Mwalimu kizimbani kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi

NA FRESHA KINASA

MWALIMU Joseph Otindo Lucas mwenye umri wa miaka 34 anayefundisha katika Shule ya Msingi Kambarage 'A' iliyopo Katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara na kusomewa shitaka la kumbaka mwanafunzi.

Ni mwanafunzi wa darasa la sita (jina limehifadhiwa) mwenye umri wa miaka 11 anayesoma katika shule hiyo.

Mtuhumiwa huyo amefikishwa katika Mahakama hiyo leo Septemba 11, 2023 na kusomewa shitaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Khadija Masala.

Mwendesha mashitaka upande wa Serikali, Ngowi Zerubabel ameiambia mahakama hiyo kuwa mtuhumiwa huyo anashitakiwa kwa kumbaka kwa nyakati tofauti mwanafunzi huyo (jina limehifadhiwa) katika maeneo ya Shule ya Sekondari Songe iliyopo katika Manispaa ya Musoma tarehe tofauti tofauti za mwezi Agosti 2023.

Imedaiwa, mtuhumiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 130 (1), ( 2) (e) na kifungu cha 131 (1) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.

Baada ya kusomewa shitaka hilo, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Khadija Masala alimtaka Mtuhumiwa huyo kujibu kuhusiana na shitaka hilo linalomkabili. Ambapo mtuhumiwa huyo Joseph Otindo Lucas amekana shitaka hilo.

Mwendesha mashitaka upande wa serikali Ngowi Zerubabel ameiambia mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo tayari umekamilika.

Aidha, Hakimu Mkazi Mwandamizi Khadija Masala ameiambia mahakama hiyo kuwa dhamana kwa mtuhumiwa huyo iko wazi baada ya kukana shitaka hilo.

Amesema, mtuhumiwa anapaswa kudhaminiwa na watu wawili ambao wanakidhi masharti ikiwemo kila mmoja kuwa na bondi yenye thamani ya shilingi milioni 2 ya mali isiyohamishika.

Mtuhumiwa huyo amekidhi masharti ya dhamana kwa kuwa na wadhamini wawili ambao ni watumishi (waajiriwa) jambo ambalo Hakimu Mkazi Mwandamizi Khadija Masala amekubaliana nalo kwa kusema kuwa, mtumishi na cheki namba zinatosha kudhamini.

Mtuhumiwa huyo Joseph Otindo Lucas ameachiwa huru kwa dhamana ambapo wadhamini wake wamepewa masharti kuwa mtuhumiwa waliyemwekea dhamana anapaswa kufika mahakamani hapo kila tarehe ya kesi inapopangwa hadi ifikie mwisho.

Ameongeza kuwa, iwapo mtuhumiwa atashindwa kufika mahakamani wadhamini hao watapaswa kufika mahakamani hapo.

Aidha, Hakimu Mkazi Mwandamizi ameliahirisha shitaka hilo mpaka Septemba 26, 2023 ambapo litatajwa kusomwa hoja za awali kwa kuwa upelelezi umekamilika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news