MPC yabaini mambo haya ukuaji wa uchumi nchini

NA GODFREY NNKO

KAMATI ya Sera ya Fedha (Monetary Policy Commitee) ya Benki Kuu ya Tanzania imefanya kikao chake cha kawaida cha 227, tarehe 31 Agosti 2023.

Lengo likiwa ni kufanya tathmini ya utekelezaji wa sera ya fedha na kubaini kwamba sera hiyo imewezesha kuendelea kuwepo kwa kiwango cha kutosha cha ukwasi kwa shughuli za uchumi.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amefafanua kuwa, mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kukua kwa kasi kubwa, na hivyo kuendelea kuchangia ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2023.

Aidha,kamati imejadili mwenendo wa uchumi wa dunia na kubaini kuendelea kuimarika, ambapo ukuaji unatarajiwa kufikia asilimia 3 mwaka 2023, ikilinganishwa na makadirio ya awali ya ukuaji wa asilimia 2.8.

Gavana Tutuba kupitia taarifa ya kamati aliyoitoa leo Septemba 1, 2023 amebainisha kuwa,bei za bidhaa katika soko la dunia na mfumuko wa bei vimeendelea kupungua.

"Kutokana na mwenendo huu, benki kuu katika nchi zilizoendelea, hususan Marekani, zimekuwa zikipunguza kasi ya kupandisha riba katika kudhibiti mfumuko wa bei. Mwenendo huo wa uchumi wa dunia unatarajiwa kuimarisha shughuli za kiuchumi hapa nchini."

Wakati huo huo,kamati hiyo imejadili mwenendo wa uchumi hapa nchini na kubaini kwamba Pato la Taifa (GDP) kwa Tanzania Bara katika robo ya kwanza ya mwaka 2023 lilikua kwa asilimia 5.6, sawia na maoteo ya ukuaji wa asilimia 5.2 kwa mwaka mzima wa 2023.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Gavana Tutuba amefafanua kuwa, ukuaji huu ulichangiwa zaidi na shughuli za kilimo, ujenzi na uchimbaji madini.

Aidha, kwa upande wa Zanzibar, uchumi ulikua kwa asilimia 6.8 mwaka 2022, ukichangiwa na huduma za malazi na chakula, mifugo, ujenzi na shughuli za uzalishaji viwandani.

"Mfumuko wa bei umeendelea kupungua na kubakia ndani ya malengo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)."

Amebainisha kuwa, kamati imebaini kwamba, mfumuko wa bei kwa Tanzania Bara umeendelea kupungua kwa miezi
sita mfululizo, na kufikia asilimia 3.3 mwezi Julai 2023 kutoka asilimia 4.9 mwezi Januari 2023.

Kwa upande wa Zanzibar, mfumuko wa bei ulipungua kufikia asilimia 6.7 kutoka asilimia 8.4. Kupungua kwa mfumuko wa bei kumechangiwa zaidi na kushuka kwa bei za bidhaa katika soko la dunia. "Mfumuko wa bei
unatarajiwa kuendelea kuwa wa chini na ndani ya lengo la muda wa kati la asilimia 5."

Gavana Tutuba ameeleza kuwa, kamati imebaini kuwa, ukuaji wa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi ulifikia asilimia 18.8 mwezi Juni 2023, ikilinganishwa na lengo la asilimia 10.3 kutokana na ongezeko la kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi.

"Mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka hadi kufikia asilimia 21.2 katika mwaka ulioishia Juni 2023 ikilinganishwa na lengo la asilimia 10.7.

"Hali hii imetokana na ongezeko la mahitaji ya mikopo kufuatia kuendelea kuimarika kwa mazingira ya biashara na uwekezaji nchini."

Vile vile, mapato ya ndani ya Serikali kwa mwaka 2022/23 yalikuwa ya kuridhisha. Kwa upande wa Tanzania bara, mapato ya ndani yalifikia asilimia 93.2 ya lengo, na kwa upande wa Zanzibar yalifikia asilimia 96 ya lengo.

"Matumizi ya Serikali yaliendelea kufanyika kulingana na mapato." Aidha, kamati imebaini kuwa, sekta ya nje iliathirika kutokana na athari za mwenendo usioridhisha wa uchumi wa dunia uliosababishwa na vita nchini Ukraine, UVIKO-19 na mabadiliko ya tabianchi.

Hali hii ilisababisha kuongezeka kwa nakisi ya urari wa biashara ya nje, kufikia asilimia 6.3 ya Pato la Taifa mwezi Juni 2023 ikilinganishwa na asilimia 4.8 ya Pato la Taifa kwa mwaka ulioishia Juni 2022.

Gavana Tutuba amesema, ongezeko hilo lilitokana na kuongezeka kwa gharama za uagizaji wa bidhaa nje ya nchi.

Kwa upande wa Zanzibar, nakisi ya urari wa biashara nje ya nchi pia iliongezeka kutokana na kuongezeka kwa gharama za uagizaji wa bidhaa.

Hata hivyo, hali hii inatarajiwa kuimarika kutokana na mwenendo wa kuridhisha wa uchumi wa dunia pamoja na hatua zinazotekelezwa nchini kukabiliana na upungufu wa fedha za kigeni, kuimarisha mauzo ya bidhaa na huduma nchi za nje, na kuongeza uzalishaji wa bidhaa mbadala zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.

"Akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kutosha, ambapo kwa mwezi Julai 2023 ilikuwa dola za Marekani milioni 5,338.9, kiwango ambacho kilikuwa kinatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi kwa miezi 4.8."

Kwa upande wa sekta ya kibenki, kamati hiyo imefafanua kuwa,iliendelea kuwa na ukwasi na mitaji ya kutosha. Ubora wa rasilimali za mabenki umeendelea kuimarika.

Ni kufuatia kupungua kwa kiwango cha mikopo chechefu kufikia asilimia 5.3 mwezi Juni 2023, kutoka asilimia 7.8
mwezi Juni 2022. "Hali hii inategemewa kuongeza chachu kwa benki kuongeza utoaji wa mikopo kwa sekta binafsi."

Mbali na hayo,kamati ilijadili changamoto ya upatikanaji wa fedha za kigeni nchini, hususan dola ya Marekani, iliyotokana na athari za mwenendo usioridhisha wa uchumi wa dunia.

"Changamoto hiyo inatarajiwa kupungua kutokana na uwepo wa akiba ya kutosha ya fedha za kigeni itakayosaidia kupunguza uhaba uliojitokeza, kuimarika kwa mwenendo wa uchumi wa dunia, na hatua zinazotekelezwa na Serikali na Benki Kuu katika kukabiliana na upungufu wa fedha za kigeni.

"Kamati inatoa wito kwa sekta binafsi kuongeza uzalishaji ili kuimarisha upatikanaji wa fedha za kigeni nchini."

Vile vile, kutokana na mwenendo wa uchumi wa dunia na wa hapa nchini, Kamati ya Sera ya Fedha iliamua kuendelea na utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kupunguza kasi ya ongezeko la ukwasi.

"Utekelezaji wa sera ya fedha unalenga kuhakikisha kiwango cha ukwasi kinaendana na mahitaji halisi ya uchumi na kufanikisha kufikiwa kwa malengo yaliyoainishwa kwenye programu ya ECF kwa mwezi Septemba 2023,"amesisitiza Mwenyekiti wa kamati hiyo, Gavana Tutuba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news