Naibu Waziri Kikwete atoa maagizo kwa maafisa utumishi

NA LUSUNGU HELELA

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewaagiza Maafisa Utumishi wa Halmashauri zote nchini kuacha tabia ya kukaa ofisini badala yake watembelee ofisi za Watumishi zilizopo katika Kata na Vijiji ili kutatua changamoto za watumishi walioko huko.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Ridhiwani Kikwete akisalimiana na baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda mara baada ya kuwasili wilayani humo kwa ajili ya kuzungumza na kusikiliza changamoto zinazowakabili watumishi hao.

Aidha, Mhe. Kikwete amepiga marufuku tabia ya baadhi ya Maafisa Utumishi kutoa vibali vya kusafiri kwa Watumishi kwenda Jijini Dodoma katika Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa ajili ya kufuatilia masuala yao binafsi ya kiutumishi ilhali kazi hiyo ni ya Maafisa Utumishi hao.
Amesema Watumishi hao hufika Dodoma kwa ajili ya kufuatilia kupandishwa madaraja, kubadilishiwa miundo na kada, kudai malimbikizo ya mshahara, kuwa vitendo hivyo vinawanyima fursa wananchi kuhudumiwa na Watumishi hao waliolazimika kusafiri.

Mhe. Kikwete ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, ikiwa ni siku yake ya tatu ya ziara anayoendelea kufanya mkoani Mara ambapo amewataka Maafisa Utumishi hao kuleta matumaini kwa Watumishi wenzao.

"Acheni ile tabia ya kuonekana miungu watu, tatueni matatizo ya watumishi," amesisitiza Mhe.Kikwete.

Sehemu ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda wakimsikiliza Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Ridhiwani Kikwete wakati akizungumza na leo wilayani hapo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.

Amesema Maafisa Utumishi katika Halmashauri hizo ni lazima watambue wateja wao namba moja ni Watumishi wenzao, hivyo ni lazima wawape kipaumbele katika kutatua changamoto zao ili kupata matokeo makubwa.

"Katika ziara zenu mtakazojipangia za kutembelea vituo vya kazi hakikisheni mnatatua changamoto za watumishi wenu huku mkitumia nafasi hizo kwa kuwapatia taarifa za fursa mbalimbali za kiuchumi na za kujiendeleza kielimu zinazopatikana kwa sasa," amesema Mhe.Kikwete.

Amesema haipendezi kuona hata masuala madogo tu ya kiutumishi yanayowakabili Watumishi wao yanasubiri hadi siku Waziri au Naibu Waziri atoke Dodoma ndo aje kuyatatua.

Amewaeleza Maafisa Utumishi hao ni lazima wahakikishe utendaji kazi zao unakuwa wa kimkakati na sio kufanya kazi kwa mazoea.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mhe. Dkt. Vicent Naano akizungumza kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Ridhiwani Kikwete kuzungumza na Watumishi hao, ikiwa ni ziara yake ya kikazi mkoani humo ya kuzungumza na kusikiliza changamoto zinazowakabili watumishi hao.

Amesema moja ya jukumu la msingi kwa Maafisa Utumishi ni kuhakikisha Watumishi wanaowaongoza wanatatuliwa changamoto zinazowakabili hata ikibidi kufika Dodoma wasisite kwenda.

"Maafisa Utumishi hakikisheni mnajipangia ratiba ya kutembelea vituo vyenu zungumzeni na kusikiliza kero za watumishi, sitegemei nikija tena nisikie changamoto ndogo ndogo kutoka kwa watumishi wenu,"amesisitiza Mhe. Kikwete.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news