya Kiswahili nchini humo.

"Haya ni mafanikio makubwa kwetu, Ubalozi wa Tanzania Havana unajivunia kusainiwa kwa makubaliano haya, sasa yatatoa mwongozo maalum utakaowezesha taasisi husika za elimu ya juu kutekeleza kikamilifu mpango wa kusambaza na kueneza lugha ya Kiswahili nchini Cuba," alisema Mhe. Balozi Polepole.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam Prof. William Anangisye na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Havana Prof. Miriam Garcia wakionesha Hati ya Makubaliano waliyosaini ya ushirikiano kati ya vyuo hivyo katika hafla ya uzinduzi wa Ubalozi wa Tanzania jijini Havana nchini Cuba tarehe 14 Septemba 2023.

Makubaliano yaliyosainiwa ni kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Cuba ambapo Chuo Kikuu cha Havana kilikubaliana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kushirikiana katika masuala ya utafiti, sayansi na Teknolojia na kufanya kazi kwa pamoja ili kutunga Kamusi ya Kiswahili na Kihispaniola.

Makubaliano mengine yaliyosainiwa ni kati ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknojia na Wizara ya Elimu ya Juu ya nchini Cuba ambayo yatawezesha ubadilishanaji wa wanafunzi, wahadhiri na watafiti katika eneo la sayansi na teknolojia ili kuwawezesha wahusika kubadilishana ujuzi na uzoefu katika maeneo hayo na hivyo kuleta tija na ufanisi kwa pande zote mbili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news