Rais Dkt.Samia amvua hadhi ya Ubalozi Dkt. Wilbroad Peter Slaa

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan amemvua hadhi ya Ubalozi Dkt. Wilbroad Peter Slaa kuanzia leo Septemba 1, 2023.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu,Zuhura Yunus ambapo imefafanua kuwa, Dkt.Slaa aliteuliwa kuwa Balozi tarehe 23 Novemba, 2017.

Dkt.Slaa ni nani?

Mheshimiwa Dkt.Willibrod Peter Slaa kabla ya uamuzi wa Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kumvua hadhi ya Ubalozi aliwahi kuwa Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Stockholm, Sweden ambapo pia aliidhinishwa kuhudumia nchi za Denmark, Finland, Norway, Iceland, Estonia, Latvia, Ukraine na Lithuania kati ya mwaka 2017 hadi Septemba 2021.

Dkt.Slaa aliyezaliwa Oktoba 29, 1948, kabla ya hapo aliwahi kuwa mtumishi wa Mungu, Mbunge wa Jimbo la Karatu na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Hapo awali aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho kuanzia mwaka 1998 hadi 2002 na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho.

Dkt.Slaa ana sifa mbalimbali za kitaaluma, ikiwa ni pamoja na PhD ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha St.Urban cha Roma, Italia, mwaka 1977.

Mwanasiasa huyo aliwahi kwenda Seminari ya Kipalapala mkoani Tabora, ambapo alipata cheti cha Theolojia mwaka 1977 na Shule ya Seminari ya Kibosho mkoani Kilimanjaro, ambapo alipata cheti cha falsafa mwaka 1973.

Kati ya mwaka 1992 na 1998, Dkt.Slaa alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanzania Society for the Blind. Mwaka 1985 hadi 1991, alikuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) na kati ya 1982 na 1985, alikuwa Mkurugenzi wa Maendeleo Dayosisi ya Mbulu.

Kwa nini avuliwe hadhi?

Mkataba wa Vienna Convension on Diplomatic Relations of 1961 Ibara ya Tatu imezifafanua kwa kina kazi za Balozi ambaye ameaminiwa na Mkuu wa Nchi kwa ajili ya kwenda kuliwakilisha Taifa lake katika nchi nyingine.

Miongonin mwa kazi hizo ni; (a) Kuiwakilisha nchi iliyomtuma (Sending State) ndani ya nchi husika itakayompokea (Receiving State).

(b) Kulinda maslahi ya nchi (dola) iliyomtuma ndani ya nchi iliyompokea pamoja na ya raia wake, bila ya kuathiri mipaka aliyowekewa kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

(c) Kujadiliana (negotiating) na serikali ya nchi iliyompokea (katika mambo mbalimbali yenye maslahi baina yao). Kwa niaba ya Rais.

(d) Kuenenda na taratibu zote za kisheria katika kufuatilia yanayojitokeza ndani ya nchi iliyompokea na kutolea taarifa yale yanayojiri kwa nchi iliyomtuma.

Aidha. kanuni hii inawakataza mabalozi kujihusisha na masuala ya siasa ya ndani ya nchi.

(e) Kuendeleza mahusiano ya kirafiki kati ya nchi iliyomtuma (Sending State) na nchi na inayompokea, kuendeleza mahusiano ya kiuchumi, kiutamaduni na kisayansi.

Aidha, Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 umetoa muongozo wa nani mwenye mamlaka ya kumvua balozi hadhi yake.

Ibara ya 32 ibara ndogo ya kwanza ya mkataba huu inaeleza kuwa, kinga ya mashitaka ambayo balozi hupewa huweza kuondolewa na nchi iliyomtuma (Sending State) tu.

Kwa mujibu wa maelezo ya ibara hiyo tunaona kuwa nchi iliyomtuma balozi kwenda kuwakilisha ndiyo yenye haki ya kuweza kumvua balozi hadhi yake.

Kwa mujibu wa Ibara ya 36 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inaeleza kuwa, Rais atakuwa na madaraka ya kuteua watu kushika nafasi za madaraka ya viongozi wanaowajibika kuweka sera za idara na taasisi za Serikali.

Sambamba na watendaji wakuu wanaowajibika kusimamia utekelezaji wa sera za idara na taasisi hizo katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, nafasi ambazo zimetajwa katika sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge kwamba zitajazwa na uteuzi unaofanywa na Rais.

Aidha, kutokana na ibara hii ya 36 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunaona kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye mwenye mamlaka ya kumteua mtu yeyote kuwa Balozi kuiwakilisha nchi.

Pia kama mwakilishi wa Rais katika nchi na vivyo hivyo ana haki ya kumvua hadhi ya ubalozi na hata kutengua uteuzi wa mtu yeyote endapo kutakuwa na hitajio la kufanya hivyo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Ibara ya 36 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inajibu swali la nani mwenye mamlaka ya kumvua hadhi ya ubalozi na kutengua uteuzi wa balozi yeyote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lililotokana na maelezo yaliyopo kwenye Ibara ya 32 (1) ya Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961.

Ni mkataba ambao unahusu Mahusiano ya Kidiplomasia ambayo inaeleza kuwa, kinga na hadhi ya ubalozi huweza kuondolewa na nchi iliyomtuma balozi (Sending State).

Sending State kidiplomasia unazungumzia mkuu wa nchi husika ambaye ilimteua balozi mtajwa na hivyo kwa mamlaka aliyo nayo kikatiba anaweza kumuondoa balozi huyo ama kumvua hadhi kama Mheshimiwa Rais Dkt.Samia alivyofanya leo kwa Dkt.Slaa.

Kumbukumbu

Novemba 5, 2028 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt John Pombe Joseph Magufuli (kwa sasa hayati) alitengua uteuzi na kumrejesha nchini aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada, Bw.Alphayo Japani Kidata na kuondolewa hadhi ya Ubalozi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news