NSSF inalipa mafao zaidi ya michango-Mkurugenzi Mkuu

NA GODFREY NNKO

"Kimsingi ni kwamba, NSSF inalipa mafao ambayo yanazidi sana michango, ukijumlisha michango yako yote mpaka unastaafu...unalipwa zaidi.
"Sasa mfuko ili uweze kutimiza hilo, lazima uwekeze na ndilo jukumu lingine kubwa la NSSF na mifuko yote ya jamii.Lakini, pia tunalipa mafao na hili unaweza kusema ndilo jukumu kubwa."

Hayo yamesemwa Septemba 25, 2023 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Kupitia kikao hicho, Mshomba mbali na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira rafiki ya uwezaji hapa nchini, hivyo kusaidia mfuko huo kuendelea kusajili idadi kubwa ya wanachama wake.

Pia, amempongeza Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu kwa ubunifu wake ambao umewezesha taasisi na mashirika yaliyopo chini ya ofisi yake kujitokeza na kuelezea mafanikio yake kwa umma kupitia wahariri na waandishi wa habari nchini.

NSSF ulianzishwa mwaka 1964 kama kitengo ndani ya Wizara ya Kazi kinachoshughulikia mafao ya wafanyakazi baada ya kustaafu. Mwaka 1975,kitengo hicho kiliboreshwa na kuwa taasisi inayojitegemea iliyoitwa National Provident Fund (NPF).

Aidha, maboresho zaidi yalifanyika mwaka 1997, ambapo Sheria Na. 28 ilitungwa na kuibadili NPF kuwa Mfuko wa Pensheni, hivyo kuwezesha kuwa na wigo mpana wa kutoa huduma za hifadhi ya jamii kwa wafanyakazi.
Mwaka 2018 Serikali ilifanya maboresho ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii yaliyosababisha kurekebishwa kwa Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii, (The National Social Security Fund) Sura ya 50.

Uamuzi huo uliifanya NSSF kuwa mfuko pekee unaohudumia hifadhi ya jamii kwa wafanyakazi wa sekta binafsi na wale wa sekta isiyo rasmi nchini.

Vile vile,Mshomba amesema, mazingira wezeshi na rafiki ya biashara nchini licha ya kuwaongezea wanachama pia yamesaidia kukuza mchango wa mfuko huo.

Amesema, kati ya Machi Mosi, 2021 na Juni 30, 2023, waliandikisha jumla ya wanachama 547,882 ambapo idadi ya wanachama wachangiaji iliongezeka kwa asilimia 36.

Ni kutoka 874,082 Machi Mosi, 2021 hadi kufikia wanachama 1,189,222 Juni 30, 2023 ikichangiwa na mkakati wa Serikali wa kuvutia wawekezaji, pamoja na utekelezaji wa mpango wa mfuko katika uandikishaji wanachama.
Amesema,wanachama wachangiaji katika mfuko wameongezeka kwa asilimia 26 hadi kufikia wanachama wachangiaji 1,189,222 tarehe 30 Juni 2023 ikilinganishwa na wanachama wachangiaji 945,029 waliofikiwa tarehe 30 Juni 2021.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, katika mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2023,makusanyo ya michango kwa mwezi uliongezeka kutoka shilingi bilioni 97.67 iliyofikiwa Machi Mosi,2021 hadi kufikia shilingi bilioni 143.05 kwa mwezi katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30,2023.

“Ongezeko hili limechangiwa na kuongezeka kwa waajiri wanaoleta michango kwa wakati na mazingira mazuri ya ufanyaji biashara kwa sekta binafsi.”
Aidha, Mshomba amesema,makusanyo ya michango kwa mwaka yameongezeka kwa asilimia 43 hadi kufikia shilingi bilioni 1,718.28 katika mwaka ulioishia Juni 30,2023 ukilinganisha na shilingi bilioni 1,201.05 zilizokusanywa katika mwaka ulioishia Juni 30,2021.

