Mbinga yaunda majukwaa 48 ya uzwezeshaji wanawake kiuchumi

NA SILVIA ERNEST

HADI kufikia Septemba 13,2023 Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma imeunda jumla ya Majukwaa 48 katika ngazi ya kata na zoezi la kuunda majukwaa hayo ngazi za vijiji na mitaa linaendelea.

Agizo la kuanzishwa kwa jukwaa la uwezeshaji wananchi katika mikoa yote ya Tanzania Bara lilitolewa Juni 6,2016 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan alipokuwa Makamu wa Rais wa Tanzania.

Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Bw.Paschal Ndunguru amebainisha hayo katika hafla ya Uzinduzi wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Wilaya ya Mbinga iliyofanyika katika Kata ya Kitura.

Ndunguru amebainisha kuwa lengo la kuazisha majukwaa hayo ni kutoa elimu za uwezeshaji kiuchumi katika fursa za ndani na nje ya nchi.

"Kupitia majukwaa hayo wanawake wa Wilaya ya Mbinga wanajengewa uwezo wa kujiamini kiuchumi na kuongeza uwezo wa kujitegemea katika ngazi ya kaya,"amebainisha Ndunguru.

Ameeleza kuwa, chimbuko la kuanzishwa kwa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ni malengo ya Milenia 17 ya mwaka 2000 namba 5 ambayo yametaja na kuelekeza uwezeshaji wa wanawake kiuchumi kama nyenzo muhimu ya kuleta maendeleo ya haraka.

Amefafanua kuwa jukumu kubwa ni kuthamini shughuli za uwezeshaji wanawake duniani na kuweka mikakati ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi duniani kote na kuhakikisha kuwa usawa wa kijinsia na ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi unafikiwa ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Idara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Bi.Martina Ngahy ametoa wito kwa wanawake wa Wilaya ya Mbinga kujikita katika Biashara ili kuweza kujikwamua kiuchumi na kuondokana na hali ya utegemezi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news