Uwekezaji

“Uwekezaji wa Mfuko (investment portfolio) iliongezeka kwa asilimia 111 kutoka shilingi bilioni 3,395.46 tarehe 1 Machi 2021 hadi kufikia shilingi bilioni 7,153.23 tarehe 30 Juni 2023 ikichangiwa na kukua kwa thamani ya vitega uchumi, michango ya wanachama na mapato ya uwekezaji.”

Pia, amesema thamani ya vitega uchumi vya mfuko imekua kwa asilimia 55 hadi kufikia shilingi bilioni 7,153.23 tarehe 30 Juni 2023 kutoka shilingi bilioni 4,622.25 zilizofikiwa tarehe 30 Juni 2021.
Mshomba ameendelea kufafanua kuwa, wastani wa mapato ya uwekezaji kwa mwezi katikamwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2023, yalifika shilingi bilioni 72.06 ikiwa ni ongezeko la asilimia 92 ukilinganisha na shilingi bilioni 37.35 zilizokusanywa mwezi Machi 2021.

Aidha, mapato halisi (real rate of return on investment) ya mfuko, amesema yameongezeka kutoka wastani wa asilimia 3.31 mwezi Machi 2021, hadi kufikia asilimia 5.32 kwa kipindi kilichoishia tarehe 30 Juni 2023.

“Mapato ya uwekezaji kwa mwaka yameongezeka kwa asilimia 93 na kufikia shilingi bilioni 864.76 katika mwaka wa fedha ulioishia 30 Juni 2023 ukilinganisha na shilingi bilioni 448.17 zilizokusanywa katika mwaka wa fedha 30 Juni 2021.”
Vile vile amesema,katika mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2023,mfuko ulilipa shilingi bilioni 61.93 kwa mwezi kama mafao kwa wanufaika mbalimbali ikiwa ni ongezeko la asilimia 22 ukilinganisha na shilingi bilioni 50.58 zilizolipwa kwa mwezi kipindi kilichoishia tarehe 1 Machi 2021.

“Ongezeko hili lilichangiwa na kuongezeka kwa madai ya fao la upotevu wa ajira (unemployment benefit) na mkupuo maalum (special lumpsum).”

Aidha, Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, malipo ya mwaka ya mafao kwa wanufaika mbalimbali wa mfuko yaliongezeka kwa asilimia 25 na kufikia shilingi bilioni 743.17 katika mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2023 ukilinganisha na shilingi bilioni 594.33 zilizolipwa katika mwaka wa fedha ulioshia tarehe 30 Juni 2021.
“Siri ya mafanikio ni pamoja na mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wake Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sera nzuri za kuvutia wawekezaji, pamoja na utekelezaji wa mpango wa mfuko katika uandikishaji wanachama na matumizi ya TEHAMA,” amesema.
Dege Eco Village

Amesema kuwa, katika mwaka wa fedha 2023/24, mfuko huo unatarajia kuuza mradi wa Dege Eco Village wenye eneo la ekari 302 ambapo mradi huo una nyumba 3,750 zilizokuwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, hadi Oktoba 31, mwaka huu mfuko huo utakuwa umekamilisha hatua zote za uuzaji wa Mradi wa Dege Eco Village kwa karibu dola milioni 220 za Marekani.

Dege Eco Village ni mradi wa shirika hilo uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam ambao unapata mteja ikiwa ni baada ya ujenzi wake kusimama tangu Januari 2016.

Mshomba amesema,mradi huo umeuzwa kama ulivyo, ikiwa ni utekelezaji wa uamuzi wa Bodi ya Mfuko na Serikali ili kurudisha fedha za wanachama zilizowekezwa awali katika mradi huo.
“Mradi huu umeuzwa kama ulivyo, ikiwa ni utekelezaji wa uamuzi wa Bodi ya Mfuko na Serikali ili kurudisha fedha za wanachama zilizowekezwa awali katika mradi huu.

“Kwa sasa Mfuko kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali unakamlisha taratibu za zabuni baada ya kukamilika kwa hatua ya tathmini ya zabuni na maafikiano ya bei. Matarajio ni kusainiwa kwa mkataba wa mauzo ya mradi huu kabla ya tarehe 31 Oktoba 2023,”amesema.

Kwa mujibu wake, hadi uamuzi wa kuuzwa mradi huo unafikiwa tayari ulikuwa umeshatumia zaidi ya shilingi bilioni 330 huku akieleza kuwa kwa mnunuzi waliyempata watakuwa wamepata faida.

"Kwa sasa mfuko kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali unakamlisha taratibu za zabuni baada ya kukamilika kwa hatua ya tathmini ya zabuni na maafikiano ya bei. Matarajio ni kusainiwa kwa mkataba wa mauzo ya mradi huu kabla ya tarehe 31 Oktoba 2023," amesema Mshomba.

Kiwanda cha Sukari

Wakati huo huo,Mkurugenzi Mkuu huyo ameema kuwa,Mradi wa Kiwanda cha Sukari Mkulazi uliopo Mbigiri Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro ambao unamilikiwa kwa ubia kati ya NSSF asilimia 96 na Jeshi la Magereza asilimia nne unatarajiwa kukamilika mwezi ujao.
“Ukubwa wa shamba la mradi huu ni hekta 4,856 (ekari 12,000) na kiwanda kinatarajiwa kuzalisha tani 50,000 za sukari kwa mwaka. Jumla ya gharama za mradi ikijumuishwa na thamani ya ardhi inatarajiwa kuwa shilingi bilioni 344.47.

“Hadi kufikia Juni 30, 2023 utekelezaji wa mradi kwa upande wa mashamba ya miwa ulifikia asilimia 86 na upande wa kiwanda ulifikia asilimia 93.

"Gharama zilizokwishatumika katika mradi huu ni asilimia 88 ya gharama zote na mradi huu unatarajiwa kukamilika na kuanza uzalishaji wa sukari mwishoni mwa Oktoba 2023.

“Mradi huu utaongeza mapato ya mfuko, uzalishaji wa sukari nchini, mapato ya kodi wa Serikali na kuongeza ajira zipatazo 11,315 nchini,”amesema Mkurugenzi Mkuu huyo.

Maboresho

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, mfuko umefanya maboresho mbalimbali ya mifumo ya utendaji kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Amesema, baadhi ya maboresho yaliyofanyika ni kuanzishwa kwa mfumo wa kujihudumia kwa ajili ya waajiri (Employer Portal), mfumo wa kujihudumia kwa ajili ya wanachama (Member Portal) na mfumo wa ukaguzi wa wanachama (Inspector Portal).

“Mfuko umeendelea kuimarisha mifumo na usimamizi wa fedha ili kuepuka mianya ya upotevu wa fedha, kuendelea kumudu gharama za uendeshaji pamoja na kulipa mafao stahiki kwa wastaafu na wanufaika wengine,”amesema Mkurugenzi Mkuu huyo.

Pia amesema,kwa mujibu wa taarifa za ukaguzi,mfuko umekuwa ukipata hati safi kutokana na kaguzi zilizofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

"Hati Safi za mkaguzi zinathibitisha kuwa fedha za wanachama zipo salama,"amefafanua Mkurugenzi Mkuu huyo wa NSSF.

Vile vile, Mshomba amesema, mfuko umefanya mapitio ya Mpango wa Utoaji wa Huduma za Hifadhi ya Jamii katika Sekta isiyo rasmi (NISS).

Amesema, hatua hii ilitokana na Mpango wa NISS kukosa mafao na huduma za zinazowavutia wananchi walio katika sekta isiyo rasmi kujiunga na mfuko.

Pia, amesema maboresho ya mpango huo yanalenga kukidhi haja na matakwa ya wananchi ambapo kuandaliwa na kuidhinishwa kwa muongozo wa uendeshaji wa NISS utasaidia kuongeza wigo wa wanachama, mapato kwa mfuko na kutoa fursa mbalimbali kwa sekta isiyo rasmi.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, mpango wa NISS ulioboreshwa unatarajiwa kuzinduliwa rasmi na kuanza kutumika kabla ya Julai, 2024.

Miradi iliyosimama

Mshomba amesema, mfuko unatekeleza miradi mitano ukiwemo wa nyumba za makazi za Dungu, Toangoma, Mtoni Kijichi, jengo la kibiashara na makazi la Mzizima Towers na hoteli ya kitalii yenye hadhi ya nyota tano jijini Mwanza.
Amesema kuwa, changamoto na kasoro za kizabuni na kimikataba zilizokuwepo zilipelekea miradi hiyo kusimama mwaka 2016.

“Miradi hii imepitia hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanyiwa mapitio na kufanyiwa kaguzi maalum ikiwepo ile ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) iliyokamilika mwishoni mwa mwaka 2020.

“Katika kipindi kilichoanzia Machi Mosi, 2021 mfuko ulitatua changamoto zilizokuwepo na kwa sasa utekelezaji wa miradi yote unaendelea na miradi hii inatarajia kukamilika kati ya Juni na Septemba, 2024,"amesema Mkurugenzi Mkuu huyo.

Waajiri

Mkurugenzi Mkuu huyo ameeleza kuwa, ukiukwaji wa taratibu na kanuni za usajili wa wanachama na uwasilishaji wa michango yao kutoka kwa waajiri na kuwasilisha michango iliyo chini ya mshahara halisi wa mtumishi, umekuwa mojawapo ya changamoto kubwa kwa mfuko huo katika kufikia malengo yake ya kutoa huduma bora kwa jamii.

Amesema, wapo waajiri ambao hawatoi mikataba ya ajira kwa watumishi wao, hivyo wanaandikisha wanachama wachache kuliko waliopo kwenye ajira.

Mshomba amesema kuwa, kutowasilishwa kwa michango ya wanachama kwa wakati inayopelekea ufinyu wa makusanyo na uwekezaji na mapato yatokanayo na uwekezaji.

TEF

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Deodatus Balile amependekeza elimu itolewe zaidi kwa waajiri juu ya umuhimu wa kupeleka michango ya watumishi wao kwa wakati NSSF.
Vile vile ameipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kuanzisha utaratibu huu wa mashirika na taasisi zilizopo chini yake kukutana na wahariri ili waweze kuelezea umma mambo mbalimbali wanayoyatekeleza.

"Utaratibu huu wa wahariri na vyombo vya habari kuzungumza na watendaji wa Serikali na taasisi zake, siyo tu unasaidia Serikali kufikisha ujumbe kwa wananchi,lakini pia Serikali kupokea mrejesho kutoka kwa wananchi.

"Nguvu ya vyombo vya habari, nguvu yake ipo ni kwamba tunakutana viongozi wakubwa kama tulivyokaa na ninyi mpaka wale wa chini."
Pia, Balile ameipongeza NSSF kwa mafanikio makubwa ambayo wameyapata, "Lakini, pia nikupongeze kwa ongezeko hili kutoka shilingi trilioni 5 mpaka trilioni 7, kuongeza wachangiaji kutoka laki nane mpaka milioni 1.1 pia kupata mwekezaji Dege Eco Village kwa sababu ni mradi ambao ulitajwa kuwa na kesi nyingi za kutosha, kiasi kwamba wengi wangeukimbia.

"Na mimi niombe sana, hata mimi msinieleze mpaka mtakapokuwa mmemaliza kuuza, ndipo na mimi mnijulishe, lakini kwa kweli ninawapongeza sana, na huu mradi wa Kiwanda cha Sukari ni mradi ambao kwa kweli utaleta si tu heshima, lakini nchi yetu itakuwa na uhakika wa sukari, kwa hiyo ni jambo jema sana."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news